BRYSON MSHANA

www.mtwarapressblog.co.tz

MASHINDANO ya Michezo ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini (UMISSETA & UMITASHUMTA) mwaka 2022 ilifanyika kitaifa mkoani Tabora, kuanzia Julai 29, 2022 hadi Agusti 19, 2022 ambapo mikoa yote ya Tanzania ilishiriki kupitia wawakilishi mbalimbali.

Michezo hiyo iliandaliwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaana Michezo ikizinduliwa rasmi Agusti 04, 2022 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa katika uwanja wa Alli Hassan Mwinyi Mjini Tabora.

Mashindano ya mwaka huu yalijumuisha michezo ya mpira wa netboli, mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa wavu,mpira wa mikono, mpira wa meza,riadha, pamoja na sanaa za maonesho zilizohusisha ngoma, kwaya na muziki wa kizazi kipya.

Pamoja na burudani ya michezo iliyotolewa na washiriki katika kipindi chote cha mashindano, lakini pia mashindano haya yaliyojumuisha takriban washiriki elfu saba, yalienda sambamba na uwepo wa fursa za kibiashara kwa wakaazi wa mji wa Tabora na maeneo ya jirani.

Wananchi hao walinufaika kupitia shughuli za kibiashara walizokuwa wakizifanya wakati wote wa mashindano, zikiwepo za uuzaji wa vyakula, usafirisha, nyumba za kulala wageni, maeneo ya kuoshea magari pamoja na maeneo ya kuuza vinywaji mbalimbali.

Aziza Hassan mkaazi wa eneo la Bomba Mzinga na Stella Kayombi mkaazi wa Kariakoo Manispaa ya Tabora ambao ni wauzaji wa chakula (Mama Ntilie) ni baadhi ya wananchi ambao walikuwa na vibanda vya kuuzia vyakula kwenye moja ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo pembezenoni mwa shule za wasichana na wavulana Tabora.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao wanasema michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA iliwafanya watanue wigo wa kibiashara kutokana na ongezeko la mauzo lililotokana na ugeni mkubwa walioupata wakati wa mashindano hayo.

“Wengi unaotuona hapa tunafanya bishara ya kuuza vyakula huko mjini, lakini kutokana na michezo hii Serikali ilituandalia eneo maalumu kwa ajili ya kuuzia hapa shule ya girls na kule boys ambapo tunawauzia waalimu, wanafunzi na watu wengine” anaeleza Stella Kayombi.

“Nichukue fursa hii kumpongeza Rais Mama Samia kwa kutukumbuka wanatabora katika hili, wiki tatu za michezo tumefanya biashara ambayo hatujawahi kabisa kuifanya na ni kwa sababu ya ugeni mkubwa uliokuwa mjini kwetu ambao ni fursa kwetu” amesema Aziza Hassan.

Akizindua rasmi mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Agusti 04, 2022 katika uwanja wa Alli Hassan Mwinyi Mjini Tabora, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa aliwataka wananchi wa Tabora kuchangamkia fursa za kibiashara zitakazoambatana na michezo hiyo.

Waziri mkuu Majaliwa alisema mashindano hayo yanaambatana na ujio wa watu mbalimbali wanaokadiriwa kufikia elfu saba, jambo ambalo lina tija kubwa kibiashara na kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Tabora na hata ile ya jirani.

“Rais anatambua na ameahidi kuendelea kuongeza ubora wa miundo mbinu ya michezo mashuleni ili kuzidi kutengeneza mazingira bora ya wanafunzi kushiriki michezo mbalimbali hivyo hamasa hii iendane sambamba na wananchi kunufaika kiuchumi kupitia michezo kama hii ambayo imeletwa kwenu Tabora” alisisitiza waziri mkuu Majaliwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batlida Buriani, anaizungumzia michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA 2022 kama moja ya matukio ambayo yameuchangamsha zaidi kibishara mkoa huo.

