BRYSON MSHANA, MTWARA

Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imeeleza kuwa maandalizi ya msimu mpya wa mauzo ya korosho ghafi wa mwaka 2025/2026 yanaendelea kwa vizuri, huku ikiahidi msimu wenye tija zaidi kwa wakulima na wadau wote wa tasnia hiyo.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliwasilishwa na Mkurugenzi wa Masoko na Udhibiti wa Ubora wa CBT, Bw. Revelian Ngaiza, katika mkutano wa wadau wa Bandari ya Mtwara uliofanyika tarehe 29 Septemba 2025 katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Mtwara, uliowaleta pamoja washirika kutoka sekta ya usafirishaji, Serikali, vyama vya ushirika, wasafirishaji, wanunuzi wa korosho na taasisi nyingine muhimu.

Kwa mujibu wa Bw. Ngaiza, hadi sasa wakulima wanaendelea na shughuli za uvunaji, na matarajio ni kuongezeka kwa uzalishaji msimu huu, baada ya msimu uliopita  2024/2025 ambao uzalishaji wa korosho ghafi  ulifikia kiasi cha tani 528,263.82, ukilinganishwa na tani 310,787.168 msimu 2023/2024 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 70%.

Kuhusu usafirishaji, CBT imeeleza kuwa msimu huu utaratibu wa usafirishaji wa korosho utaendelea kama ulivyokuwa katika misimu miwili iliyopita, ambapo Korosho kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma zitasafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara, huku zile za Pwani, Morogoro na mikoa mingine zikipitia Bandari za Dar es Salaam na Tanga, kwa mujibu wa Mwongozo wa Masoko na Mauzo ya Korosho Ghafi.

Aidha imesema kuwa  imeshakamilisha na kusambaza miongozo kwa wadau wote wa tasnia kwa ajili ya msimu wa 2025/2026, ikiwemo Mwongozo wa Usimamizi wa Masoko na Mauzo kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi Ghalani, Udhibiti wa Ubora wa Korosho Ghafi, Ununuzi kwa Wabanguaji wa Ndani na Muhtasari wa Sheria na Masharti ya Mauzo (Rules and Sales Conditions).

Kwa upande wake Bandari ya Mtwara imeeleza kuwa imefanikiwa kuongeza kiwango cha ufanisi katika kuhudumia shehena ya korosho baada ya kufanikisha usafirishaji wa jumla ya tani 370,896 katika msimu wa 2024/2025, ikilinganishwa na tani 253,616.94 za msimu wa 2023/2024.

Meneja wa Bandari ya Mtwara Ndg. Ferdinand Nyati, amesema ongezeko hilo ni sawa na 46.2%, na limevuka lengo la kuhudumia tani 200,000 pamoja na makadirio ya uzalishaji wa tani 300,000 yaliyotolewa na Bodi ya Korosho Tanzania.

Nayo Serikali ya Mkoa wa Mtwara imewataka wadau wote wanaohusika kwenye usafirishaji wa zao la korosho ghafi kufuata maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha korosho zinazozalishwa mikoa ya kusini Lindi, Mtwara na Ruvuma zinasafirishwa kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) mkoani Mtwara.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amesema maagizo ya serikali lazima yafuatwe kwani korosho kupitia bandari ya Mtwara kwenda kwenye masoko ya nje kunaongeza ajira na kukuza uchumi wa mkoa huo pamoja na mikoa jirani.

‘’Nitoe wito kwa wadau na taasisi zinazosafirisha korosho kuendelea kuzingatia maelekezo ya serikali ya kutumia bandari ya mtwara kusafirisha korosho zote za mikoa ya kusini Ruvuma, Lindi na Mtwara katika hili niwapongeze kwa ushirikiano huo, maelekezo hayajabadilika kwahiyo tuendelee kujipanga kwamba korosho zetu tunapoingia kwenye msimu kutoka mikoa yetu hii mitatu zitasafirishwa kupitia bandari ya mtwara’’amesisitiza Kanali Sawala

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…