BRYSON MSHANA, MTWARA
Wiki ya ubunifu Tanzania mwaka huu ilizinduliwa jijini Dar es Salaam Mei 10, 2022 huku wabunifu wakielezea kufurahishwa na taasisi zilizojitokeza kuwashika mkono katika harakati za kuonesha ubunifu wao ili ulete tija katika jamii zao.
Wiki hii huandaliwa kila mwaka na kuwapa nafasi wabunifu kuonekana, kupata nafasi ya kufahamiana na kutengeneza ushirikiano na maarifa kwa lengo mfumo mzuri wa masuala ya ubunifu hapa nchini.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndiyo inayoandaa wiki ya ubunifu Tanzania kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambapo wabunifu wanapata nafasi ya kujadili kwa kina masuala yanayohusu ubunifu na hatua wanazochukua kuendeleza sekta ya ubunifu ili kuwa na tija kwa Watanzania.
Katika kuongeza wigo wa wiki ya ubunifu kitaifa, mwaka huu watanzania wameshuhudia maonesho mbalimbali ya ubunifu, sayansi na tekinolojia katika mikoa mbalimbali ambapo pia kumekuwepo na semina, mikutano, makongamano na majukwaa mbalimbali ya wadau wa ubunifu, satayansi na tekinolojia.
Mkoani Mtwara uzinduzi wa wiki ya ubunifu ulifanyika tarehe 10 Mei, 2022 kwenye viwanja vya soko kuu Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa uratibu wa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), mgeni rasmi akiwa mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dustan Kyobya alikuwa mgeni rasmi.
Meneja wa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoani Mtwara Twaha Sued, anaeleza kuwa hii ni mara ya kwa kwanza tukio kama hili la kihistoria kufanyika katika Mkoa wa Mtwara na kuratibiwa na SIDO.
Twaha anaongeza kuwa katika kuendeleza suala la ubunifu kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuendeleza na kusimamia viwanda vidogo, SIDO Mtwara kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa maendeleo wamejitahidi kutimiza majukumu yao na hivyo kufanikisha azama yao ya kuvihudumia viwanda vidogo.
“Katika wiki ya ubunifu mkoa wa Mtwara, zilishuhudiwa mashine pamoja na bidhaa mbalimbali, kulitolewa mafunzo ya usindikaji wa bidhaa za vyakula na matunda, utengenezaji wa sabuni na vipodozi na mafunzo ya stadi mbalimbali za biashara”
“Sio hivyo tu lakini wiki hii ilitumika kuwaunganisha wajasiriamali na masoko mbalimbali kwa njia ya kuwakutanisha na wanunuzi kwa njia kushiriki katika maonesho mbalimbali ndani ya nchi, kuwawezesha wajasiriamali katika upatikanaji wa teknolojia na usimamizi wa teknolojia bila kusahau kutoa mikopo ya riba nafuu kwa wajasiriamali katika Mkoa wa Mtwara” anafafanua Twaha Sued.
Kuhusu changamoto ya ajira inayowakabilia vijana, Meneja huyo wa SIDO anasema kuwa vijana wengi wanaomaliza vyuo vyetu bado wanafikra za kuajiriwa serikalini, hivyo SIDO imeandaa program maalum kwa vijana kuwa na mawazo ya ubunifu ili waweze kupata fursa za kifedha kutoka kwenye taasisi za kifedha na pia kupitia mikopo ya vijana ya halmashauri
“Bado hatuna Kanzi data ya wabunifu kwa mkoa wote wa Mtwara ili waweze kutambuliwa na kusaidiwa, SIDO itaendelea kushirikiana na ofisi za wakurugenzi wa halmashauri kupitia kwa maafisa biashara na maafisa maendeleo ya jamii pamoja na wadu wengine ili kutambua wabunifu waliopo na kuweza kuwasaidia kuendeleza ubunifu wao kwa lengo la kuongeza tija. Amesisitiza
Wiki ya ubunifu Mkoani Mtwara ilishuhudia pia kiwanda cha kuzalisha maji cha Ndanda splash kikizindua mashine ya kuchakata maji inayotembea, ubunifu unaolenga unaolenga kuwapatia wanachi maji safi na salama kwa gharama nafuu.
Mkurugnezi mtendaji wa kiwanda hicho Mwang’ini Madenge anasema mashine hiyo ni kiwanda chenye uwezo wa kumfuata mteja mahali alipo na ni rafiki wa mazingira kwani kitapunguza matumizi ya plastics.
“Ubunifu huu umegawanyika katika maeneo matano;Aeration system(Mfumo wa kuboresha kiwango cha oksijen kwenye maji), Filtration system(Mfumo wa usafishaji maji),Cooling System(Mfumo wa kupooza maji),Power system(Mfumo wa kufua umeme rafiki kwa mazingira usio tumia fuel) na Electronic Digital Systems(Mfumo wa kuuzia maji kidigitali) na vyote vinafanyika katika hili hili gari letu lenye kiwanda unaloliona hapo”ameeleza Madenge.
