BRYSON MSHANA, DAR ES SALAAM
mtwarapressclub@gmail.com

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo Octoba 11, 2023 amefungua Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.

Mkutano huo umejumuisha zaidi ya wadau 500 kutoka nchi 33 zinazozalisha na kula korosho, unatarajiwa kuchukua siku tatu na kumalizika Octoba 13, ambapo mada mbalimbali zinazohusu uendelezaji wa sekta ya Korosho kimataifa zitajadiliwa.

Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde akimpokea Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip mpango, kwa ajili ya kufungua Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam (Tarehe 11-13 Oktoba 2023).

Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Mpango ametoa wito kwa Wizara ya Kilimo kuhakikisha kuwa inafikia azma ya kubangua korosho zinazozaliswa nchini badala ya kusafirisha nje ya nchi zikiwa ghafi, lengo ambalo linatakiwa kutimia ifikapo mwaka 2026.

Amesema kuendelea kuuza korosho isiyochakatwa (ghafi) kunasababisha kupunguza ajira za watanzania, kupunguza mapato ya fedha za kigeni pamoja na upatikanaji wa bidhaa zitokanazo na zao la korosho kama vile maziwa, mvinyo, juisi na mafuta.

Makamu wa Rais amesema ni muhimu mkutano huo ukajadili na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuimarisha huduma za ugani na utoaji pembejeo kwa wakati ili kuongeza uzalishaji wa zao la Korosho, ambalo ni moja ya mazao yanayoliingizia Taifa fedha za kigeni.

Naibu waziri wa Kilimo David Siline akimkabidhi zawadi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip mpango iliyoandaliwa na Bodi ya Korosho Tanzania, ambao ni waandaaji wa Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam (Tarehe 11-13 Oktoba 2023).
Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa mkutano huo kujadili namna bora ya kuwa na mkakati wa kufikia masoko ya zao la korosho kwa usawa.
Awali akimakaribisha Makamu wa Rais, Naibu waziri wa Kilimo David Siline alieleza kuwa tayari kumekuwepo na mikakati ya wizara ikishirikiana na wadau wengine kuhakikisha kuwa korosho ya Tanzania inaongezwa ubora kabla ya kuuzwa nje ya nchi.
Silinde ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya kilimo imeshatenga eneo la ujenzi wa viwanda Wilayani Nanyamba Mkoani Mtwara ambalo linatarajiwa kujengwa viwanda zaidi ya 10 vitakavyowezesha kubangua zaidia ya tani elfu 60 za Korosho.
Amesema kuwa hatua hiyo sio tu kwamba itaongezea thamani Korosho ya Tanzania lakini pia wakulima wataongeza kipato ambacho kitaimarisha uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
“Mhe.Makamu wa Rais mipango ya Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia suluhu Hassan imejielekeza kwenye kumkomboa mkulima wa Korosho kwa vitendo, na ndio maana hata kasi ya kuhakikisha kuwa korosho zinabanguliwa nchini inaenda kwa kasi na nikuhakikishie kuwa sisi wizara tutaikamilisha kwa wakati” amesisitiza Silinde
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip mpango, akionesha zawadi aliyopewa na Bodi ya Korosho Tanzania kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam (Tarehe 11-13 Oktoba 2023).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya CBT Brigedia Jnerali Mstaafu Aloyce Mwanjile, ameeleza kuwa mipango ya kubangua Korosho hapa nchi inayoendelea inalenga kuhakikisha kuwa Sekta ya Korosho nchini inakuwa.
“Bodi ya Korosho imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa inaikuza sekta hiyo na sasa tunao mpango mkubwa wa kujenga viwanda katika eneo la maranje lililopo Halmashauri ya Mji Nanyamba Mkoani Mtwara ambalo tunaamini kuwa litazidi kuiheshimisha korosho” ameeleza Brigedia Jnerali Mstaafu Aloyce Mwanjile

Mkutano huo wa siku tatu (Tarehe 11-13 Oktoba 2023) unashirikisha Zaidi ya wadau 500 kutoka nchi 33 zinazozalisha na kula korosho.

Pamoja na mambo mengine lengo la Mkutano huo ni kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko katika mnyororo wa thamani wa zao la korosho.

Sehemu ya Washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam (Tarehe 11-13 Oktoba 2023).

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…