HAIKA KIMARO, MTWARA
mtwarapressclub@gmail.com
Wakati dunia ikikabiliwa na mabadiliko ya tabia nchi. Shughuli za kinadamu zinaelezwa kuwa chanzo cha mabadiliko hayo ikiwamo ukataji miti bila ya kupanda mingine.
Miti hukatwa kwa sababu nyingi, wapo wanaokata kwasababu ya shughuli za ujenzi na kilimo, lakini ukataji wa miti kwa ajili ya nishati ya kupikia, yaani mkaa na kuni unatajwa zaidi kuchangia uharibifu wa mazingira.
Takwimu za shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira WWF zinaonesha kuwa dunia imepoteza hekta 7 milioni za misitu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kati ya hizo hekta 3.9 milioni zimepotea barani Africa.
Nchini Tanzania inakadriwa kuwa hekta 400,000 za misitu hupotea kila mwaka kutokana na shughuli za binadamu zinazochagiza uharibifu wa mazingira.
Barani Africa wanawake ndiye wahanga wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi, kutokana na ukataji kwa miti hovyo kwa sasa wanalazimika kutumia muda mwingi kwenda porini kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia.
Madhara ya matumizi ya kuni hayaishii kuteketeza misitu pekee, bali pia huathiri afya za wanawake kwa kuvuta moshi wa kuni wakati wa uandaaji wa chakula.
Kutokana na changamoto hiyo Amina Hassan mkazi wa Naliendele wilaya ya Mtwara mkoa wa Mtwara anasema hutumia nishati ya kuni kwa ajili ya matumizi ya kupikia.
Kutokana na upatikaji wake kuwa adimu Amina hulazimika kununua kuni za Sh 2,000 hadi 3,000 kwa siku ili kutosheleza mahitaji ya ya kupikia kwa familia yake ya watu saba.
“Ili niweze kupikia familia yangu milo mitatu inanibidi kununua kuni sio za chini ya Sh 3,000 na kama sina fedha inabidi nisitishe shughuli zangu zote na kwenda porini kukata kuni, lakini kama ningekuwa na gesi nisingekuwa na sababu za kwenda kutafuta kuni na huo muda ningeutumia kuzalisha mali”anasema Amina.
Amidu Hassan ni muuzaji wa mkaa kutoka kijiji cha Mdui anasema anapoandaa mkaa kwa ajili ya biashara huitaji muda na viroba kwa ajili ya kuhifadhia mkaa lakini, hata hivyo biashara hiyo imekuwa ikimsaidia kumudu tu gharama za kuhudumia familia kwenye mambo madogo madogo.
“Mtaji ni muda wako na viroba tu, misitu ya kukata miti iko lakini maajabu toka nimeaza hii biashara mwaka 2009 naweza kuhudumia familia yangu mahitaji ya kujikimu tu lakini sio kusema ni kazi ambazo imenisaidia kuboresha makazi yangu au kuanzisha biashara nyingine ya kudumu” anasema Hassan
Anabainisha katika biashara hiyo changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja na kukamatwa na mamlaka ya maliasili na kupigwa faini na wakati mwingine hulazimika kukimbia na kutekeleza baskeli ili kukwepa adhabu.
“Kuna wakati unachoma mkaa unakuwa sio mzuri, hiyo ni changamoto ya kwanza, lakini unaweza ukakamatwa na watu wa maliasili na kupigwa faini lakini kutokana na ugumu wa maisha kuna muda baadhi wanakwepa kulipa ushuru na inapotokea amekamatwa anakimbia anatekeleza baskeli ambayo ndio ya nyenzo muhimu ya kusafirisha mkaa kwa wateja,”anasema Hassan
Ili kukabiliana na changamoto ya ukataji mkataji miti kwa ajili ya mkaa Serikali ya Tanzania imeanzisha mradi wa kuunganisha wananchi na gesi asilia kwa ajili ya kupikia majumbani.
Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) tayari imefanikiwa kuwaunganishia zaidi ya familia 1500 huduma ya gesi asilia kwa ajili ya kupikia.
