BRYSON MSHANA, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Imeelezwa kuwa Watu 2,686 wamegundulika kuwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI Mkoani Mtwara, katika zoezi la upimaji uliohusisha watu 150,224 lililoanzia mwezi Januari hadi Desemba 2023.

Hayo yameelezwa Desemba 01, 2023 mjini Mtwara na Mratibu wa Kudhibiti VVU na UKIMWI Mkoa wa Mtwara Dk. Makarious Moris, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani kwa Mkoa wa Mtwara, yaliyofanyika viwanja vya Sabasaba Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Dk. Makarious amesema kwa takwimu za upimaji wa mwaka uliopita (2022) watu 138,665 waliopimwa ambapo kati yao, watu 2,837 (2%) waligundulika kuwa na maambukizi.

“Mwaka huu hatujamaliza lakini mpaka kufikia leo (Desemba 01) kwa halmashauri zote tumepima watu 150,224 na mpaka sasaivi waliogundulika kuwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ni 2,686 (1.7%).” Amesema Dk. Makarious.

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Dk. Stephen Mwakajumilo, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, akawataka wataalamu wa UKIMWI kufika vijijini kutoa elimu ya udhibiti wa gonjwa hilo.

“ Mimi nipo Nanyumbu mwezi 1 na Nusu, sijapata huduma zozote kama hizi na hakuna yeyote aliyekuja kwamba kuna huduma zinazotolewa, kwahiyo niwaombe ndugu zangu mnaotoa huduma hizi nendeni vijijini wananchi wana uhitaji mkubwa wa huduma hizi isiwe mjini inawezekana hizi takwimu tunazotolewa nyingi zipo mjini.” Ameagiza Dk. Mwakajumilo.

Wakati hayo yakijiri Mkoani Mtwara, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliongoza maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kitaifa, kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Morogoro, mjini Morogoro.

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu ameitaka mikoa na wilaya zote nchini itekeleze maelekezo ya kufanya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani na kutoa huduma stahiki kwa wananchi.

Sambamba na hilo Waziri Mkuu ameagiza kila mkoa uandae taarifa ya maadhimisho hayo yaliyofanyika Decemba 1, 2023 itakayoainisha huduma mbalimbali za kijamii na kuiwasilisha kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI,”

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…