OR TAMISEMI, SIMIYU

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo J. Dugange(Mb) ameridhishwa na usimamizi wa fedha za ujenzi miundombinu ya Hospitali ya wilaya Itilima na Kituo cha Afya Mwanhunda katika halmashauri ya wilaya Itilima mkoani Simiyu.

Ameeleza hayo Januari 17, 2023 wakati wa ziara yake mkoa Simiyu ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya afya ambapo amejionea majengo yakiwa yamejengwa kwa viwango vinavyoenda na thamani ya fedha.

“Niwapongeze kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa Jengo la wagonjwa wa dharula (EMD) ambalo limefika asilimia 99 kwa gharama ya milioni 300, pia nimepita kwenye wodi zote na nyumba ya watumishi nimeshuhudia ujenzi umefanyika kwa viwango na thamani ya fedha inaonekana” amesema Dkt. Dugange akiwa katika Hospitali ya wilaya Itilima

Amesema Hospitali ya wilaya Itilima ina majengo 17 kati ya hayo majengo 8 yameshaanza kutoa huduma kwa wananchi na majengo mengine 9 yapo katika hatua za mwisho ukamilishaji na maandalizi ya kuanza kutoa huduma yanaendelea.

Aidha, Dkt. Dugange amesema hospitali hiyo imeanza kutoa huduma ya upasuaji na huduma nyingine muhimu kama huduma za wagonjwa wa nje, huduma ya dharura, afya ya uzazi, vipimo vya maabara, kliniki ya kifua kikuu na kliniki za Mama, Baba na Mtoto.

Dkt. Dugange ametoa wito kwa halmashauri nyingine ambazo zinaendelea kutekeleza miradi ya afya kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa miundombinu kwa wakati na kuzingatia ubora unaoendana na thamani ya fedha zilizotolewa.

Kadhalika, Dkt. Dugange wakati akikagua ujenzi wa kituo cha Afya Mwanhunda amejionea majengo ya awamu ya kwanza ambayo ni jengo la OPD, maabara na kichomea taka yakiwa katika asilimia 98 kwa gharama ya milioni 250.

Pia, amekagua majengo ya awamu ya pili katika kicho cha Afya Mwanhunda ambayo ni jengo la kujifungulia na upasuaji, jengo la kufulia ambayo yamefika asilimia 90 kwa gharama ya milioni 250 na akaagiza majengo yote yakamilishwe ifikapo machi 1, 2023 na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…