Akizungumza na Habitat News, Mhandisi wa Idara ya Biashara ya Mafuta na Gesi kutoka TPDC, Mhandisi Eva Swila anasema mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2019 na hadi kufikia mwaka 2023 zaidi ya nyumba 1,500 zimeunganishwiwa huduma hiyo ikiwemo ngazi ya familia na taasisi zenye watu wengi kama shule, magereza,vyuo na hoteli.
Mhandisi Eva anasema lengo la mradi huo ni watu waweze kunufaika na rasilimali zinazopatikana nchini na kuwapunguzia gharama za kununua kuni au mkaa na kwamba huduma hiyo inaokoa gharama kwa zaidi ya asilimia 40 ikilinganishwa na matumizi ya nishati nyinginezo.
“Unit moja ya gesi asilia inayouzwa Sh 1,000 ina uwezo wa kupikia familia ya watu sita kwa siku moja na hapo ni kwa ile familia ambayo inapika sana, lakin kuna ambao wana uwezo wa kutumia pungufu ya hapo,”anasema Eva
Anasema kwa kuanza mradi huo umeanza kutekelezwa katika mkoa wa Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 shirika hilo linakusudia kuunganisha huduma hiyo kwa nyumba takribani 1,000 katika mkoa wa Pwani na Lindi ambapo takribani Tsh. 6 bilioni zitatumika.
“Mkoa wa Pwani wao wameshaanza kunufaika na matumizi ya gesi asilia kwenye viwanda, matumizi ya nyumbani yataanza mwaka huu wa fedha 2023/25 ambapo zaidi ya nyumba 500 zitaunganishwa lakini pia mkoa wa Lindi zaidi ya nyumba 400 zitanufaika,”anasema Eva
Mwanaid Ally ni mnufaika wa mradi wa gesi asilia kwa ajili ya kupikia nyumbani anasema kwa sasa inamsaidia kuokoa gharama pamoja na muda bila kujali ni wakati wa masika au kiangazi.
“Wakati napikia kwa kutumia mkaa ilikuwa ikifika kipindi cha mvua bei inapanda hadi mara mbili na upatikanaji wake unakuwa mgumu lakini sasa iwe mvua au jua napika wakati wowote na sipotezi muda ile kusema lazima nitumie dakika kadhaa kukoleza mkaa;’anasema Mwanaid
Naye Bryson Mshana ni mkazi wa Railway Mtwara ni mnufaika wa huduma ya gesi asilia kwa ajili ya kupikia anasema licha ya kuwa serikali ilimuunganishia bure huduma hiyo inampunguzia gharama na haitaji wa kuwa na pesa nyingi ili kununua unit za kupikia.
“Kwanza inaokoa gharama na muda, kabla ilikuwa lazima kununua gesi ya mtungi mdogo sio chini ya Sh 20,000 lakini sasa sihitaji kuwa na 20,000 au 5,000 hata nikiwa na Sh 1,000 nina uwezo wa kununua unit na familia ikapika, kwa hiyo inasaidia kubana matumizi,”anasema Mshana na kuongeza;
“Mbali na kuokoa gharama ilikuwa hata kama unapokia gesi ya kawaida ilikuwa lazima kununua na mkaa kwa ajili ya vyakula vigumu kama maharage lakini sasa hivi nikinunua unit za gesi asilia zinatumika kupikia kila kitu na kusave gharama mara tatu,”anasema Mshana
Mbali na matumizi ya gesi asilia kwa ajili ya kupikia majumbani miongoni mwa taasisi zenye idadi kubwa ya watu wanaotumia nishati hiyo ni pamoja na shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara.
Akizungumza Makamu Mkuu wa shule hiyo, Babis Bwire anasema kabla ya kuanza kutumia nishati hiyo walilazimika kutumia Sh 6 milioni hadi 7 milioni kwa mwezi lakini bada ya kufungiwa huduma ya gesi asilia gharama zimeshuka hadi Sh 1.5 milioni na matumizi yakizidi inakuwa Sh hadi 1.7 milioni.
