ABDUL LUKANGA, MTWARA
Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan, amefanya ziara rasmi ya kutembelea Bodi ya Korosho Tanzania mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Urusi.
Ziara hiyo imefanyika leo septemba 8/ ambapo ilimfikisha Balozi kwenye Kongani ya Viwanda inayoendelea kujengwa katika kijiji cha Maranje, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, ambapo alikutana na viongozi wa sekta ya korosho pamoja na viongozi wa serikali za mitaa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred, amesema serikali inaendelea kufanya jitihada za kutafuta masoko mapya ya zao la korosho, likiwemo soko la Urusi, ili kukuza zaidi sekta hiyo muhimu ya kilimo nchini.
>> “Urusi ni miongoni mwa nchi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikinunua korosho kutoka India na Vietnam, lakini kwa sasa kuna fursa ya wao kununua moja kwa moja kutoka Tanzania,” alisema Francis.
>>Aidha, Francis ameongeza kuwa serikali imejiwekea lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030, korosho zote zinazozalishwa nchini zibanguliwe hapa hapa nchini, jambo litakalosaidia kuongeza thamani ya zao hilo na kuongeza ajira. Ujenzi wa Kongani hiyo ya viwanda unatarajiwa kuwa kichocheo kikuu cha kufanikisha azma hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amesema uhusiano wa Tanzania na Urusi ni wa muda mrefu, hususan katika nyanja za uwekezaji, elimu na kilimo. Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhi korosho, hatua itakayochochea uwekezaji mkubwa zaidi mkoani humo.
>> “Tunatarajia uwekezaji mkubwa katika mkoa wa Mtwara kupitia miradi hii. Serikali imejipanga kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaboreshwa kwa manufaa ya wananchi wetu,” alisema Kanali Sawala.
Wananchi wa Mtwara pia wameeleza kuridhishwa kwao na maendeleo hayo. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Abdalla Selemani na Mwalimu Sadiki, wameishukuru serikali kwa hatua hiyo wakisema itatoa ajira kwa vijana wengi waliokuwa hawana shughuli za kufanya.
>> “Ujenzi wa maghala haya na viwanda utatupa ajira sisi vijana wa Mtwara. Tunaomba serikali iharakishe ujenzi ili tuanze kunufaika mapema,” alisema Abdalla Selemani.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






