HAIKA KIMARO, MTWARA
mtwarapressclub@gmail.com
Kutokana na baadhi ya wanawake kukosa au kunyimwa uhuru wa kijieleza ndani ya taasisi mbalimbali au maeneo ya kazi kunatajwa kudhorotesha utendaji kazi na ufanisi na hivyo kuonekana hawawezi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kukosekana kwa uhuru huo kunapelekea wengi kukaa kimya na kushindwa kujieleza kuhusu mambo wanayokutana nayo katika jamii na katika maeneo ya kazi kwa hofu ya kupoteza kazi na hivyo kuishi katika msongo wa mawazo.
Hata hivyo baadhi yao wamekuwa hawashirikishwi katika masuala ya kutoa maamuzi na hivyo kujiona kama hawana uhuru wa kuhoji hata pale mambo yanapoharibika.
Lydia Moses (sio jina lake halisi) Mkazi wa Magomeni wilaya ya Mtwara anasema alipoteza ajira yake baada ya kunyimwa haki ya uhuru wa kujieleza na kusikizwa kutokana na changamoto alizokuwa akikumbana nazo kipindi akiwa kazini kwani zilikuwa nje ya uwezo wake na hata alipofanya maamuzi magumu jamii iliyomzunguka ilimshangaa.
“Nilipoteza ajira yangu 2021 baada ya mwajiri wangu kukataa kunipa nafasi ya kunisikiliza, nilikuwa nafanyiwa unyanyasaji wa kijinsia na aliyekuwa mume wangu, muda mwingine alinipiga hadi nikashindwa kufika kazini na hata nilipojaribu kumueleza kiongozi wangu eneo la kazi hakutaka kunisikiliza kabisa,”anasema Lydia
Lydia ansema licha ya kukosa fursa ya kusikilizwa kazini aliamua kupoteza ajira yake lakini bado mume wake hakuwa akimuhudumia zaidi ya kuendelea kumnyanyasa.
“Baada ya kupoteza kazi nililazimika kushinda nyumbani na muda mwingi niliishia kuambulia maneno ya kufedhehesha kutoka kwa mume wangu na hivyo niliamua kuondoka ili kulinda amani yangu lakini jamii nayo haikunielewa wengine walinishangaa nakubali vipi kupoteza kazi na mume lakini hawakuwa wanajua machungu nayopitia,”anasema Lydia
Kutokana na urasimu huo, mkazi wa Chikongola Manispaa ya Mtwara Mikindani, Neema Bakari anasema mwajiri anapomnyima mfanyakazi uhuru wa kujieleza juu ya changamoto anazopita hasa mwanamke kwanza anakosa kujiamini kwa kile anachokifanya na kuvunjika moyo kwa anayopitia nje ya kazi au yanayotokea sehemu za kazi na hata kukosekana kwa ufanisi wa kazi.
Anasema wakati mwingine watu huwadhara kutokana na jinsi zao na kuona hawana uwezo wa hata kama wanaweza kutoa mawazo ya kuleta mabadiliko chanya maeneo ya kazi ili kutoka eneo moja kwenda lingine.
“Unaweza kufanya kazi na mwanamke na ana mawazo mazuri kuliko kile unachokifikiria lakini kumnyima fursa ya kuzugumza ni tatizo kwake kwa sababu huwezi kupata kilicho ndani yake. Sikila mwanamke hawezi kuwa na maamuzi au mawazo sahihi..kwa hiyo unakuta kunyumwa uhuru hawezi kusonga mbele na atafanya kazi bila weledi ili tu siku ziende alipwe,”anasema Neema
Betina Contine anasema changamoto nyingine inayopelekea wanawake washindwe kujieleza ni suala a hedhi kutochukuliwa kwa uzito wake na hivyo wakati mwingine kupelekea ufanisi wa kazi kuwa chini.
