RAMLA MASALI, MTWARA
mtwarapressclub@gmail.com
Mabasi ya abiria yanayofanya safari ndani ya wilaya ya Mtwara na maeneo jirani, yamerejea rasmi stendi ya Zamani ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas.
Mtwara Press Blog, Novemba 06, 2023 imefika katika stendi hiyo na kushuhudia mabasi hayo yakipakia na mengine kushusha abiria.
Baadhi ya madereva wamepongeza hatua hiyo ya serikali na kueleza kuwa “kwa mfano ile stendi ile we mwenyewe ukienda kuangalia yani kipindi cha upepo ni vumbi tu tunakula kipindi cha mvua ni tope.” Amesema Athuman Salumu ‘Kipande’ aliyejitambulisha kuwa meneja wa magari ya Nanguruwe.
Licha ya kupongeza hatua ya kurejesha mgari stendi hiyo, baadhi ya madereva pia wamelalamikia kitendo cha kutakiwa kupita soko la Chuno na Hospitali ya Rufaa ya Ligula, wakati wanafanya safari zao.
“Kama ni gari ndogo Hiaice za hapa mjini hazina shida, lakini kama ni gari kubwa zinazoenda Nanyamba, zinazoenda Tandahimba, sio kuonekana kwamba lazima zipitie Chuno wapi ni mbali abiria anakaa muda mrefu kusubiria abiria mwingine tena, wakishajaa abiria aanze tena kuzungusha hapa mjini tena ni mbali.” Amesema Abdul Lipondo.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani Mkoa wa Mtwara Nassoro Mansour, amesema zoezi la mabasi kurejea stendi hiyo limeenda vizuri na amewashukuru madereva kwa kutekeleza agizo hilo na Mkuu wa Mkoa.
Kisha Mansour akazungumzia hoja ya baadhi ya madereva waliolalamikia kupita soko la Chuno na Hospitali ya Ligula, kuwa jambo hilo halikuwahi kuzungumzwa kwenye vikao vya awali walivyokaa ambavyo hata madereva walishiriki na kwamba ndio kwanza amelisikia kwa mara ya kwanza stendi hapo.
“Niseme tu binafsi nalichukuwa lakini nitoe angalizo moja, kwa sasa tufuate huu utaratibu ambao umewekwa huu utaratibu umewekwa na baraza la madiwani kwasababu mji wowote una taratibu zake namna ya gari za abiria kupita, lengo ni wananchi wa maeneo hayo kupata huduma.” Ameeleza Mansour.
Mabasi yaliyorejeshwa stendi ya zamani ni yale ambayo hayapo kwenye ratiba ya kufanya safari za kwenda makao makuu ya Wilaya na Mikoa mbalimbali.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






