BRYSON MSHANA, MTWARA

Manispaa ya Mtwara-Mikindani mkoani Mtwara imesaini mkataba wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 27 zinazolenga katika uboreshaji wa miundombinu ya mji kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) unaofadhiliwa na Serikali kuu kupitia mkopo wa Benki ya Dunia wenye thamani ya dola za Kimarekani Milioni 410 (Bila VAT).

Halfa ya kusaini mkataba huo wa kihistoria imefanyika Tarehe 10 Octoba 2025 Mjini Mtwara, ukishuhudiwa na mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala ambapo fedha hizo zinatarajiwa kutumika kujenga kituo cha kisasa cha mabasi, mifereji ya kuondoa maji yanayosababisha mafuriko kila mwaka, barabara za lami, na kituo cha wajasiriamali eneo la skoya.

Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Emanuel Manyanga, amesema sehemu ya utekelezaji wa mradi huo utahusisha ujenzi wa barabara ya Chuno yenye urefu wa kilomita 3.38, barabara ya Samia City Access kilomita 2.4, pamoja na mitaro ya Kiyangu yenye urefu wa kilomita 1.73.

Amesema utekelezaji wa mradi huo utahusisha ujenzi wa kituo cha wajasiriamali katika eneo la Skoya, Kituo  kikuu cha Mabasi Chipuputa, pamoja na jengo la uratibu wa miradi, huku akieleza kuwa usimamizi Mkataba wa utekelezaji wa miradi hiyo ni wa miezi 15 kuanzia Oktoba 15, 2025 hadi Januari 14, 2027, chini ya mkandarasi M/S Serengeti Limited.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amemtaka mkandarasi anayetekeleza miradi hiyo kukamilisha kazi ndani ya muda uliopangwa ili wananchi waweze kupata huduma kwa wakati, na kusisitiza uaminifu kwa wananchi watakaopata ajira wakati wa utekelezaji sambamba na  kulinda miundombinu ya miradi.

“Ni matarajio yetu sote kuwa miradi hii italeta mabadiliko chanya kwa Wananchi wa Manispaa yetu ya Mtwara Mikindani na wageni ambao watafaidi huduma za mahitaji mbalimbali ya usafiri na usafirishaji, pamoja na mazingira bora ya shughuli za kiuchumi kwani ni dhahiri kuwa thamani ya maeneo husika itapanda na hivyo kusababisha ongezeko la mapato kwa Halmashauri yetu” amesema Kanali Sawala

Kuanza kutekelezwa kwa miradi hii muhimu kunaiunganisha Mtwara na manispaa zingine 18 nchini, ambazo zinanufaika na uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania, pamoja na kujengea uwezo taasisi (Halmashauri) ili ziweze kujiimarisha katika usimamizi wa uendelezaji miji pamoja na ukusanyaji wa mapato.

Lengo kuu la maradi wa TACTIC ni kuboresha usiamamiziwa ukuaji wa Miji pamoja na kuziwezesha Halmashauri za Miji na Majiji kutoa huduma bora kwa wananchi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali, kulingana na vipaombele vya eneo husika, kuimarisha usimamizi wa uendelezaji Miji na kuborrsha mazingira ya uwekezaji ili kukuza uchumi wa Halmashauri husika.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…