BRYSON MSHANA

www.mtwarapressblog.co.tz

Agusti 27, 2022 ilifanyika hafla ya kutoa tuzo kwa Vijana Chipukizi Tanzanaia ukumbi wa Julius Nyerere Dar es Salaam , zilizolenga kutambua mchango wao chanya katika sekta mbalimbali za kimaendeleo, jamii na taifa kwa ujumla.

Tuzo hizo ziliandaliwa na Taasisi ya Africa Youth Transformation inayojishughulisha na uwezeshaji wa mambo ya kiuchumi na kijamii kwa vijana ikishirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine.

Tuzo hizo za Vijana Chipukizi Tanzania – TEYA 2022 ambazo zimetolewa kwa mwaka wa pili mfululizo, zinatoa ari na kuhamasisha vijana kupanua fikra ili kuwawezesha kujikomboa kiuchumi kwa kutangaza shughuli wanazozifanya kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( Tehama).

Moja ya kipengele kilichokuwa kinawaniwa katika tuzo hizo, ni kile cha tuzo ya kijana chipukizi Tanzania aliyefanya vizuri katika ujumuishwaji wa watu wenye ulamavu (outstanding youth on disability inclusion).

Tuzo hizo ziliomuibua mshindi Dorice Ahmed Mkiva (29), ambaye ni kijana mwenye ulemavu wa viungo aliyeshinda na kutangazwa mshindi katika kipengele hicho.

Dorice ambaye anafanya kazi na shirika la kutetea haki za watu wenye ulemavu liitwalo ADD international (Action on disability and development), anasema tuzo aliyoipata imezidi kumuimarisha katika kutekeleza vema majukumu yake.

Dorice Ahmed Mkiva, mshindi wa tuzo ya kijana chipukizi Tanzania aliyefanya vizuri katika ujumuishwaji wa watu wenye ulamavu (outstanding youth on disability inclusion) kwa mwaka 2022. Tuzo TEYA 2022 ziliandaliwa na Taasisi ya Africa Youth Transformation ikishirikiana na Serikali.

“Hii ni tuzo muhimu kwangu na vijana wengine wote Tanzania, inaonesha jinsi ambavyo wadau na serikali wanatambua mchango wa watu wenye ulemavu katika kufikia maendeleo endelevu”

“Nikiwa kama mwanaharakati kijana wa masuala ya watu wenye ulemavu, lengo ni kuhakikisha kuwa wote wanapata haki sawa na wasio na ulemavu hususani katika masuala ya ajira kwa kuzingatia Sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 (Disability act no 9, 31(2)) ambayo inasisitiza 3% ya waajiriwa wenye ulemavu kwenye taasisi yenye waajiriwa kuanzia 20 na kuendele” anafafanua Dorice.

Akizungumzia malengo yake ya baadae, Dorice  anasema ni kuwa kiongozi atakayeshiriki katika ngazi za maamuzi kama Mbunge au waziri ili aweze kusuguma hoja za watu wenye ulemavu.

“Nikiwa kwenye ngazi ya kufanya maamuzi mfano Mbunge au Waziri itaniwezesha kuhakikisha haki na agenda za watu wenye ulemavu zinasonga mbele Kwa utekelezwaji ili tuwe na jamii jumuishi isiyokua na vikwazo vyovyote” amesisitiza Dorice.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Africa Youth Transformation, Justine Mponda akizungumzia tuzo hizo anasema lengo ni kutambua mchango wa vijana katika sekta za uchumi na namna ambavyo wanaleta ubunifu katika kutatua changamoto katika jamii.

“Huu ni mwaka wa pili tunaandaa tuzo hizi, zinaleta hamasa kubwa kwa vijana na tunazidi kuendelea kuzipa nguvu hususan kipengele cha watu wenye ulemavu ili kuonesha kwa vitendo nafasii yao waliyonayo katika maendeleo ya Taifa hili”

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako anawasisitiza wadau wengine kuendelea kujitokeza kuunga mkono juhudu za Serikali katika kutambua mchango mchango wa watu wenye ulemavu.

“Hiki kilichofanywa na Africa Youth Transformation Agosti 27, pale ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam kinapaswa kuigwa na wadau wengine, na sisi serikali tupo tayari kushirikiana na yeyote atakayeonesha nia ya kuhakikisha kuwa mchango wa vijana wetu unatambulika katika sekta mbalimbali.

Africa Youth Transformation  ni shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa mwaka wa 2018 na lilisajiliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Julai 19, 2019, linalolenga kukuza haki za kiuchumi na kijamii, amani, pamoja na kuboresha upatikanaji rafiki wa vijana katika elimu, afya na ushirikishwaji wa jamii ili kuondokana na umaskini nchini Tanzania.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…