BRYSON MSHANA, MTWARA
mtwarapressclub@gmail.com
Machi 24 ya kila mwaka, Dunia inaadhimisha siku ya Kifua Kikuu ambayo mwaka huu kitaifa yanafanyika Wilayani Bariadi mkoa wa Simiyu na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Okoa maisha wekeza katika kutokomeza kifua kikuu nchini”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Ibadakuli, Shinyanga akiwa njiani kuelekea Bariadi mkoani Simiyu ambako atakuwa mgeni rasmi kaaika Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani, Machi 24, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Ugonjwa wa Kifua Kikuu au TB, bado unaelezwa kusalia kuwa miongoni mwa magonjwa hatari zaidi duniani, Umoja wa Mataifa (UN) ukiripoti kuwa TB inaua watu wengi zaidi kuliko ugonjwa wowote wa kuambukiza.
Mwaka 2022, Tanzania ilitajwa kuwa ni miongoni mwa nchi 30 zenye maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ambazo zinachangia asilimia 87 ya wagonjwa wote duniani.
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2021 ilionesha kuwa kulikuwa na wagonjwa wapya wa Kifua Kikuu 9.9 milioni duniani kote na kati ya hao wagonjwa milioni 1.4 walifariki.
Mwaka huo wa 2121 Tanzania ilikuwa na wagonjwa wapya wa kifua kikuu 133,000 sawa na wagonjwa 222 kwa kila watu 100,000 ikionesha maambukizi kupungua kwa asilimia 27 ikilinganishwa na miaka mitano ya nyuma.
Mkoa wa Mtwara ni moja ya maeneo ambayo yamekuwa yakiweka mikakati ya kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu, huku jitihada zaidi zikielekezwa katika kuwatambua wagonjwa wenye maambukizi ili waweze kupatiwa matibabu kwa wakati.
Jitihada hizi ambazo zimehusisha sekta ya afya, jamii na wadau wengine katika Wilaya zote za Mkoa wa Mtwara, zimewezesha wagonjwa 4, 884 kutambulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu katika ya mwaka 2021 hadi 2022.
Mwaka 2021 wagonjwa 2,405 walitambuliwa kuwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu, huku wengine 2,479 wakigundulika katika mwaka wa 2022 ikiwa ni ongezeko la wagonjwa 74.
Akizungumza ofisini kwake katika mahojiano maalum na www.mtwarapressblog.co.tz Machi 24, 2023 iliyotaka kujua hali ya ugonjwa wa kifua kikuu kimkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Dr Hamadi Nyembea amesema kuwa jukumu la kwanza ni kuwatambua wagonjwa ili waweze kupatiwa tiba.
“Ugonjwa huu unaathiri rika zote, ukishaupata ni lazima utibiwe na kwa mkoa wa Mtwara ugonjwa bado upo, hivyo niendelee kuwashauri wadau na jamii kuendelea kushirikiana ili wale wanaoonekana kuwa na dalili na kubainika kuwa na Kifua Kikuu waweze kupatiwa tiba”
“Tunaendelea kuongeza uwezo wa kuwabaini wagonjwa, hilo ndilo jambo kubwa kwa sababu usipowabaini huwezi kuwatibu ndio maana wagonjwa waliobainika tumehakikisha wamepata tiba kwa 98%” amesisitiza Dr Nyembea
“Msisitizo wetu ni kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano pale inapohisi kuna mtu mwenye dalili za Kifua Kikuu katika maeneo yao, mfano hizo takwimu za mwaka 2021 na 2022 jamii ilisaidia sana kuwabaini na kuwapeleka wagonjwa kwenye vituo vya afya kisha serikali ikahakikisha wanapata tiba na kupona” ameeleza Dr. Nyembea
Siku ya Kifua Kikuu Duniani inaadhimishwa wakati ambapo Serikali ya Tanzania ikifanya jitihada za kudhibiti ugonjwa huo, ikisema kuwa imedhamiria kuendelea kushirikiana na wadau katika sekta zote ili kudhibiti na kuutokomeza TB ifikapo mwaka 2030.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi wakati wa kikao na Makatibu Wakuu wa Wizara kilichofanyika Machi 21, 2023 katika ofisi za Waziri Mkuu Jijini Dodoma, alieleza umuhimu wa kushirikiana ili kutokomeza ugonjwa kifua kikuu nchini.
