MWANDISHI WETU, MOROGORO

mtwarapressclub@gmail.com

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, meitaka mikoa na wilaya zote nchini itekeleze maelekezo ya kufanya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani na kutoa huduma stahiki kwa wananchi.

Sambamba na hilo Waziri Mkuu ameagiza kila mkoa uandae taarifa ya maadhimisho hayo yaliyofanyika Decemba 1, 2023 itakayoainisha huduma mbalimbali za kijamii na kuiwasilisha kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI,”

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo Desemba 1, 2023 Mkoani Morogoro, wakati akizungunguza katika maadhimisho ya Ukimwi Duniani ambayo kitaifa yamefanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Morogoro, mjini Morogoro.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini, wa siasa na wa kimila watumie majukwaa waliyonayo kuendelea kusema na kukemea taarifa za ubaguzi dhidi ya waathirika wa virusi vya ukimwi na kuhimiza upendo na huruma kwao.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka vijana wajitambue na kuthamini maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, na kuwasisitiza juu ya umuhimu wa kulinusuru kundi hilo.

“Wadau wote wekeni kipaumbele katika kundi hili muhimu ili kulinusuru na athari za UKIMWI.” Amesisitiza Waziri Mkuu.

Pia amewataka watu wanaoishi na VVU waendelee kutumia dawa za ARV kwa ufuasi sahihi bila kuacha ili kufubaza VVU na kuimarisha afya zao. “Taifa linawategemea, Serikali itaendelea kuhakikisha huduma za ARV nchini zinapatikana.”

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ili kukabiliana na kasi ya kuenea kwa maambukizi wa VVU, wizara yake imezindua mpango wa kuoanisha VVU, magonjwa ya ngono na homa ya ini kwani kuna ushabihiano mkubwa wa njia za maambukizi za magonjwa hayo.

Amesema hatua hiyo imekuja baada ya kubaini kuwa asilimia 4.4 ya Watanzania wana maambukizi ya magonjwa ya ini.

Akielezea mpango wa wizara kufikisha huduma ya afya kwa ngazi ya jamii, amesema wizara hiyo inatarajia kuajiri wahudumu wa afya ya jamii 137,000 ambao watafanya kazi kuanzia ngazi ya mitaa na vitongoji.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…