BRYSON MSHANA, MTWARA
mtwarapressclub@gmail.com
NOVEMBA 13, 2023 Naibu waziri Mkuu ambaye pia ni waziri wa nishati Dkt. Dotto Biteko alianza ziara ya siku tatu Mkoani Mtwara akikagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo hususan katika eneo la Gesi asilia na umeme.
Ziara hiyo ya Dkt. Biteko, ni ya tatu kufanywa na viongozi wa Juu wa Serikali ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania katika kipindi cha mwezi Agust hadi Novemba 2023 ikiwa ni ndani ya miezi minne pekee sawa na wastani wa kiongozi mmoja kila mwezi.
Mwezi wa 7 na 8 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alifanya ziara Mkoani Mtwara kwa nyakati mbili tofauti na kuzitembelea Wilaya za Mtwa, Tandahimba na Newala kisha akafuatiwa na Rais Dkt Samia Suluhu Septemba 14 hadi 18 aliyezitembelea wilaya zote za Mtwara.
Akiwa Mkoani Mtwara Rais. Dkt Samia alizindua rasmi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, kutembelea Bandari ya Mtwara, Uwanja wa Ndege Mtwara pamoja na kuzindua Barabara ya Mtwara – Mnevata yenye urefu wa Kilomita 50 iliyojengwa kwa kiwango cha Lami.
Akiwa ameongozana na Mawaziri zaidi ya watano, Rais Dkt. Samia alitembelea wilaya zote za Mkoa wa Mtwara akizindua miradi, kusalimia wananchi na kufanya mikutano ya hadhara huku majibu ya kero za wananchi yakitolewa na mawaziri alioambatana nao.
Moja ya msisitizo wa Rais Dkt Samia wakati wa ziara yake ilikuwa ni kuhakikisha kuwa mikoa ya kusini na nchi jirani zinazopakana na mikoa hiyo zinaunganishwa kupitia Mtwara, na hali hiyo inathibitishwa kulingana na uwekezaji unaoendelea.
Baada ya Rais Samia sasa ni Naibu Waziri Mkuu Dkt Bitekeo ambaye katika ziara yake Mkoani Mtwara alitembelea na kukagua visima vya kuzalisha na mitambo ya kuchakata Gesi ya Mnazi Bay iliyopo katika Kata ya Msimbati wilayani Mtwara.
Tarehe 14 Novemba, 2023, Dkt Biteko alipata fursa ya kuzungumza na wananchi katika Kijiji cha Msimbati wilayani Mtwara, ambao alisikiliza kero zao na kuanza kuzitafutia ufumbuzi wakati mkutano wake unaendelea.
Wananchi wa Kata ya Msimbati walimweleza Dkt.Biteko kuhusu changamoto walizonazo ikiwemo barabara, kituo cha afya, kutopata fedha zozote kutokana na kazi za uzalishaji wa uchakataji Gesi Asilia unaofanyika kwenye kijiji hicho na kutopata taarifa mbalimbali za mradi ikiwemo zinapotokea changamoto kwenye bomba la Gesi Asilia.
“Changamoto kwenye miradi hii zinatokea lakini lazima awepo mtu ambaye ni daraja kati ya Serikali na Wananchi, na Mtu huyu analipwa mshahara kwa kazi hiyo, haiwezekani Waziri au Rais kuja kutoa taarifa kwa wananchi wakati kuna mtu kaajiriwa kwa kazi husika, wananchi hawa wanapaswa kupata taarifa.” Amesisitiza Dkt.Biteko
Dkt. Biteko aliagiza Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuondolewa katika nafasi hiyo kutokana na majibu yasiyo stahiki wanayojibiwa wananchi wanapopiga simu kwenye Shirika hilo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
Vilevile, Dkt. Biteko ameagiza kuwa, miradi inapotekelezwa katika eneo lazima ibadilishe maisha ya wananchi, ikiwemo pia upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile Shule, Vituo vya Afya, Barabara na Maji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko tarehe 15 Novemba, 2023 alikagua miradi ya umeme vijijini na kuwasha umeme katika Kata ya Naliendele, eneo la Pachota A na Kijiji cha Nachenjele Wilayani Mtwara.
Sambamba na hilo Naibu Waziri Mkuu alitoa katazo kwa kampuni zinazosimamia na kutekeleza miradi ya umeme nchini, kutonunua nje ya nchi vifaa vya umeme ambavyo vinazalishwa hapa nchini ili kukuza viwanda vya ndani vinavyozalisha vifaa hivyo, kuvipa thamani, kukuza ajira na uchumi wa nchi.
Ziara hii ya Naibu waziri mkuu, imeendelea kuonyesha namna ambavyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza kwa vitendo juhudi za kuifungua mikoa ya kusini mwa Tanzania na kuiunganisha kimaendeleo.
Ziara hii imendelea pale ilipoishia ile ya Rais Dkt Samia, na kama kuna eneo ambalo Dkt. Samia hakufika ni dhahiri kuwa Naibu waziri Mkuu amefika na kuzungumza na wananchi jambo limeendelea kuwaweka karibu wananchi na Serikali.
Kazi sasa imebaki kwa wananchi kuendelea kunufaika na fursa mbalimbali zinazoendelea kufunguliwa na serikali katika maeneo ya ikiwa ni pamoja na kubuni miradi midogo midogo ya kuwaingizia kipato.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Jones Olotu Mkoa wa Mtwara umetengewa shilingi bilioni 170 kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini na kwamba katika vijiji 785 vya mkoa huo, Vijiji 401 bado havina umeme lakini wakandarasi kampuni ya Derm, Central na Namis wanaendelea kusambaza umeme kwenye Vijiji vilivyosalia.
Ametaja miradi inayoendelea kutekelezwa mkoani humo kuwa ni REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili (REA III Round II), Mradi wa kusambaza umeme katika maeneo ya pembezoni mwa miji (Vijiji-Miji) (Peri-Urban III), Mradi wa Kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo, Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji pamoja na Mradi wa ujazilizi (Densification 2C).
SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI USHIRIKI WA WADAU KATIKA MAENDELEO YA MAKAZI NCHINI
Na Munir Shemweta Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ushiriki wa wadau katika…






