HADIJA OMARY, LINDI

mtwarapressclub@gmail.com

Watu 7 wamefariki dunia na wengine 22 wamejeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha basi lenye namba za usajili T 604 DJJ aina ya Scania mali ya kampuni ya Saibaba, lililogongana na Basi dogo aina ya Tata lenye namba za usajili T 217 DXG mali ya kampuni ya Baharia.

Ajali hiyo imetokea Oktoba 5, 2023 katika kijiji cha Kiwawa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi ACP PILI MANDE.

ACP PILI MANDE amesema chanzo ni derva wa basi la kampuni ya Saibaba kutaka kulipita gari kubwa la mizigo ambalo lilikuwa mbele yake na ndipo walikutana na basi hilo dogo la kampuni ya Baharia likitokea Dar es salaam kwenda Tandahimba Mtwara, na kugongana uso kwa uso.

Amewataja Waliofariki dunia kuwa ni, Lucas John (59) dereva aliyekuwa akiendesha basi la kampuni ya Saibaba pamoja na Omari Alli Abdalah (49) ambaye ni dereva wa Basi dogo ya kampuni ya Baharia na kwamba Miili ya marehemu 5 bado haijatambuliwa majina yao na Majeruhi 3 ambao hali zao ni mbaya majina yao hayajafahamika.

Kati ya majeruhi hao wanawake ni Wawili na mtoto mdogo jinsia ya kiume Mmoja wamelazwa katika hospitali ya Kinyonga wilaya ya Kilwa.

Kamanda Mande amesema pia Majeruhi wengine 19 wanaendelea kutibiwa na kuangaliwa hali zao na madaktari na wataruhusiwa kulingana na hali zao za unafuu huku akitoa wito kwa madereva wote kufuata sheria za usalama barabarani na kuwa makini kipindi hiki mvua inapokuwa inanyesha kwa kuwa barabara inakuwa inateleza.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa halmashauri ya kilwa Dkt. Lusajo Mwakajoka amethibitisha kupokea majeruhi 22 kati yao wanawake 11 na wanaume 11 ambao kati yao wawili ni watoto huku watatu kati yao wakiwa na majeraha makubwa katika maeneo ya kichwani.

Alisema licha ya kupokea majeruhi hao wamepokea pia miili ya marehemu saba ambapo kati yao wanaume walikuwa wanne na wanawake mmoja pia na watoto wawili wakiume mmoja na wakike mmoja na miili yao tayari imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…