“Kwa upande wa gharama tumesave kutoka sh. 7 milioni mpaka 1.7 milioni, na kwa upande wa taalum kipindi tunatumia kuni kuna wakati ulipofika muda wa chakula wanafunzi ilibidi wasibiri lakini sasa hivi chakula kinakuwa tayari kwa wakati kusubiria wanafunzi na wala hatuna wasiwasi, hivyo tunaishukuru serikali,”anasema Bwire
Mbali na matumizi ya shule pia walimu wa shule hiyo wameunganishiwa nishati hiyo ambapo Bwire anasema kwa sasa anatumia Sh 30,000 kwa mwezi kutoka Sh 90,000.
Somoe Mustafa ni mama wa familia ya watu watano yeye bado anatumia nishati ya kuni kupikia ambapo anasema changmoto anazokumbana nazo ni kutumia muda mwingi pamoja na kuugua macho.
“Kutumia kuni lazima nitenge muda niende porini kuzitafuta ndipo niweze kupika lakini kubwa zaidi la kuumiza wakati mwingine maporini tunakutana na wadudu kama nyoka na ng’e na tunaporudi nyumbani wakati wa kupika kuni huwa zinatoa moshi na kuumiza macho ndio sababu macho yangu unaona ni mekundu,”anasema Somoe.
Kuhusu kama anafahamu matumizi ya gesi asilia kwa ajili ya kupikia Somoe anasema amekuwa akisikia taarifa kwenye vyombo vya habari lakini hana ujuzi nayo.
“Nimekuwa nikisia gesi ya mitungi lakini sasa hivi nasikia kuna nyingine ya kununua kama luku unafungulia tu kama bomba la maji unatumia (gesi asilia) lakini sasa masharti yake naona kwangu itakuwa ngumu kwa sababu sina jiko,”anasema Somoe
Mhandisi wa Idara ya Biashara ya Mafuta na Gesi, Mhandisi Eva Swila anasema kwa sasa hakuna gharama wala mchakato wa kufuata ili mtu kuunganishwiwa na huduma hiyo isipokuwa TPDC wanachangua maeneo ambayo tayari yamefikiwa na mradi.
“Kwa sasa tunachagua maeneo ambayo mradi umefika, yale mabomba ya gesi ya presha ya kawaida, kwa hiyo tunaamua kwa mwaka huu tutaunganisha nyumba kadhaa eneo hilo, lakini pia kwenye hiyo nyumba lazima kuwe na chumba cha jiko kilichopangwa ili kuruhusu mabomba yaweze kuwekwa na sio kwenye zile nyumba unakuta labda jiko ni hapo hapo unapolala au unapikia kwenye kordo,”anasema Eva
Mchumi
Mhadhiri wa Chuo cha Biashara (CBE) Dkt Dickson Pastory anasema gesi ni gharama nafuu zaidi ikilinganishwa na kuni au mkaa kwani matumizi ya mkaa yanaharibu mazingira pamoja na miti kupotea na kuchochote mabadiliko ya tabianchi na ndio sababu sehemu nyingi hata upatikanaji wa mvua ni mdogo lakini pia usafirishaji wa mkaa unatumia ghara zaidi kwenye usafirishaji.
Anasema ni vyema kama serikali itaangalia namna ya kupunguza gharama gesi na kuweka mazingira ya upatikanaji wake ili kupunguza uharibufu wa mazingira.
“Inatakiwa bei zipunguzwe na upatikanaji wake uwepo na isambazwe sehemu mbalimbali kwa sababu hakuna mtu asiyetaka kutumia gesi lakini bei ni gharama, zikipungua watu wengi watakimbilia kwenye gesi na wataachana na mkaa na kuwe na uwezekano wa kupatikana vijijini,”anasema Dkt Pastory
Anasema kwa upande mwingine kutokana na gharama za mafuta kuwa juu baadhi ya wenye magari wamehamia kwenye matumizi ya gesi lakini upatikanaji wake bado ni mdogo huku Dar es Salaam ikiwa na vituo viwili pekee vya kujaza nishati hiyo.
“Matumizi ya gesi yatatusaidia sana kwenye matumizi ya magari na matumizi ya nyumbani, sasa hivi ukisafiri kwenda mikoani utaona miti inavyokatwa hiyo ni hatari sana na inafanyika kwa sababu watu hawana uwezo wa kununua gesi. Iangaliwe njia nzuri kama wataweza kutumia gesi asilia na zile za mituni pia bei upunguzwe,”anasema Dkt Pastory
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