Ubunifu mwingine ni wa kiwanda cha Duma Distilleries Ltd, ambacho kinazalisha pombe kali (spirit) itokanayo na mabibo ya korosho ambayo awali yalionekana kuwa hayana kazi.
Kiwanda hiki kwa sasa kina uwezo wa kuzalisha lita 100 kinywaji hicho kitokanacho na mabibo kwa siku, na kwa upande wa ajira, kimeweza kutengeneza ajira 5 za moja kwa moja, na ajira 50 za msimu ( ajira za kukusanya mabibo kwa wakulimu msimu wa korosho) huku kikirajia kutoa ajira zaidi ya 30 za moja kwa moja kitakapofikia uzalishaji kamili.
Kwa mujibu wa Allex Abraham ambaye ni meneja wa kiwanda hicho anasema “teknolojia yetu ni rafiki sana na mazingira, uzalishaji wa bidhaa zetu hautumii kemikali za aina yeyote na wala hakuna gesi ya ukaa inayozalishwa wakati wa utengenezaji wa bidhaa”
“Pia kwa kutumia teknolojia hii tunaweza kupunguza kiwango cha uchafuzi wa mazingira kwa kupunguza uzagaaji wa mabibo hovyo mtaani, ambayo yangeweza kuleta athari kiafya hususani kwa mlipuko wa magonjwa huku wananchi nao wakinufaika kiuchumi”
“Ikumbukwe kuwa asilimia 90 ya mavuno ya korosho ni mabibo, hii ina maana kwamba uzalishaji wa juu uliowahi kurekodiwa kwa Tanzania wa tani 300,000 mabibo zaidi ya tani 2,700,000 yalizalishwa ambayo ni kiasi kidogo sana kilitumika kutengeneza bidhaa mbalimbali,hivyo ubunifu huu utasaidia kuongeza matumizi ya mabibo na hivyo kusaidia kuongeza kipato cha mkulima wa korosho, hii ni muhimu kwani mkulima atakua hategemei korosho peke yake” amefafanua
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mtwara, Upendo Mchata anabainisha kuwa wiki ya ubunifu inafaa kuungwa mkono na kupewa kipaombele na wadau kutokana na umuhimu wake katika kukuza na kuendeleza sekta ya ubunifu nchini.
“wiki hii inatoa fursa ya kushuhudia mambo mbalimbali ya kiubunifu yanayofanywa na watanzania ambayo wengi wetu hata hatujawahi kuyafikiria lakini wapo vijana wameshayafanya na tunayaona hapa, hii ni hamasa kubwa kwetu, serikali na wadau wengine”
“Mtwara sio tu kwamba imeweka historia ya kushiriki wiki hii kwa mara ya kwanza lakini pia ubunifu uliooneshwa hususan katika sekta ya viwanda umeoutangaza na kuupa heshima mkoa na hizi ni dalili njema za kuelekea mapinduzi makubwa ya viwanda katika siku zijazo” anasema Upendo Mchata
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dustan Kyobya anasema wiki ya Ubunifu Tanzania iliyokuwana kauli mbiu isemayo “Ubunifu kwa maendeleo endelefu” na kufanyika kwa mara ya kwanza katika mkoa wa Mtwara ni jambo la kujivuni.
DC Kyobya anaamini kwamba ubunifu ulioonesha na wabunifu mbalimbali katika sekta ya kilimo na viwanda unaendelea kudhihirisha namna ambavyo Mkoa wa Mtwara ulivyo na hazina kubwa ya fursa mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi.
Niwashukuru wadau wote wa maendeleo kutoka ndani ya mkoa, viongozi wa ngazi mbalimbali za Serikali, viongozi wa asasi za kiraia na wageni wote mliojitokeza kushiriki katika wiki ya ubunifu, aidha, niwapongeze kamati nzima ya maandalizi chini SIDO, kwa kufanikisha maandalizi ya hafla hii na kuweza kuwaleta wadau wote pamoja”
“Kama ulivyosikia mkoa wa Mtwara umepitisha ubunifu wa aina mbili kwa mwaka huu, moja ni kiwanda cha NDANDA SPLASH ambacho kimekuja na ubunifu wa maji safi na salama ya kunywa, pili ni kiwanda cha Duma Distiller Ltd ambacho kimekuja na ubunifu wa bidhaa ya pombe kali ya mabibo (spirit na mvinyo) unaotokana na mabibo ya korosho, hii kwetu ni hatua kubwa”
Mkoa wetu wa Mtwara zao la korosho ndio zao tegemezi lakini utekelezaji wa kilimo hiki tumekuwa tunavuna korosho tu na tunda la bibo tunalitupa, sasa kupitia ubunifu wenzetu wa Duma distiller LTD waliliona hilo na kuamua kuanzisha kiwanda kidogo kinacho lithaminisha na kuchakata tunda la bibo na kutengeneza kinywaji aina ya Duma spirit” Amesisitiza Mkuu wa Wilaya.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






