BRYSON MSHANA, MTWARA

www.mtwarapressblog.co.tz

Msingi wa kuanzishwa kwa mashirika yasiyo ya kiserikali hapa nchini Tanzania unatokana na Ibara ya 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya (1977), ambayo inatoa uhuru wa mtu kushirikiana na wengine.

Uhuru huo kikatiba unaenda sambamba na mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania ni nchi mwanachama.

Kwa mujibu wa Ibara ya 22 (1) ya Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), na Kifungu cha 10 cha Mkataba wa Afrika juu ya Haki za Binadamu na Watu, ni wazi kwamba watu wote wana haki na uhuru wa kushirikiana na wengine, ikiwa hawakiuki sheria za nchi.

Ili kutekeleza shughuli za Mashirika yasiyo ya kiserikali kwa ufanisi Mwaka 2001, Serikali kwa kushirikiana na wadau iliandaa Sera ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Kutungwa kwa sera ilipelekea pia kutungwa kwa Sheria ya MashirikaYasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria Na.11 ya mwaka 2005 na Sheria Na. 3 ya mwaka 2019, lengo kuu likiwa ni kuweka misingi imara ya uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa Marekebisho imetungiwa Kanuni mbalimbali zikiwemo Kanuni za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali zilizotangazwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 609 za mwaka 2018, zikiwa zinatoa ufafanuzi wa utekelezaji wa Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuhusu uwazi na uwajibikaji.

Kwa utangulizi huo ni dhahiri kuwa viongozi, watendanji na wanachama wa mashirika yasiyo ya kiserikali wanao wajibu wa kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za nchi.

Ili kuhakikisha kuwa hilo linafanikiwa, serikali na wadau mbalimbali wanapaswa kuendelea kuzikumbusha na kuzijengea uwezo Asasi za kiraia ambazo ni washiriki muhimu wa maendeleo ya nchi kuhusu uelewa wa sheria na taratibu za uendeshaji wake ili kuhakikisha kuwa hazikiuki taratibu na kutoka kwenye malengo ya uanzishwaji.

Afisa kutoka ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Lindi Bw. Kasongo Kitapa, akimsikiliza mmoja wa washiriki mafunzo ya kuzijengea uwezo Asasi za kiraia (mwenye kofia), yaliyolenga kukuza uelewa wa sheria na taratibu za uendeshaji wake katika mafunzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Foundation for Civil Society Septemba 14 na 15, 2022 Mkoani Lindi.

Hivi kribuni Taasisi ya Foundation for Civil Society yenye makao yake makuu Jijini Dar es salaam, iliandaa mafunzo kwa viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserkali katika mikoa ya Lindi na Mtwara, yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kuelewa matakwa ya kisheria katika kufanya kazi.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa Uratibu wa Mafunzo kutoka Taasisi hiyo Bi. Rehema Malongo alieleza umuhimu wa mashirika yasiyo ya kiserikali kuzingatia mahitaji ya kisheria katika kila hatua ya ufanyaji wa kazi, ili yaweze kitimiza malengo ya kuwahudumia wananchi pasipo kukiuka taratibu za nchi.

“FCS inatamani kuona Tanzania yenye mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu, ndio maana inajitahidi kuyajengea uwezo na uelewa juu ya masuala muhimu, na mategemeo ni kuwa kila shirika itaenda kufanya shughuli zake kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya nchi” alisema Rehema Malongo

Mwakilishi wa Uratibu wa Mafunzo kutoka Taasisi ya Foundation For Civil Society Rehema Malongo, akiwasilisha mada “Uzingatiaji wa sheria na uadilifu wa ndani ua Ushirika” wakati wa mfunzo ya kukuza uelewa wa sheria na taratibu za uendeshaji wake kwa mashirika yasiyo ya kiserikali Septemba 15, 2022 Mkoani Lindi.

Serikali inasemaje?

Kwa upande wake Serikali inaamini kuwa bado haijachelewa, na inaendelea kuunga mkono na kushirikiana na wadau wengine katika kuyakumbusha mashirika yasiyo ya kiserikali juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria katika utekelezaji wa majukumu yake.

Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara Abdalah Malela, anakiri kuwa serikali inatamini mchango wa asasi za kiraia kutokana na umuhimu wa sekta hiyo katika kuchangia na kukuza maendeleo na ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo anasisitiza kuwa ni muhimu kukumbushana juu ya wajibu wa serikali katika kusimamia na kuratibu Taasisi hizo, na wajibu wa Taasisi husika katika kutimiza matakwa ya kisheria ikiwemo ulipaji wa kodi,kuwasilisha taarifa zake kwa wakati, na kutofanya shuguli zinazoenda kinyume na maadili ya jamii ya kitanzania.

“Upo umuhimu mkubwa wa kukutana na kujadili masuala yanayohusu Asasi za Kiraia kwenye Mikoa na Wilaya zetu, kwa kuwa sekta hii ni muhimu katika kuchagiza maendeleo na ustawi wa wananchi, Serikali inathamini mchango na kazi zinazofanywa na wabia hawa wa maendeleo kwa ajili ya manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla”

“Tunapoikuza jamii yetu ya kitanzania, tunamsaidia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutekeleza maono yake kwenye Taifa hili na nipende kumshukuru kwani amekuwa akihamasisha tuzidi kuimarisha ushirikiano na asasi za kiraia” anasisitiza Malela

Kwa upanade wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Dkt. Bora Gretha Haule, anaeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayatambua Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), kuwa wabia muhimu katika kuleta maendeleo ya kijamii na Taifa.

