BRYSON MSHANA, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Novemba 22, 2023 Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (sera, bunge na uratibu) Ummy Nderiananga alifungua mafunzo ya kuzijengea uwezo kamati za usimamizi wa maafa kutoka Wilaya za mkoa wa Mtwara.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, yaliambatana na ziara ya Naibu Waziri Ummy Nderiananga kukagua utekelezaji wa hatua zinazochukuliwa kuzuia na kujiandaa kukabiliana na maafa kwa kamati za usimamizi wa maafa mkoa wa Mtwara.

Vikao kazi hivi, mafunzo na ziara imefika pia katika mikoa ya Lindi na Ruvuma, hivyo kutoa fursa kwa mikoa mitatu ya kusini mwa Tanzania kufikiwa na kupata elimu ya kukabiliana na maafa kupitia kamati za usimamizi wa maafa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Naibu Waziri Ummy Nderiananga aliwataka Viongozi katika Mikoa na Halmashauri nchini, kuweka jitihada za kujiandaa kuzuia na kukabiliana na maafa hususan katika kipindi hiki ambacho kumetangazwa uwepo wa Mvua za Elnino zilizotabiriwa na Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Nchini (TMA).

Juhudi hizi za Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu zinafanyika katika kipindi ambacho tayari mikoa mbalimbali nchini imeshaanza kupata mvua za Elnino, na kushuhudia athari za mafuriko zilizosababisha maafana na uharibifu wa miundombinu.

Naibu Waziri Ummy Nderiananga anasema kuwa kuwa lengo la mafunzo na ziara yake katika mikoa ya kusini ni kukumbushana wajibu muhimu wa kila mmoja kuwajibika katika eneo lake ili kuokoa maisha na kulinda mali za wananchi.

“Kamati hizi zina wajibu wake kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya Mwaka 2022 na Kanuni zake, ambayo ilizianzisha kwa ajili ya usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji au Mitaa”

“Jukumu la msingi la Kamati hizi ni kuchukua hatua kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea” anasisitiza Naibu Waziri

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas, anaamini kuwa juhudi zinazofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu zimesaidia jamii kujikinga na maafa katika maeneo mbalimbali nchini, na zinapaswa kuungwa mkono na wadau wengine, huku akisisitiza kuwa maafa hayapo kwenye mvua pekee.

“Sisi Mkoa wa Mtwara ni moja ya mikoa yenye shughuli nyingi za uwekezaji kupitia mkakati wetu wa kuifungua Mtwara kiuchumi, sasa shughuli hizi huwa zinaweza kupelekea mabadiliko ya kimazingira na kusababisha majanga mbalimbali na kupelekea maafa, hivyo juhudi hizi za Ofisi ya Waziri Mkuu tunazichulia kwa umuhimu mkubwa sana”

“Kamati zote zilizohusika katika mafunzo yale nazielekeza kuhakikisha kuwa zinazingatia yote yatakayofundishwa na kuendelea kuyafanyia kazi kwa vitendo ili tuendelee kuwakinga wananchi na majanga mbalimbali” anaeleza Kanali Abbas

Kwa upande wa wabunge wa mkoa wa Mtwara ambao ni wawakilishi wa wananchi Hassan Mtega Mbunge wa Mtwara Mjini na Anastazia Wambura ambaye Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Mtwara, wanaamini kuwa kikao kazi cha Novemba 22, 2023 kilichoambatana na mafunzo kitasaidia kuwambusha wadau juu ya umuhimu wa kujiandaa na kujikinga na maafa.

“Hili ni Jambo jema sana, na limekuja wakati muafaka ambao mvua zimeanza kunyesha maeneo mengine, lakini sio mvua tu maana jiografia ya mkoa wetu kunaweza kuwa na vimbunga, milipuko ya viwandani nk. hivyo kwa hiki kilichofanyika ni tahadhari nzuri naipongeza ofisi ya waziri mkuu kwa niaba ya wananchi wa Mtwara Mjini” anasema Mtenga

“Mimi siangalii tu katika majanga ya mvua, lakini hata kunapotokea milipuko ya magonjwa athari zake zinakuwa kubwa hususan kwa watoto na akina Mama, hivyo kwa kukumbushana kulikofanywa na ofisi ya waziri mkuu, ni matumaini yetu kuwa sasa kamati zetu zimejizatiti na zipo kwenye maeneo mbalimbali zinaendelea kuwaelimisha wananchi” anaongeza Anastazia Wambura

Kwa nyakati tofauti katika mwaka huu wa 2023, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kupitia vyombo vya habari pamona na tovuti yake ya www.meteo.go.tz imekuwa ikitoa tahadhari juu ya mvua za kiwango cha juu zinazoweza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

Kujengewa uwezo kwa kamati za usimamizi wa maafa kutoka Wilaya za mkoa wa Mtwara na mikoa mingine ya kusini mwa Tanzania, ni ishara kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imechukua tahadhari za kutosha na kinachofuatia ni wadau kuendelea kuzingatia tahadhari na kamati zilizowezeshwa ziendelee kutendea kazi kwa vitendo mafunzo zilizoyapata.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…