BRYSON MSHANA, MTWARA
SHIRIKA la kimataifa la Search for Common Ground linalojishughulisha na uhamasishaji wakutunza amani katika jamii, na kufadhiliwa na umoja wa Ulaya (European Union) kwa takriban miezi 30 iliyopita limekuwa likiwajengea uwezo wadau mbalimbali katika mkoa wa Mtwara kuendeleza na kutunza amani Nchini.
Mradi wa Jenga Amani Yetu, ulianza mwaka 2020 ikitekelezwa maeneo ya Mtwara, Tandahimba, Pwani (RUFIJI), Tarime na Zanzibar lengo ikiwa ni kujenga ushirikiano kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali, Vyombo vya habari na viongozi wa serikali katika kuangazia matatizo yanayohusishwa na migogoro ikiwemo vyanzo vya migogoro katika maeneo hayo na nafasi ya washirikishwaji hao katika kutatua tatizo.
Makundi haya ya waandishi wa Habari, viongozi wa serikali, viongozi wa dini na asasi za kiraia yalipewa kipaombele kutokana na ushawishi unaowezesha kutoa nafasi kwa jamii nzima kuzungumzia maswala ya migogoro.
Mradi huu umebadilisha mtazamo wa watu mbalimbali katika jamii walivyokuwa wanafikiri juu ya utatuzi wa migogoro, ambapo wanufaika wanakiri kuwa wameona umuhimu wa kuepuka migogogoro na machafuko, na kutatua changamoto zinazojitokeza kwa njia shirikishi.
Husna Hassan ni mwandishi wa habari anayefanya kazi katika kituo cha safari redio mjini Mtwara, ambaye anaeleza kuwa mradi wa “jenga amani yetu” umemuwezesha kujua namna ya kutatua migogoro kwa kutumia kazi yake.
“Mwanzoni sikua naelewa chochote, nilikuwa nikisikia mahali kuna mgogoro mfano wa ardhi naenda narekodi na kurusha kama vilivyo, sasa nimepata mafunzo kupitia mradi wa jenga amani yetu ambayo yamenisaidia kuchuja habari zangu na kuziripoti kwa namna ya kutatua na sio kuchochea migogoro”
“Jenga amani yetu haibadilishi miongozo yako ya kiuandishi, bali inakusaidia kuiboresha na kuripoti kwa namna ambayo hata jamii inayozozana ikisikia, kusoma au kutazama habari yako inajirekebisha yenyewe” amesisitiza Husna Hassan.
Ameongeza kuwa kupitia mradi wa jenga amani yetu amejua aina ya migogoro na namna ya kuitatua, wakati kabla hakuwa na uelewa mkubwa na migogoro mingi alikuwa haifanyiii kazi maana alikuwa anaichukulia kawaida.
“Lakini pia nimejua Aina ya migogoro kwasababu kabla ya kupata mafunzo kuna migogoro ambayo mimi kama mwandishi nilikuwa naiyona na kuipotezea kwakujua ni maisha yetu ya kawaida kumbe ni sababu ambayo inaweza kuvunja amani”
Naye Grace Hamis kutoka kituo cha Radio Jamii FM cha Naliendelea Mtwara, anasema mradi wa “jenga Amani Yetu” umembadilisha yeye binafsi kimtazamo na namna ya kuitazama migogoro kuanzia katika ngazi ya familia.
Grace anaeleza kuwa wasikilizaji na jamii wanaelewa kuwa migogoro ni ile inayohusisha mataifa, jamii kama wakulima na wafugaji au ugaidi jambo ambalo amegundua kwamba sio sawa baada ya kushiriki mradi.
“uelewa wangu juu ya migogoro nilidhani ni ile mikubwa tunayosikia mfano Israel na Palestina, kumbe ni tofauti kabisa na baada ya mafunzo niliyoyapata wakati wa mradi nilipata uelewa mkubwa na mimi nasaidia sasa kuielemisha jamii inayonisikiliza katika vipindi vyangu”
“Mwisho nimejua kuwa pasipo amani hakuna maendeleo kwa familia,jamii na nchi kwa jumla kitu ambacho jamii yetu haina uelewa wa kutosha juu ya hilo na mm kama mnufaika wa mradi inanipasa kuweka nguvu kwaajili ya kutoa elimu juu ya kuimarisha amani katika Jamii zetu ili kukua kimaendeleo” amesisitiza Grace Hamis.
