BRYSON MSHANA, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamis Munkunda, ameipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania –TPA, kwa kuwa mstari wa mbele katika kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo zinazokuwa zimeandaliwa Mkoani Mtwara.

Mkuu huyo wa Wilaya ametoa pongezi hizo Novemba 23, 2023 wakati akihitimisha siku nne za mafunzo kwa waandishi wa habari, maafisha habari na wakuu wa Taasisi za Serikali ikiwa ni sehemu ya shughuli za Jukwaa la habari na Mawasiliano lililozinduliwa Novemba 20, 2023.

Jukwaa hilo lililoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC),  lilizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanal Ahmed Abbas, likidhaminiwa na Taasisi mbalimbali  ikiwemo TPA ambao walikuwa wadhamini wakuu.

“Lakini mimi pia niwashukuru TPA, mnifikisheni salamu kwa viongozi wa TPA, kila mara tunapowafikia katika mambo yetu ya mkoa wanaungana nasi kwa ajili ya kutoa hamasa lakini pia na ushiriki wao”

“Tunafahamu pia wanazo taarifa nyingi na wao wanafanya biashara kama zilivyo Taasisi nyingine, kwa hiyo pia watumie vema jukwaa hili na waandishi wa habari kuuelezea umma ili kuwafikishia wateja bidhaa zao wanazoziuza au huduma wanazozitoa pale Bandarini”

Awali akitoa salam za kuhitimisha Jukwaa hilo, Afisa Uhusiano Mkuu wa TPA Levina Kato alivishukuru vyombo vya habari kwa kuendelea kuandika habari za maendeleo, ikiwepo uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali ya Tanzania katika Bandari ya Mtwara.

“Tuendelee kuandika habari za hatua kubwa za kiuchumi na uwekezaji zinazoendelea kupigwa na serikali ya awamu ya sita, TPA inaahidi ushirikiano kwa wanahabari wakati wote kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu” alisisitiza Bi. Levina

Mkoa wa Mtwara umekuwa Mkoa wa kwanza kuzindua Jukwaa la Habari na Mawasiliano, lenye lengo la kuboresha mawasiliano na uhusiano baina ya wadau wa habari, ili kushirikiana kwa pamoja katika kuleta maendeleo.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…