“Ili kudhibiti ugonjwa huu wa Kifua Kikuu ni muhimu kushirikiana na wadau wengi kama sekta ya afya, wadau sekta ya elimu, sekta ya usafirishaji na sekta nyingine mbalimbali.” alisema Dkt. Yonazi

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akizungumza wakati wa kikao na Makatibu Wakuu wa Wizara kilichofanyika Machi 21, 2023 katika ofisi za Waziri Mkuu Jijini Dodoma.
Kwa upande wake Mtaalamu Mshauri kutoka Stop Tb Partnership (STP) Bw. Oscar Mukasa wakati akiwasilisha taarifa ya mpango kazi wa kudhibiti Kifua Kikuunchini, amesema watu wenye hatari zaidi ya kupata Kifua Kikuu ni pamoja na watu wanaoishi kwenye makazi duni, Watoto, Wavuvi na Wanaoishi Bweni.
Amesema Watu wenye VVU, watu wenye Utapiamlo, wachimbaji madini, wanaoishi na mgonjwa wa Kifua Kikuu, watoa huduma za afya na wanaotumia madawa ya kulevya kwa kujidunga sindano.
Bw. Mukasa amewashauri wanaoishi katika mazingira hayo kuchukua tadhari za kujikinga na ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB).
Dalili za ugonjwa wa Kifua Kikuu ni pamoja na kikohozi cha muda mrefu, kukosa hamu ya kula, kukohoa damu, homa, kutokwa jasho usiku, kupungua uzito na uchovu.
Inaelezwa kuwa ugonjwa wa Kifua Kikuu ni ugonjwa unaotibika lakini wengi huacha kutumia dawa kabla ya muda waliopangiwa na hii imekuwa sababu kubwa ya wagonjwa kuugua kwa muda mrefu zaidi.
Kwa upande wa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Kitengo Shirikishi cha Ukimwi ,Homa ya Ini na Ukoma imedhamiria kuongeza mapambano ili kufikia malengo ya kuutokomeza Ugonjwa wa Kifua Kikuu ifikapo 2030
Naibu Mkurugenzi Idara ya Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Fatma Kabole, amesema katika kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya mwaka huu Wizara ya Afya imeandaa mikakati madhubuti ya kupambana na janga hilo kwa Kuongeza Mashine za kisasa zenye uwezo mkubwa zaidi wa kupima Sampuli za wenye dalili za Ugonjwa huo.

Naibu Mkurugenzi Idara ya Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Fatma Kabole akizungumza wakati wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari juu ya hali ya ugonjwa wa Kifua kikuu Machi 23,2023 PICHA NA FAUZIA MUSSA – MAELEZO ZANZIBAR
“kuna wimbi kubwa la watu wenye dalili za ugonjwa huu katika jamii na bado hawajafika katika vituo vya afya kwa uchunguzi hivyo nawaomba Wanachi kufika katika vituo vya Afya mara waonapo dalili za Ugonjwa huo ikiwemo kukohoa kwa wiki mbili au zaidi na kupata makohozi ya damu,”Ameshauri Fatma.
Naye Meneja wa Kitengo Shirikishi Ukimwi Homa ya Ini na Ukoma Zanzibar Mohammed Jabir Dahoma, amesema kundi la Wanaume Kati ya miaka 25 Hadi 55 wapo hatarini zaidi kuathirika na ugonjwa huo kutokana na harakati zao za kazi na mfumo wa maisha .
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinasema kuwa upande wa Zanzibar jumla ya wagonjwa 1077 waliripotiwa wana ugonjwa huo mwaka 2022, ikilinganisha na wagonjwa 1090 waliogunduliwaa mwaka 2021, huku 15 kati yao waligundulika kuwa na kifua sugu.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