Abdallah Nassoro ambaye ni mwandishi wa habari wa IPP Media Mtwara, amesema kuwa mradi umemsaidia kubaini maeneo yenye migogoro na kumuonyesha namna ya kufanya kazi ya uandishi wa habari kwa njia ya kuleta suluhu.
“kuna mambo ambayo mtu unajua hakuna shida na kuna amani lakini ukishaingia kwenye mafunzo haya ndio yanakufungua kujua kipi ni mgogoro na ukubwa wake hivyo ni ukweli kuwa kupitia mradi huu nimejifunza mambo ambayo shuleni sikuyapata” amemalizia Nassoro.
Naye Kassim Chikwenga kutoka kundi la mashirika yasiyo ya kiserikali anashuhudia kuwa kupitia mradi wa “Jenga Amani Yetu” kumeongezeka wigo wa utendaji kazi katika taasisi mbalimbali zilizopo kwenye mradi jambo ambalo limeonyesha tija kubwa.
“huwezi kujua kila kitu, lakini miradi kama hii inatufungua sana kutokana na upekee wake hususan huu wa kuhamasisha amani katika jamii ni mambo ambayo unaweza ukayafanyia kazi hata katika ngazi ya familia. Kassim Chikwenga
Bw. Shaahari Hamis ni muwakilishi kutoka katika kundi la watendeji wa serikali za Mitaa kutoka kata ya Shangani Manispaa ya Mtwara Mikindani Mkoani mtwara, anayekiri kuwa mradi umesaidia katika kutatua migogoro mbalimbali ya jamii wanazoziongoza.
“Ukiwa kiongozi hususan katika ngazi ya kata kama nilivyo mimi migogoro inaripotiwa kila siku, hivyo kupitia mradi huu nimejikuta natatua na kuzuia migogoro kiurahisi tofauti na zamani jambo ambali naliona kuwa ni mafanikio makubwa kwangu”
“Awali ilikuwa kesi za migogoro zikifika ofisini natatua kwa mazoea na wakati mwingine kwa maelekezo ya kimamlaka niliyo nayo kazini, lakni mradi wa “jenga amani yetu” umenionmgezea uzoefu naweza kutatua mgogoro kwa kuwatajia wahusika mfano tu ambao niliusikia ukitolewa na mwalimu wakatikuta wanacheka na kushikana mikono”
“Japo mradi utamalizika lakini mm najivunia kushiriki mmoja wa miradi michache ambayo jamii inaweza kuendelea kufanyia kazi yale yaliyokuwepo kwenye mradi” amemalizia Shaahari Hamis
Sheikh mkuu wa Mkoa wa Mtwara Nurdin Mangochi anaeleza umuhimu wa jamii kuepuka migogoro inayoweza kusambaratisha amani ambayo ikishatoka ni nadra kurudi tena.
“Viongozi wa dini tunalo jukumu kubwa sana la kuunga mkono juhudi za wadau katika kutunza amani, ukaribu wetu na waumini tunapaswa kuutumia katika kujenga amani na kuwasisitiza juu ya kuepuka migogoro”
“hii migogoro mnayoisikia mikubwa ilianza kidogokidogo tu, hata wao hawakujua kama ingefikia ilipo sasa sisi kwa kuwa tayari tunayo mifano basi tujitahidi sana kuhakikisha kwamba tunahubiri amani katika kila eneo”
“Nimefurahi kuusikia huu mradi Yetu wa kujenga amani, nimejisikia vizuri kuuzungumzia pia na naamini waumini wengi na jamii imefikiwa na matokeo yake yatakuwa yameshaanza kuonekana na haipaswi kuwa mwisho bali endelevu.
Johson Mbwambo ni afisa miradi msaidizi wa Shirika la kimataifa la Search for Common Ground anayehudumu katika Mkoa wa Mtwara ambaye anaamini kuwa washiriki wa mradi na jamii ya ndani na nje ya mtwara, watakuwa wamenufaika kupitia masuala mbalimbali.
Amesisitiza wanufaika kuendelea kutumia nyezo walizopata kuhamasisha amani ili kuepesha athari za migogoro ambazo zimeonekana katika maeneo mengine ya ndani na nje ya nchi.
Shirika la Search for Common Ground lilianzishwa mwaka 1982, linafanya kazi na jamii moja kwa moja likiwa na ofisi katika nchi zaidi ya 3o kutoka Afrika, Asia na Mashariki ya kati, huku miradi 124 ikiwa inaendelea kwenye maeneo hayo, ambapo hapa Nchini Tanzania lilianza kufanya kazi mwaka 2010.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