Anaishukuru Serikali kwa kuuchagua mkoa wa Tabora kuwa mwenyeji wa UMITASHUMTA na UMISSETA kwa mwaka 2022, jambo ambalo amesema limezidi kuwasogezea wanachi wa Tabora fursa mbalimbali za kiuchumi.

“Mkoa wa Tabora tunaishukuru sana Serikali ya Mama Mhe. Rais Samia, na kupitiakwa Waziri mkuu Kassim Majaliwa ametueleza kuwa Tabora itakuwa mwenyeji wa mashindano haya kwa mara nyingine mwaka ujao wa 2023, hii ni heshima kubwa kwetu na tunaahidi kuwaandaa zaidi wananchi ili wanufaike kiuchumi”

“Nilimweleza hata Waziri Mkuu alivyokuja kwenye uzinduzi Agusti 04, 2022 kuwa mashindano hayo yaliuchangamsha mkoa wa Tabora kibiashara, na kusaidia uchumi wa watu mbalimbali kuongezeka kutoka na huduma zinazotolewa kwa wageni waliokuja kushiriki michezo” anaeleza Balozi Dkt. Batlida Buriani.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa usafirishaji maarufu kama bodaboda Omary Said mkaazi wa Mtaa wa Jida – Uzunguni Manispaa ya Tabora anaeleza kuwa wakati wa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA biashara ilikuwa ikifanyika mara mbili zaidi ya siku za kawaida.

“Biashara ilikuwa nzuri sana, kwanza bei ziliongezeka kutosha shilingi elfu moja hadi elfu mbili kwa safari moja kutokana na michezo kuchezwa nje kidogo ya mji hivyo kutupa fursa ya kuongeza kipato zaidi, tunatamani ingekuwa hata miezi miwili”

“Seriklali ya Mama Samia imetuheshimisha sana vijana wa bodaboda Tabora kupitia michezo hii, tunamshukuru na tunasubiri tena mashindano ya mwakani tuendelee kutengenza kipato kupitia michezo hii” amasema Omary Said

Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Peter Maiga Nyanja anaeleza kuwa UMISSETA & UMITASHUMTA 2022 imeacha alama kubwa Mjini Tabora, ni imemgusa kila mkaazi wa eneo hilo kwa namna moja ama nyingine.

“Kupitia michezo hii kila mwananchi amefikiwa kwa namna flani kwa njia ya huduma za kijamii ambazo zilikuwa zinatolewa na wanatabora wenyewe kwa wageni zaidi ya elfu saba ambao walihusika katika michezo ya mwaka huu”

“Tunapopata wageni kama hivi wananchi wananufaika pamoja serikali pia, michezo hii ilileta burudani lakini vilevile iliongeza kipato kwa wanachi na mwaka ujao tutajipanga zaidi kuandaa mazingira mapema ikiwepo kuboresha zaidi mazingira ya kibiashara kwa wanachi wetu”

Dkt. Nyanja anaongeza kuwa Tabora imewaonesha wageni waliofika kwa ajili ya michezo kuwa zipo fursa nyingi za kiuchumi zinazochagizwa na miundombunu rafiki na huduma za kijamii ambazo zimesambaa kila mahali.

“Wageni watakuwa wameondoka na picha tofauti ya Tabora, na nina uhakika baadhi yao huko walipo hivi sasa watakuwa wanafikiria kuhamia Tabora kikazi kutokana na yale waliyoyaoni na sisi tunawakaribisha sana” anamalizia Dkt. Nyanja.

Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA 2022 yaliyofunguliwa rasmi Agusti 4,2022 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, yalisimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na yatanatarajiwa kufanyika kwa mara Mkoani Tabora mwaka ujao 2023.

Uwepo wa mashindano haya mkoani Tabora umeonyesha ni jinsi gani michezo inaweza kuleta fursa za kiuchumi kwa wananchi, hivyo ni wakati sasa wa Serikali ya mkoa wa Tabora ikishirikiana na wadau wengine, kujipanga na kuandaa mazingira bora zaidi ili hamasa ya kibiashara iliyojitokeza mwaka huu iendelee na kukua maradufu kwenye UMITASHUMTA na UMISSETA 2023.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…