BRYSON MSHANA, IRINGA
November 10, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto UNICEF lilitoa ripoti iliyozinduliwa Jijini New York Marekani iliyozungumzia idadi ya watoto wenye ulemavu Duniani kufikia takriban milioni 240.
Ripoti ilisema kuwa watoto wenye ulemavu wanakosa fursa ikilinganishwa na watoto wasio na ulemavu katika hatua nyingi za ustawi wa watoto, ikieleza kwamba wastani mtoto 1 kati ya 10 anakosa mahitaji ya msingi ikiwemo afya, elimu na ulinzi.
Ripoti hiyo ilijumuisha takwimu kutoka nchi 42 ikishughulikia zaidi ya viashiria 60 vya ustawi wa watoto, iliangazia kwa uwazi vikwazo vinavyozuia watoto wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika jamii na athari mbaya za kiafya na kijamii ambazo mara nyingi hutokea.
Utafiti huo ulithibitisha kile ambacho tayari jamii inakifahamu kuwa watoto wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto na mara nyingi athari limbikizi katika kutekeleza haki zao jambo ambalo wadau wanapaswa kulitilia mkazo.
Katika kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali, wapo watu, wadau na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yamekuwa yakichukua hatua madhubuti ili kulifikia kundi hilo.
Moja ya mashirika hayo ni lile liitwalo IBO ITALIA, kutoka nchini Italia lililopo hapa Tanzania mkoani Iringa, ambalo taarifa zake kwa mara ya kwanza www.mtwarapressclub.co.tz
ilizipata wakati wa mashindano ya michezo ya shule za msingi (UMITASHUMTA) yaliyofanyika mkoani Tabora kuanzia July 29, 2022 hadi August 8, 2022.
Michezo ya UMITASHUMTA 2022 yalihusisha michezo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, na mkoa wa Iringa uliwakishwa na baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu kutoka katika shule mbalimbali huku IBO ITALIA wakutuma mmoja wa wafanyakazi wake Bw. Elikana Katambi kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya watoto hao.
Mwandishi wa Mtwara Press Blog alishawishika kuomba maelezo ya shirika hilo na baada ya mashindano aliamua kufanya ziara mkoani Iringa Agusti 22 hadi 23, 2022 ili kutembelea na kujionea mambo mbalimbali yanayotekelezwa na wadau hao waliojikita katika upatikanaji wa fursa za kielimu kwa watoto wenye ulemavu.
Shirika hili ambalo lilianza kufanya shughuli zake mkoani Iringa mwaka 2018 limeweka lengo la kuhakikisha watoto wote wenye ulemavu wanapata fursa ya kwenda na kusoma shule, na watoto wote waliopo shuleni wapate mfumo bora wa Elimu jumuishi.
Katika kufanikisha malengo yake, Shirika hilo linatekeleza miradi mbalimbali, ukiwepo mradi wa kuhakikisha kuwa hakuna mtoto mwenye ulemavu anayeachwa nyuma katika suala la elimu uitwao “NO ONE LEFT BEHIND”, unafadhiliwa na wakala wa maendeleo wa Italia.
PAOLA GHEZZI ni Mkurugenzi wa IBO ITALIA, ambaye anaeleza kuwa mradi wa “NO ONE LEFT BEHIND”, unalenga kufanya shughuli kuu tatu ambazo ni MAFUNZO KWA WALIMU (In-service training); ambapo shirika kwa kupitia wataalamu na wafanyakazi wake, linatoa mafunzo mbalimbali kuhusiana na Ulemavu na Elimu jumuishi kwa walimu na wadau mbalimbali wa elimu mkoani Iringa.
“ Hii iia tunashirikiana na viongozi wa wilaya kwa kupitia maafisa elimu na maafisa elimu maalum wa wilaya na wadau wengine wa serikali katika juhudi ya kuboresha elimu maalumu, lakini pia IBO Italia inapanga shughuli maalum za kujumuisha watoto wenye ulemavu katika shule 10 za Wilaya ya Iringa” ameeleza GHEZZI.
GHEZZI ameieleza Shuguli nyingine kuwa ni UJENZI (accessibility), ambapo shirika limekuwa likijenga na kuboresha miundombinu jumuishi ya shule mbalimbali hasa shule zinazofanya kazi na shirika (targeted schools) kama vile ujenzi wa ngazi mteremko (Ramps), vyoo jumuishi na Mabweni (hostel).
Anatolea mfano wa Bweni la wasichana shule ya Msingi Kipera iliyopo Halimashauri ya Iringa, ambapo pamoja na ujenzi kumefanyika ugawaji wa vifaa visaidizi kwa wanafunzi na walimu wenye ulemavu, vikiwepo vya kusaidia usikivu (hearing devices), Baiskeli ya kutembelea wenye walemavu wa viungo (wheelchairs), mashine ya kuandikia watu wasio ona (braille mashine) na karatasi zake.