“Kila mwanamke anakuwa na kalenda yake sasa tunatofautiana inapotokea mtu ameshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo inachukuliwa tofauti lakini kama mwanamke angekuwa na uhuru wa kujieleza kazini suala la hedhi lingezungumziwa na kupewa kipaumbele pale inapotekea mtu ameshindwa kutekeleza majukumu yake,”anasema Betina
Shaban Said ni baba wa familia ya watoto watatu anasema mwanamke anapokosa uhuru wa kujieleza au anapojieleza na kutochukuliwa kwa uzito kunachochoa wanawake kuendelea kuwa chini na kuonekana kama hawezi kuwa kiongozi au kusimama mbele ya wanaume kutokana na baadhi ya jamii kuwa na mtizamo hasi kwa wanawake.
“Watendaji waweke mfumo utakaosadia wanawake kuweza kutoa maoni yao ili waweze kusaidika katika jamii kwa sababu na wao wana mchango mkubwa katika kuleta maendeleo kama watasikilizwa na kupewa nafasi kama ilivyo kwa baadhi ya wanaume,”anasema Said
Naye Gasper Charles anasema kukosekana kwa uhuru wa kujieleza kwa wanawake kunaathiri utendaji kazi wao kwani ili mtu awe na utendaji ulio bora ni lazima awe na uhuru wa kutoa mawazo juu ya anachokitenda au kukipitia.
“Tumekuwa tukishuhudia namna wanawake wanakumbana na matatizo mbalimbali hasa wakiwa sehemu za kazi na wanashindwa kwani hakuna mazingira yamewekwa na yanayowapa fursa kuzungumza kile kinachowakabili mfano udhalilishaji katika maeneo ya kazi kama kukosekana kwa madawati ya jinsi ambayo yanatoa fursa kwa wanawake kutoa maoni na kuwasilisha changamoto zinazowakabili.
Bryson Mshana ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kijamii anasema sula la kujieleza ni suala la kikatiba na limeelezwa katika sura ya kwanza kuanzia ibara ya 18 kila raia kila mtu katika eneo lolote ana uhuru wa kujieleza.
Anasema katika kujieleza ndiko ambako mtu anaweza kusema amekwama wapi, ameshindwa wapi au nini kifanyike ili kuboresha kazi anayoifanya, hivyo anapokosa uhuru wa kijieleza inaathiri utendaji wake wa kazi na kuleta mdororo wa kazi ofisini.
“Anapokosa nafasi hiyo anashindwa kujipambanua na kujionesha kwamba yeye hodari katika eneo lipi, kujieleza kule anaweza kujipambanua masuala mbalimbali aidha yeye au kwa wenzake, unapomnyima uhuru atafanya kile kidogo ambacho anatakiwa na anapobaki nacho bila kusema inakuwa yeye na ofisi wote wamekosa,”anasema Mshana
Hata hivyoo anasema wanawake wanapokosa uhuru wa kujieleza kumefanya uwezo wa wanawake kutoonekana na kufifisha malengo yao ambayo wangeweza kuyafikia kwa muda mfupi au kwa muda mrefu.
Mkurugenzi wa Shirika la Door of Hope Tanzania, Clemence Mwombeki anasema mwanamke anapokosa uhuru wa kujieleza ananyimwa fursa ya kushiriki kikamilifu kwenye majukwaa ya maamuzi na kutoa nafasi ndogo au kunyiwa kabisa ujasiri wa kushiriki kwenye maoni ya mgawanyo wa rasilimali kuanzia ngazi ya familia, jamii na Taifa.
Anaongeza hali hiyo inawakosesha uhuru na ujasiri wa kusemea na kuripoti masuala nyeti yanayowasibu hususani vitendo vya ukatili maeneo ya nyumbani, kazini, sokoni na maeneo ya wazi pamoja na kuwakosesha nafasi ya kuonyesha vipawa vyao, na kipee inaua vipaji na kuondolewa hali ya ukuaji na kujiongezea thamani.
“Inawapa nafasi finyu ya kushiriki kikamilidu kwenye Nyanja zote za maisha hasa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiteknolojia,”anasema Mwombeki na kuongeza;
“Kukosa uhuru wa kujieleza pia kunaleta ushiriki hafifu kwenye masuala yanayohusu afya ya uzazi, uzazi wa mpango, imani, mila na desturi, uzalishaji na maoni mengie yanayohusu kundi la wasichana na wanawake,”anasema
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






