BRYSON MSHANA, MTWARA
Tangu mwaka 2014, Mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) umekuwa ukitekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara yenye jumla ya kaya za walengwa 7,595 zilizofikiwa katika kipindi cha takribani miaka nane iliyopita.
Kati ya walengwa hao, wapo 5,194 kutoka katika vijiji 57 vya awali na walengwa wapya 2401 kutoka katika vijiji vipya 37 na kufanya jumla vijiji 94 viwe vimeingia kwenye mpango wa TASAF, kati ya vijiji 110 vya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Kupitia mpango wa kushirikisha kaya masikini awamu ya kwanza ulioanza mwaka 2014 hadi 2019, na ule wa awamu ya pili ulioanza mwaka 2020 umewezesha kufikiwa kwa walengwa wote waliokusudiwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mtwara kupitia kitengo cha TASAF imekuwa na majukumu ya kuratibu na kusimamia malipo ya fedha za ruzuku kwa walengwa wa kaya maskini,Kusimamia uibuaji wa miradi ya ajira ya muda, kutoa elimu juu ya kuweka akiba na uwekezaji ili kuhakikisha walengwa wa kaya maskini wanaondokana na umaskini.
TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara imeendelea kuwafikia walengwa na kuendelea kupewa elimu ya matumizi sahihi ya ruzuku wanayoipokea kupitia warsha za jamii zinazofanyika muda mfupi kabla ya kuanza kwa zoezi la malipo.
Kufuatia elimu hiyo walengwa wamepata elimu juu ya matumizi sahihi ya ruzuku katika kaya, ikiwa ni pamoja na kuwezesha wanafunzi kupata mahitaji ya msingi ya shule kama vile sare na chakula lishe.
Vilevile walengwa wamepata elimu juu ya Kuweka akiba na kuwekeza katika ufugaji wa kuku, mbuzi, kilimo na hata biashara ndogo ndogo ili waweze kuongeza kipato katika kaya, ushiriki wa kazi za ajira za muda (PWP) katika miradi yao waliyoibua katikaviijiji vyao ili waweze kujiongezea kipato hususani katika kipindi cha hali.
Katika kuthibitisha mafanikio ya mpango wa TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Walengwa wameweza kuunda vikundi 520 vya watu kati ya 10-15 vyenye dhamira ya kuweke akiba na kuwekeza, kwa kuchangia hisa na akiba ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea kupitia katiba za vikundi vyao.
Asha Ally Mohamed, mlengwa mwenye namba ya mpango MTD – 08571 kutoka katika kijiji cha Litembe Kata ya Madimba, ni mmoja wa wale walionufaika na mpango kwa kuweza kujenga nyumba ya kisasa ambayo hivi sasa anaishi.
“Nawashukuru sana TASAF, mwanzo nikuwa naishi kwenye banda tu, lakini baada ya kufikiwa na mpango nikaanza kujiongeza na sasa ninamiliki nyumba nzuri tu ya kunitosha kuishi mimi na familia yang” anasema Asha Ally.
TASAF imeviwezesha vikudi hivi kusajiliwa na Halmashauri pamoja na Benki kuu ya Tanzania (BOT), ili viweze kuendana na sera za wizara ya fedha kwa ajili ya kuanza kukopeshana na kufanya biashara ndogondogo pamoja na utatuzi wa changamoto mbalimbali za kifamilia.
Vikundi hujishughulisha na shughuli za uvuvi wa samaki, mashamba ya Korosho, Miradi ya miti ya Matunda (Miembe, Michungwa na Ndimu), Miradi ya visima vya kuvuna maji ya mvua, ujenzi wa Nyumba za bati, ufugaji mbuzi na kuku.
Kata za Libobe, Madimba, Mbawala, Namayanga, Naumbu, Dihimba, Nanguruwe ni sehemu ya waliofikiwa na kunufaika na uanzishwaji wa vikundi hivyo ambavyo vimeta tija kwa walengwa.
Kupitia ujuzi huu mlengwa Mohamed Hamis Madenge mkaazi wa kijiji cha unguja kata ya Libobe, mwenye namba 05214 ameanzisha mradi wa kufuga mbuzi na biashara ya kuuza Nazi, ambavyo anasema vimeweza kumuinua kiuchumi.
“TASAF haikupi tu fedha, bali imeenda mbali zaidi kutuunganisha na vikindi na kutupa elimu ya bishara hivyo kutuwezesha kuanzisha biashara na kuzisimamia kisasa” anasisitiza Mohamed.
Pamoja na hayo, mpango wa TASAF umewezesha miradi ya kutoa ajira ambayo imekuwa itatekelezwa kwa kutumia nguvu kazi kutoka katika Kaya zilizoandikishwa kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini na kulipwa ujira wa Tsh 3,000 kwa siku.
Utekelezaji huu umefanikisha walengwa kushiriki katika miradi 92 ya ajira za muda, kwa kufanya kazi masaa manne kwa siku ndani ya siku 10 za mwezi, huku washiriki wakiwa ni wale wenye umri kati ya miaka 18-65.
Mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) umekuwa wa mafanikio kwa walengwa wa kata zote 21 na vijiji 94 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kufuatia Kaya kuwekeza katika shughuli ndogo ndogo za uzalishaji.
Vilevile mpango huu umewezesha kaya kuaminiwa na jamii kwa kurejesha heshima kwa jamii ambayo ilikuwa imepotea kutokana na kuwa maskini, ambapo sasa zinapata fedha na kuweza kununua mahitaji muhimu ya kaya kama vile chakula, mavazi, kuboresha makazi na kumudu gharama za huduma za afya.
Mafanikio mengine ni ongezeko la mzunguko wa fedha katika kijiji kufuatia fedha zinazopelekwa kijijini kwa ajili ya kuhawilisha kwa kaya maskini, kutoa msukumo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kuongeza mzunguko wa fedha katika vijiji husika.
Mpango huu umeonyesha kuwa na tija kubwa kwa jamii hususan kaya maskini, hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara itaendelea kufanya jitihada za makusudi kuhakikisha walengwa wote wanatumia vizuri fedha wanazopata kwa kuanzisha miradi mbalimbali kwa ajili ya kujiongezea kipato.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






