OR – TAMISEMI

mtwarapressclub@gmail.com

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mohamed Mchengerwa amewataka wadau wa afya wanaofanya kazi nchini kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-TAMISEMI ili kuboresha huduma za afya ya msingi kwa wananchi.

Mchengerwa ameyasema hayo Octoba 06, 2023 kupitia hotuba yake ya kufunga Kongamano la Afya iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Wilson Mahera.

Katika hotuba hiyo Mchengerwa amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimejenga vituo vingi vya kutolea huduma za afya na kupeleka vifaa tiba vya kisasa kwenye ngazi ya msingi, hivyo juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono na wadau wote ili kufikia lengo la kila mwananchi kupata huduma bora ya afya kabla ya mwaka 2030.

Amesema kwa sasa Serikali inaandaa mwongozo utakaowaunganisha wadau wote katika sekta ya afya nchini ili waweze kufanya kazi kwa umoja tofauti na sasa ambapo kila mdau anatekeleza mradi wake kivyake.

“Serikali inataka wadau wote watekeleze kwa pamoja miradi ambayo Serikali inaona inafaa kutekelezwa kwenye sekta ya Afya na ndio maana inandaa mtaala wa kufundishia wahudumu wa afya, na pindi ukikamilika wadau wataitwa kuujadili kwa lengo la kuuboresha ili uanze kutumika na usaidie kutatua changamoto zinazoikabili afya ya msingi nchini,”amesema.

Kongamano hilo la siku tatu limewakutanisha wataalamu wa afya nchini na wadau wengine wa afya kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili changamoto zinazoikabili afya ya msingi na utatuzi wake ikiwa ni pamoja na kutumia fursa zilizopo kuboresha afya ya msingi nchini.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…