BRYSON MSHANA, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Wakulima wa zao la Korosho katika Kijiji cha Mkahala Halmashauri ya Nanyamba mkoani Mtwara, wameuza kiasi cha zaidi ya Tani Elfu 6.5 za Korosho kwenye Mnada wa Nne  uliosimamiwa na Chama Kikuu chu Ushirika MAMCU Ltd, Novemba 10, 2023.

Katika mnada huo, jumla ya Kampuni 30 zilijitokeza na kuwasilisha maombi ya kununua Korosho Ghafi katika Maghala mbalimbali yaliyopo Masasi, Nanyumbu na Mtwara kwa bei ya juu ya Shilingi 2,000/= na bei ya chini shilingi 1,850/=.

Mnada huo pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda ambaye alipata nafasi ya kuwasilisha salama za Serikali kwa wakulima wa Korosho waliojitokeza mnadani.

Katika salam zake DC Munkunda alivitaka vyama vya msingi kuharakisha malipo kwa wakulima wa korosho kwa wakati, ili wapate fedha kwa ajili ya kununulia mahitaji mbalimbali ikiwemo chakula.

“Wanunuzi walionunua Korosho wanaendelea kufanya malipo kupitia vyama vyao vya ushirika, niwaombe viongozi wa vyama kuharakisha malipo hayo yawafikie wakulima kwa wakati ili waweze kuendelea na shughuli zao zingie”

“Pia niwaombe tu wakulima kutumia vizuri malipo wanayoyapata ili yaweze kuwasaidia katika kufanya shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kupeleka watoto wao shule” amesisitiza Mkuu wa Wilaya

Awali akitoa taarifa yam nada huo kwa wakulima, Meneja wa MAMCU Biadia Matipa, alieleza kuwa hadi kufikia jumatano Novemba 8, 2023 Chama Kikuu kilikuwa kimepokea Kiasi cha Kilo 8,342,102 za Korosho ambazo zote zimepelekwa sokoni kupitia mnada wa leo.

“Tunaendelea na Minada yetu na leo tupo kwenye mnada wa nne, Tayari tulishafanya minada mitatu kwa mafanikio makubwa na kuuza jumla ya Tani 32,538 za Korosho ambazo zimeingiza kiasi cha fedha Shilingi Bilioni 64, 814 ambacho kimeenda kwa wakulima” amesema Bi Matipa.

Check Also

SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI USHIRIKI WA WADAU KATIKA MAENDELEO YA MAKAZI NCHINI

Na Munir Shemweta Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ushiriki wa wadau katika…