BRYSON MSHANA, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Julai 14, 2023 Serikali ya Tanzania kupitia Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) ilitangaza kuanza maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa wa Korosho utakaohusisha zaidi ya Mataifa 30 yanayolima zao la Korosho Duniani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, Mkutano huo wa kihistoria kwa nchi ya Tanzania, unatarajiwa kufanyika Tarehe 11 October 2023 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa JNICC Jijini Dar es Salaam.

Inakaridiwa kuwa zaidi ya washiriki 500 kutoka katika mataifa mbalimbali ambayo yanajihusisha na kulima, kununua na ullaji wa Korosho wanatarajiwa kuwa miongoni mwa washiriki katika mkutano huo.

Huu ni Mkutano ambao unaambatana na fursa mbalimbali kwa wadau wa Korosho kutoka Nchini Tanzania, ambao kama watautumia vizuri unaweza kuwaletea manufaa chanya katika shughuli zao za kulima, kununua, kubangua au kuuza korosho.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa wadau wote mahususi wa sekta ya Korosho, watahusika katika Mkutano huu wenye wazo kuu la fursa za uwekezaji kwenye tasnia ya Korosho Tanzania (an insight and investment opportunities in Cashew Industry Tanzania).

Ukiwa na kauli mbiu isemaypo “wekeza kwenye Korosho kwa mendeleo endelevu” (invest in cashew for sustainable development), Mkutano huu utashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchi ambazo ni walaji wa korosho ikiwa ni pamoja na Marekani, Nchi za Ulaya, China, Uarabuni, Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na nchi zingine za bara la Afrika.

Kwa upande wa chi zinazolima Korosho zinazotarajiwa kushiriki ni pamoja na Ivory Coast, Cambodia, India, Vietnam, Brazil, Indonesia, Sri Lanka, Nigeria, Guinea Bissau, Burkina Faso, Mali, Benin, Ghana, Madagascar, Zambia, Msumbiji, Kenya, Mauritius, Visiwa vya Komoro na wenyeji Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania Francis Alfred, anasisitiza kuwa mkutano huu unaenda kuwashirikisha wadau wote walioko kwenye mnyororo wa thamani wa Tasnia ya Korosho Duniani kama vile wakulima, wabanguaji, wasindikaji, wakaangaji, wasafirishaji na Vyama vya Ushirika.

“Mkutano huu unakusudia kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko kwenye Tasnia ya Korosho hapa Tanzania, kuanzia shambani ambapo tunategemea kupata uwekezaji wa kwenye mashamba makubwa, Ubanguaji ambapo matarajio ni kuongezeka kwa viwanda vya kubangua na kusindika korosho na bidhaa zake na kuimarika kwa masoko kwa kufungua masoko ya korosho na bidhaa zake ndani na nje ya nchi” Ameeleza Francis

Mkutano huu unakuja wakati ambapo Bodi ya Korosho Tanzania katika kusimamia maendeleo ya Tasnia imeweka malengo makuu matatu ambayo ni: Kuongeza uzalishaji wa korosho ghafi kufikia tani 1,000,000 ifikapo mwaka 2030; Kubangua asilimia 60 ya korosho hizo; na Kuwa na masoko ya uhakika na endelevu ya korosho na bidhaa zake ifikapo 2030 ili kufikia agenda 10/30.

Agenda 10/30 inaelekeza sekta ya kilimo kuchangia asilimia 10 ya pato la Taifa na kuingiza fedha za kigeni kwa wingi.

Kwa mujbu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi ya Mwaka 2022, zao la korosho liliongoza kwa kuliingizia Taifa kiasi cha Dola za Marekani Milioni 226.9 ikilinganishwa na mazao mengine ya tumbaku (Dola Milioni 178.), kahawa (Dola Milioni 161.2), Pamba (Dola milini 103.4), karafuu (Dola Milini 42.18M), Chai (Dola Milioni 30.0M) na mkonge (Dola Milini 24.3).

Takwimu hizi zinaonesha kuwa fursa zilizoko kwenye Tasnia ya Korosho zikitumika vizuri ikiwa ni pamoja na kuziwekea mipango endelevu inayotekelezeka kwa wakati, zinaweza kupelekea Taifa kupata nyoneza zaidi ya fedha nyingi zaidi za kigeni katika kipindi kijacho.

Mkutano wa Kimataifa wa Korosho mwaka 2023 unaoandaliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Bodi ya Korosho Tanzania, ni moja ya fursa za hivi karibuni kabisa ambazo zinatakiwa kupewa kpaombele cha kipekee na wadau wa Tasnia hiyo hapa nchini.

Watanzania hususani wakulima, wawekezaji na wadau kwa ujumla wanapaswa kutumia fursa hii adhimu kuhudhuria mkutano huu ili kuweza kujifunza kutoka kwa nchi zilizofanikiwa na zaidi katika zao la korosho.

Mkutano huu pia ni fursa ya kipee inayoweza kupelekea kupata wawekezaji wa kuweza kushirikiana nao katika miradi mbalimbali ya korosho

Bodi ya Korosho Tanzania imeandaa fomu ya kidigitali iliyoko kwenye tovuti ya Bodi ya Korosho Tanzania (www.cashew.go.tz) ambayo itatumiwa na washiriki kuomba kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Korosho wa mwaka 2023.

Aidha, washiriki wa ndani ya nchi wataweza kupiga namba ya bure 0800112159 ili kupewa maelekezo ya namna ya kujisali pale watakapokuwa na changamoto kwenye kujaza fomu, huku fomu za usajili pia zikipatikana kwenye ofisi za Bodi zilizoko Mtwara, Dar es Salaam, Tanga, Tunduru, Manyoni na Morogoro.

 

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…