Dkt. Haule anasema kwa kulitambua hilo Serikali imekuwa ikishirika katika vikao vya kujenga na kuimarisha uhusiano wa kiutendaji baina ya Sekretarieti ya Mkoa, Halmashauari na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali, hali inayotoa nafasi ya kukumbushana juu ya uwajibikaji.

“Uwajibikaji ni takwa la kisheria na siyo hiari, Asasi hizi zinatakiwa kufuata maelekezo ya Sheria, Kanuni na Taratibu, ni wazi kuwa hata upangaji mipango ya shughuli za NGOs hauna budi kuwashirikisha wananchi/jamii iliyolengwa katika afua za NGO husika” ameeleza Dkt. Haule

Maoni ya wawakilishi wa Asasi za kiraia

Mjumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoani Mtwara Balthazar Komba, anaamini kuwa utaratibu wa mshirika yasiyo ya kiserikali kukumbushwa juu ya kufuata kanuni na sheria za nchi unapaswa kuwa endelevu.

Komba anasema kuwa uwepo wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo lengo lake ni kuchochea maendeleo katika jamii yanapswa kuendana na uelewa wa sheria za uendeshaji wake.

“Serikali na Asasi za kirai ni wabia wakuu wa maendeleo ya Taifa, sasa hatuwezi kujiita wabia wa maendeleo halafu hatufuati taratibu ambazo zimewekwa na mbia mwenzetu (Serikali) ambaye tunaamini kuwa tunaenda naye sambamba katika kuwahudumia wananchi” anamalizia Komba.

Mjumbe wa Mwanvuli wa Mashirika yasiyo ya kiserikali kitaifa kutoka Mkoa wa Lindi Stambuli Shemkomba, anapongeza juhudi zinazofanywa na wadau wengine kama Foundation for Civil Society akieleza kuwa zinafaa kuigwa na wadau wengine wa maendeleo.

“Foundation for Civil Society wameonesha mfano wa kuzijengea uwezo Asasi za kiraia na wapo wadau wengine wakiwepo kutoka Taasisi za serikali ambao wanaweza kufanya mwendelezo wa hili kwani kuyawezehs amashirika ni kuwawezesha wananchi”

“Ukifuatilia unagundua kwamba matakwa haya ya kisheria yanasimamiwa na Taasisi za Serikali mfano Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mamlaka ya mapato Tanzania, Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini hivyo uandaliwe utaratibu wa wadau hawa kuzifikia Asasi za kiraia mara kwa mara na kuzikumbusha juu ya kanuni na sheria mbalimbali”ameeleza Shemkomba

Wataalam wa Sheria wanasemaje?

Denis Bashaka, ni Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Msajili wa Mashirika yasiyo ya kiserikali makao makuu Dodoma, anawasisitiza viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali kutosahau wajibu wao wa kisheria.

Anaeleza kuwa yapo mambo ya kisheria ambayo ni muhimu na yanapaswa kuzingatiwa, kama kuweka wazi vyanzo vya rasilimali zinazoendesha miradi yao, matumizi yake na shughuli zinazotekelezwa.

Ameongeza kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kuwasilisha mikataba ya ufadhili unaozidi milioni ishirini kwa Msajili wa NGO na Hazina, pamoja na kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji wa kifedha ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi mabaya ya fedha za ufadhili zinazotolewa.

“Haya ni matakwa ya kisheria ambayo yanapaswa kufuatwa na zipo adhabu zake iwapo kutakuwa na ukiukwaji wa sheria, hivyo ni vema mashirika yakazingatia na pale ambapo kunakuwa na mkwamo basi tufahamishwe kwa ajili ya kuwekana sawa” amesema Bashaka.

Naye Grace Shao ambaye ni Waikili wa Serikali kutoka Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) anazitaka Asasi za kiraia kujenga utaratibu wa kutembelea katika mamlaka za serikali na kuomba ufafanuzi iwapo yapo mambo wasiyoyelewa.

“Tunaweza kuwa na utaratibu wa kukutana lakini sio lazima kusubiri mpaka kwenye vikao ndio tuelekezane bali sisi pia ka wadau tunaweza kujiwekea utaratibu wa kutembeleana ofisini na kujadiliana juu ya mambo mbalimbali yanayotuhusu”

Afisa kutoka ofisi ya TRA Mkoa wa Mtwara Denis Urio, anasema kama ilivyo kwa walipakodi wengine, taasisi za kiraia zina wajibu kuelewa sheria na taratibu mbalimbali za kodi.

Anazitaja kuwa ni pamoja na Taasisi/vikundi vyenye mueleko wa imani za kidini, Vyama vya kijamii, Vyama vya Ushirika, Vituo vya kutoa msaada wa kisheria, Taasisi za hisani, n.k

Urio anasisitiza kuwa lengo siyo kutengeneza faida au kugawana mapato yanayotokana na shughuli za taasisi, bali kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni au masuala ya mazingira katika jamii.

Kwa mantiki hii, ni dhahiri kuwa Mashirika yasiyo ya kiserikali yanatakiwa kuzingatia masharti ya sheria na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na Kujisajili kwa mujibu wa Sheria Na. 24 ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa Marekebisho na Sheria Na. 11 ya mwaka 2005 na Sheria Na. 3 ya mwaka 2019 kabla ya kuanza shughuli yoyote ya shirika;

Vile vile mashirika haya yanapaswa kuendelea kukumbushwa kuwa  yanatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa nyaraka za usajili ikiwemo cheti cha usajili na Katiba kwa mujibu wa kifungu cha 30 cha Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali Na.24 ya mwaka 2002;

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…