BRYSON MSHANA, DAR ES SALAAM

mtwarapressclub@gmail.com

Wadau mbalimbali wa sekta ya korosho, wamepongeza maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.

Mkutano huo wa siku tatu unaoj umuisha zaidi ya wadau 500 kutoka nchi 33 zinazozalisha na kula korosho, ulianza Octoba 11, 2023 na kufunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo pia unahusisha uwasilishaji wa mada mbalimbali zinazohusu uendelezaji wa sekta ya Korosho, huku wawasilishaji kutoka mataifa mbalimbali wakipata nafasi ya kueleza namna ambavyo sekta ya Korosho inaweza kuendelezwa na kuleta Tija.

Yusufu Nanila ambaye ni Mmoja wa wakulima wa Korosho kutoka Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara na pia Mwenyekiti wa Mkutano wa wadau wa zao Korosho ameeleza kuwa Mkutano huo ni fursa ya kipekee kwa nchi ya Tanzania kuweza kujitangaza kimataifa kuhusu uwezo wake mkubwa uzalishaji wa korosho bora Duniani.

“Miaka yote tulikuwa tunawafuata wadau kuwaeleza juu ya ubora na uwezo wetu wa uzalishaji wa Korosho, sasa mwaka huu tumepata fursa ya wao kuja hapa Tanzania kushuhudia wenyewe yali waliyokuwa wanasikia, tutapata muda mzuri wa kuwaeleza na kuonesha fursa za sekta ya Korosho zinazopatikana Tanzania”

“Mkutano huu unashirikisha wadau wanaohusika na Korosho kutoka karibu kila kona ya Dunia, tumewapokea hata kabla ya mkutano na tutaendelea kuwa nao baadae ili kuweza kuonesha na kuelekeza yale ambayo watataka kuyajua kwa undani zaidi lengo ikiwa ni kuzidi kujenga ushawishi wa wawekezaji kujitokeza katika sekta hii muhimu”  amesisitiza Nanila.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo ba Mifugo, Mariam Ditopile Mzuzuri (Mb) amesema Mkutano huo ni ishara ya Tanzania kuendelea kuvutia Mataifa mengine duniani kutokana na kuwa na sera nzuri za uwekezaji hususan katika kilimo cha korosho.

Amewahakikishia wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika Tasnia ya Korosho Nchini kuwa mazingira ya uwekezaji ni mazuri na bunge linaendelea kuisimamia Serikali ili kuendelea kuvutia uwekezaji zaidi kwa ajili ya kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Sisi kama Kamati ya bunge majukumu yetu ni kuendelea kuisimamia na kuishauri Serikali, na moja ya mambo tunayoyafanya hivi sasa ni kuhakikisha kuwa wawekezaji waoajitokeza kwenye eneo hili la korosho wanakuta mazingira safi ili kama Taifa tuweze kufikia malengo ya ubanguaji wa Korosho zinazozalishwa hapa nchini” amesisitiza Mariam Ditopile Mzuzuri.

Mkutano ambao umeingia siku ya pili unaambatana na fursa mbalimbali kwa wadau wa Korosho kutoka Nchini Tanzania, ambao kama wadau watautumia vizuri unaweza kuwaletea manufaa chanya katika shughuli za kulima, kununua, kubangua au kuuza korosho.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa wadau wote mahususi wa sekta ya Korosho, wanahusika katika Mkutano huu wenye wazo kuu la fursa za uwekezaji kwenye tasnia ya Korosho Tanzania (an insight and investment opportunities in Cashew Industry Tanzania).

Ukiwa na kauli mbiu isemayo “wekeza kwenye Korosho kwa mendeleo endelevu” (invest in cashew for sustainable development), Mkutano huu utashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchi ambazo ni walaji wa korosho ikiwa ni pamoja na Marekani, Ulaya, China, Uarabuni, Mashariki ya Kati, Afrika Kusini na nchi zingine za bara la Afrika.

Mkutano huu unakuja wakati ambapo Bodi ya Korosho Tanzania katika kusimamia maendeleo ya Tasnia ikiwa imeweka malengo makuu matatu ambayo ni: Kuongeza uzalishaji wa korosho ghafi kufikia tani 1,000,000 ifikapo mwaka 2030; Kubangua asilimia 60 ya korosho hizo; na Kuwa na masoko ya uhakika na endelevu ya korosho na bidhaa zake ifikapo 2030 ili kufikia agenda 10/30.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…