Shuguli ya tatu ni UHAMASISHAJI (Community Awareness), ikiwa ni kuihamasisha jamii kuachana na imani potofu kuhusu watoto na watu wenye ulemavu kwa kufanya vikao na wazazi pamoja na walezi wa Watoto wenye ulemavu.
Uhamasishaji huo pia hufanyika kupitia mikutano ya hadhara, hamasa redioni, picha na matamasha mbalimbali yenye lengo la kutoa fursa na haki ya Elimu jumuishi kwa Watoto wenye ulemavu mkoani Iringa, na pia kuandaa mikutano na wanafunzi wa shule za sekondari na hafla za umma.
“Mbali na shughuli kuu hizo tatu, shirika limekua na linaendelea kutengeneza shughuli (programs) mbalimbali katika shule za msingi ; shughuli jumuishi ndani ya shule (Inclusive school activities) kama vile Busitani, michezo (mpira wa miguu, nyavu, kikapu, goalball na riadha),
“Pia kutengeneza vikundi vya kujifunza (school clubs) kama vile lugha ya alama /sign language, upigaji wa picha/ photovoice na uchoraji/ drawing” amefafanua Mkurugenzi huyo wa IBO ITALIA.
Kwa upande wa Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na shirika hilo katika kuhakikisha kuwa watoto wote wenye ulemavu wanapata fursa ya kwenda na kusoma shule, na watoto wote waliopo shuleni wapate mfumo bora wa Elimu jumuishi Mkoani Iringa.
Afisa elimu maalum Halmashauri ya Wilaya ya Iringa bw. Wilfred Mattu ameeleza kuwa Shirika la IBO ITALIA limekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wenye ulemavu na serikali inatambua mchango wake mkubwa katika kuihudumia jamii.
“Shirika hili linatoa huduma mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mabweni, kutengeneza ngazi mteremko kwa ajili ya kurahisisha watoto wenye ulemavu kuingia na kutoka katika vyumba vya madarasa pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia” amesema Wilfred Mattu
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Kipera Bi Faines Mteleka amesema shule yake ambayo imekuwa ikipata msaada kutoka katika shirika hilo, ni ya mseto yenye wanafunzi wenye ulemavu na wasio na ulemavu.
Amesema hadi kufikia sasa shuleni kuna wanafunzi 97 wenye umemavu wa aina mbalimbali wakiwepo wasioona, wasio sikia, ulemavu wa viungo na wenye changamoto ya akili ambao pamoja na kuhudumiwa na serikali lakini pia wamekuwa wakipata msaada kutoka shirika la IBO ITALIA.
Suala la watoto wenye ulemavu kupata mfumo bora wa elimu jumuishi linapaswa kupewa kipaombele kutoka kwa jamii, serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Agusti 08, 2022 wakati anahitimisha michezo ya shule za msingi nchini (UMITASHUMTA) mkoani Tabora, Naibu Waziri Utamaduni Sanaa na Michezo Pauline Gekul, aliiipongeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi kwa wanafunzi wote wakiwepo wenye mahitaji maalum.
Naibu waziri Gekuli alisema utekelezaji huo umeleta tija katika kuimarisha ushirikiano na ushirikishwaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalam kitaaluma na kimichezo kuanzia ngazi ya shule hadi Kitaifa.
Juhudi hizi za serikali pamoja na zile za wadau, zinaonyesha kuwa kuna hatua imeanza kupigwa katika suala la ujumuishwaji wa wa watoto wenye ulemavu kielimu japo bado zipo changamoto ambazo zinapaswa kuangaziwa na kutafutiwa ufumbuzi ili kuendelea kuleta uswa wa kielimu nchini.
Juhudi zinazofanywa na wadau kama Ibo Italia na wengine hazipaswi kuishia Mkoani Iringa ama kuiachia Serikali pekee, bali jamii, mashirika na Taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa wanapaswa kuunga mkono juhudi hizi na kuzifanya kuwa endelevu ili kuhakikisha kwamba watoto wenye ulemavu wanapata haki zote za msingi.
Kwa mujibu wa umoja wa Matafa kupitia shirika lake linaloshughulikia watoto UNICEF, upo uwezekano mkubwa kwamba asilimia 49% ya watoto wenye ulemavu Duniani hawajawahi kwenda shule.
UNICEF inasema kati ya hao asilimia 47% ni katika shule za msingi, asilimia 33% katika shule za sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na asilimia 27% ni katika shule za sekondari za vidato vya juu.
Zaidi ya hayo, watoto wenye ulemavu wana uwezekano wa kufaidika na shughuli za malezi ni asilimia 24% na wakati huo huo, ni asilimia 42% tu ndio wenye uwezekano wa kujua kusoma na kuhesabu.
Katika ngazi nyingine, UNICEF inasema watoto wenye ulemavu wana uwezekano wa kubaguliwa kwa asilimia 41%.
Kwa mantiki hiyo UNICEF inatoa wito kwa serikali kuwapa Watoto wenye ulemavu fursa sawa na wengine, kuondoa vikwazo vya kimwili, kifedha, na kimiundombinu vinavyowasababishwa wakaachwa nyuma katika jamii.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






