BRYSON MSHANA, LINDI
0787 568 733
Sekta ya madini imeendelea kukua kwa kasi katika mkoa wa Lindi kutokana na maeneo mengi mkoani humo kuelezwa kuwa na madini ya aina mbalimbali.
Ukuaji huu wa sekta ya Madini Mkoani Lindi, umetokana na usimamizi mzuri wa Serkali kupitia Wizara ya Madini, uongozi wa Mkoa, Ofisi ya Kamishna wa madini, wananchi na wadau wengine.
Vilevile ukuaji huu umechangiwa pia na uwepo wa madini ya aina mbalimbali, kukua kwa teknolojia na uwepo wa wawekezaji wakubwa na wadogo katika sekta hiyo ambayo ni muhimu katika ukuaji wa sekta na uchumi wa Taifa la Tanzania.
Agusti 1 hadi 8, 2023 yalifanyika maonesho ya Kilimo,Ufugaji na Uvuvi maarufu kama Nanenane Kanda ya kusini katika viwanja vya Ngongo vilivyopo Manispaa ya Lindi Mkoani Lindi.
Ofisi ya Tume ya Madini Mikoa ya Lindi na Mtwara, zilishiriki katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali wa madini waliokuwa na shauku ya kupata fursa ya kujua zaidi kuhusu madini.
Malick Masoud Omar ni Mjiolojia kutoka Tume ya Madini Lindi, katika mahojiano maalum na Mtwara Press Blog, anaeleza juu ya hamasa kubwa waliyokuwa nayo wananchi kufika katika banda la Tume hiyo kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo madini.
Malick anaeleza kuwa pamoja na kutoa elimu juu ya aina ya madini na maeneo yanayopatikana katika kanda ya kusini, lakinni pia walifanikiwa kuelimisha juu ya utaratibu wa kujirasimisha kwa wachimbaji wanaofanya shughuli hiyo.
“Muitikio wa watu ni mkubwa tumetembelewa mpaka na wanafunzi wa shule na vyuo mbalimbali, ukiangalia madaftari yetu ya wageni yameshajaa yote kutokana na wingi wa wananchi wanaofika hapa, tumewapa elimu ya kujua aina za madini yanayopatikana katika mikoa ya kusini, maeneo yanapopataikana na taratibu za kufuata wanaotaka kuwekeza”
“Sio hilo tu lakini pia tunao mfumo wa taarifa za leseni za madini wenye fomu za kuwaunganisha kwenye mfumo wale wanaotaka kupata usajili wa kujishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini, watu zaidi ya 20 wamejaza fomu kupitia maonesho haya” ameelza Malick.
Kuhusu Aina za Madini Mjiolojia huyo ameeleza kuwa Lindi kuna aina nyingi za madini yakiwepo ya Viwandani ambayo ni zaidi ya 80%, yakifuatiwa na Madini ya Ujenzi, Vito na dhahabu huku tafiti zingine zikiwa bado zinaendelea.
“Lindi kuna aina nyingi za madini, kila Wilaya ya Lindi ina madini, wawekezaji waje tu kuwekeza hususana kwenye eneo la viwanda ambalo malighafi zake nyingi zinapatikana katika mkoa wa Lindi” ameongeza Mjiolojia Malick.

Baadhi ya wanafunzi waliotembelea banda la Tume ya Madini lililojumuisha mikoa ya Mtwara na Lindi, wakati wa maonesho ya Wakulima, Wafugaji ya Wavuvi (Nanenane) Kanda ya Kusini Viwanja vya Ngongo Lindi.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliotembelea maonesho ya Nanenane Kanda ya kusini na kufika katika Banda la Kamishna wa Madini Lindi & Mtwara, wanaeleza kuwa wamejifunza mambo ambayo hawakuwa wanayajua kabla.
Tatu Abdallah Mkaazi wa Kijiji cha Nyengedi Halmashauri ya Mtwama Mkoani Lindi, anasema “sisi tunasikia tu na kuona kwenye tv kuwa Lindi kuna madini, lakini kupitia Nanenane hii tumejionea wenyewe na kujifunza”
“Serikali ya Mama Samia ituletee viwanda na wachimbaji wakubwa wa madini kama mikoa ya wenzetu tunayoiona na kuisikia, ili na sisi tuharakishe maendeleo yetu na watoto wetu kupitia ajira mbalimbnambali zitakazozalishwa” anasema Tatu Abdallah
Kupitia maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, Wananchi na wadau wamezidi kujionea na kufahamu utajiri wa Madini unaopatikana katika Mkoa wa Lindi, na wengi wao wamekuwa wakisisitiza juu ya uharakishwaji wa uwekezaji mkubwa na mdogo ambao utachangamsha uchumi wa mikoa ya kusini.
Kwa mujibu wa https://lindi.go.tz/economic-activity/mineral, inayataja baadhi tu ya madini yanayopatikana Wilaya ya Lindi ina Madini ya ujenzi, chumvi, mawe, chokaa, feldspar, pozzolana, Makaa ya mawe, chuma, jasi, kinywe (graphite) huku Wilaya ya Kilwa ikiwa na madini ya Jasi, mawe ya chokaa, madini ya ujenzi, chuma, vito kinywe.
Kwa upande wa Wilaya ya Ruangwa kuna dhahabu, vito, kinywe, madini ya ujenzi, chuma, shaba, feldspar, Garnet (RED & GREEN), na Wilayani Liwale inapatikana Dhahabu, nikeli, mabo (marble), manganese, amazonite wakati Nachingwea kuna Dhahabu, kinywe, vito, chuma, shaba, Nikeli nk.
Katika kile kinachoonekana kuwa ni juhudi za Serikali kuwekeza kwenye sekta ya madini kusini mwa Tanzania, Juni 18, 2023 Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko alifanya ziara na kuzungumza na wanachi wa Kijiji cha Namangale katika Halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi na kueleza juu ya uwekezaji wa Madini ya kinywe (graphite) kwenye eneo hilo.
Dkt. Biteko alisema tayari imeshapatikana Kampuni ya Volt Resources Limited ya Nchini Austria itakayochimba madini hayo inatarajiwa kuwekeza zaidi ya Dola za Marekani Milioni 40 katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa mgodi huo ikikadiriwa kuwa na hifadhi ya zaidi ya tani milioni 461 za madini ya Kinywe katika kijiji cha Namangale Mkoani Lindi.
“Uwekezaji huu utasaidia kuongeza ajira na kuchochea maendeleo kwa wananchi wa mkoa wa Lindi na maeneo ya jirani kupitia shughuli mbalimbali kuanzia wakati wa maandalizi ya mgodi na uchimbaji wa madini” alieleza Dkt. Biteko.
Taarifa hizi za wingi wa madini yanayopatikana na yanayoendelea kutafitiwa katika mkoa wa Lindi na juhudi za uwekezaji zinazofanyika, zinaenda kuufanya Mkoa wa Lindi kuingia kwenye mikoa itakayozidi kuchangia pato la Taifa kupitia Sekta ya Madini ambayo iliongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017, hadi asilimia 7.2 mwaka 2021.
Aidha, katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2022/2023 mchango wa sekta ya madini ni asilimia 9.6, ambapo Serikali kupitia sekta ya madini imeweza kukusanya shilingi bilioni 409.66 sawa na asilimia 85.43 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 479.51 katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2022/2023.
Mei 09, 2023 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasim Majaliwa wakati akifungua Kongamano la Wachimbaji Madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) kwenye ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza, alieleza kuwa ongezeko hilo linatokana na kuendelea kuimarisha sekta hiyo muhimu katika ukuaji wa uchumi hapa nchini.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






