BRYSON MSHANA, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule kubwa ya wasichana Mkoani Mtwara, ambayo itakuwa maalum kwa ajili ya vipaji vya Sayansi.

Dkt. Samia ameeleza hayo leo Septemba 16, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa halmashauri ya Mji Nanyamba, wakati akiwa njiani kuelekea wilayani Tandahimba katika Mkutano wa hadhara, ikiwa ni sehemu ya ziara yake Mkoai Mtwara.

Dkt. Samia amesema kuwa ujenzi wa shule hiyo ni muendelezo wa Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha kuwa inawekeza katika elimu kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari – (Sequip) ili kuzalisha madaktari, wahandisi na wataalm wengine wa kike ambao watakuja kushika nafasi mbalimbali miaka ijayo.

“Shule tutakayojenga haitakua na wasichana wa kutoka huku peke yake, watatoka maeneo mengine ya nchi yetu, tuchunge wasichana Wetu, Kina Samia watatoka huku Nanyamba” ameeleza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan

Aidha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wakazi wa Mtwara kuwaacha watoto wakike watimize ndoto zao kielimu, wakati serikali ikiendelea kuwajengea misingi bora ya kupata elimu.

“Lakini mkianza kuwashughulikia mapema hivi mnavyofanya, hawa wasichana hawatafika kule, shule tunayojenga haitakuwa na wasichana haitakuwa na watoto na wakiwepo watatoka mkoa mwingine kuja huku kwenu.”

“Nawaomba sana kina mama, kina mama baada ya mavuno mambo ya kuwacheza wasichana na kuwaambia sasa mpo huru nendeni yasiwepo, tuchunge wasichana wetu wakina Samia watatoka huku Nanyamba, mkiwashughulikia mapema hawa hawatakuja juu.” Dkt. Samia.

Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo Mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi ya siku nne itakayohitimisha Septemba 17, 2023.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…