BRYSON MSHANA, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Mbaazi ni zao la chakula ambalo pia linaweza kulimwa kama zao la biashara likionesha kuwa na soko zuri katika miaka ya hivi karibuni kutokana na mahitaji yake kuongezeka ndani na nje ya nchini.

Mikoa ya Lindi na Mtwara ina jumla ya eneo linalofaa kwa kilimo cha mazao lenye jumla ya Hekta 5,000,000 kwa Mkoa wa Lindi na Hekta 1,400,000 kwa Mkoa wa Mtwara.

Mazao makuu yanayolimwa katika eneo hili ni pamoja na mazao ya chakula ambayo ni muhogo, mtama, mahindi, mpunga, mazao ya jamii ya mikunde na mazao ya biashara ni kama korosho, ufuta na nazi.

Ukuaji wa sekta ya kilimo katika mikoa ya kusini unahusishwa moja kwa moja na uwepo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI-Naliendelea iliyo Mkoani Mtwara.

Taasisi hii  imekuwa ikifanya utafiti pamoja na kuzalisha mbegu za mazao mbalimbali ya chakula na biashara, kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wananchi wanaojihusisha na kilimo wanalima kisasa ili kuongeza uzalishaji sambamba na kuongeza kipato.

TARI – Naliendele, kupitia wataalam wake imekuwa ikitafiti na kuzalisha mbegu za mazao mbalimbali kama Korosho, Ufuta, Karanga, Mihogo, mazao ya jamii ya mikunde, Matunda pamoja na Mbogamboga.

Zao la Mbaazi ni moja ya mazao ambayo yamekuwa yakistawi katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya kusini, huku TARI ikiwa imejielekeza katika kutafiti na kuzalisha mbegu bora na zinazokomaa kwa muda mfupi.

John Tenga, ni Mtafiti wa kitengo cha Nafaka na Jamii ya mikunde kutoka TARI – Naliendele ambaye anaeleza kuwa Udongo wa maeneo mengi ya mikoa ya Kusini ni rafiki kwa kilimo cha zao la Mbaazi, hivyo kazi yao kama watafiti ni kuhakikisha kuwa utaalamu wao unawafikia na kuwahudumia wakulima.

Dr. Tenga amesema kuwa katika kuwahudumia wakulima, wameweza kutafiti na kuzalisha mbegu ambazo zinakuwa kwa siku 180 (miezi mitatu), tofauti na awali ambapo mkulima ilibidi kusubiri miezi 8 kuvuna mazao yake.

“Muitikio wa wakulima kutumia mbegu za kisasa ni mkubwa, na hii inatokana na matokeo yake kuonekana kuanzia kwenye uzalishaji lakini pia muda wa mazao kukaa shambani kupungua jambo ambalo linawapa hamasa wengi kuingia kwenye kilimo hiki cha Mbaazi” amefafanua Dr. Tenga

Juhudi hizi za TARI katika kukuza zao la Mbaazi zinaenda sambamba na Serikali kuwekeza nguvu katika kuhakikisha kuwa wakulima wanapata soko la uhakika.

Sehemu ya juhudi hizo ni mkakati wa kuingiza zao la Mbaazi katika mfumo wa skabadhi ghalani, ambapo mikoa ya Mtwara na Lindi sasa imeingia rasmi kwenye mfumo huo ambao utaanza kutumia kwenye msimu wa mwaka huu 2023/2024.

Julai 31, 2023 wadau wa mazao ya mbaazi mkoa wa mtwara, walifanya kikao cha pamoja kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali  Ahmed Abbas, ambaye alieleza  kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani utakaotumika kwenye ununuzi wa zao la Mbaazi msimu 2023/2024 unalenga kumnufaisha mkulima kupata soko la uhakika.

Kanali Abbas alieleza kuwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, wakulima watakusanya Mbaazi na kuuza kwa pamoja kupitia vyama vyao vya ushirika kwa ajili ya kupata bei nzuri inayoendana na soko.

“Mfumo huu ni sehemu ya juhudi za serikali kumtafutia soko mkulima, hivyo ukasimamiwe vizuri ili na kama kuna makato yawe ni yale tu yaliyopitishwa kisheria na  yaelekeza katika shughuli za maendeleo ya wananchi zilizopitishwa” alieleza Kanali Abbas.

Kwa upande wa watafiti TARI, wanaamini kuwa mfumo huo utawawezesha kupata takwimu halisi za kilimo cha Mbaazi katika mikoa ya Mtwara na Lindi, hali itakayorahisisha kuwafikia na kuwahudumia wakulima kwa wakati.

“TARI tumefurahi kuwa Mbaazi sasa itauzwa kupitia mfumo rasmi, hii ni hatua kubwa na pongezi kwa serikali na wadau kwa kufanikisha hili, sasa tunaenda kulirasimisha zao hili na tutegemee manufaa makubwa kwa wakulima tunaowahudumia” amesisitiza DR. John Tenga, ni Mtafiti wa kitengo cha Nafaka na Jamii ya mikunde  kutoka TARI

Kwa mujibu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi Mtwara (MAMCU), kimejiandaa vizuri na Msimu wa Mbaazi 2023/2024 na tayari imeshaagiza vifungashio ambavyo vinatarajiwa kuwasili ifikapo Tarehe 05/08/203.

Taarifa ya MAMCU iliyowasilishwa Julai 31, 2023 Kaimu Meneja wa MAMCU Tawi la Masasi Costantine Francis kwenye kikao cha wadau wa mazao ya mbaazi mkoa wa mtwara, ilieleza kuwa imeweka makisio ya kununua Mbaazi Tani 15,000 kutoka vyama 187 ambavyo vitashiriki katika ununuzi wa zao hilo kwa msimu 2023/2024.

Kwa upande wa baadhi ya Wakulima wa Mbaazi  wameonesha kuridhishwa na mfumo huo wakieleza kuwa unafaa kuungwa mkono na changamoto zitakazojitokeza zitaendelelea kutatuliwa kulingana na muda unavyoenda.

Bi. Hawa Mkata Mkulima kutoka Kijiji cha Chigugu Wilayani Masasi, ameipongeza Serikali kwa kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani kwenye zao la Mbaazi, akieleza kuwa utakuwa na manufa kwa wakulima wote ikiwepo wale wa wadogo.

“Kwa kuanzia kunaweza kuwa na changamoto ambazo zitaendelea klutatuliwa polepole, hata wakati tunaingiza Korosho kwenye mfumo ilikuwa hivyohivyo lakini wote sasa tunaona mafanikio ya mfumo huu, nashauri tuingie kwa aslimia 100 mfumo huu ni mkombozi wa mkulima” Amesisitiza Hawa Mkata

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…