BRYSON MSHANA, MTWARA
mtwarapressclub@gmail.com
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesaini hati ya makubaliano ya ujenzi wa miradi Mitatu ambayo ni kituo cha Afya, kituo cha Polisi na uwekaji wa Taa za Barabarani kata ya Msimbati, halmashauri ya wilaya ya Mtwara Mkoani humo.
Hafla hiyo imefanyika Novemba 24, 2023 kata ya Msimbati halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo Mwanahamisi Munkunda, ambapo makubaliano hayo ni baina TPDC na viongozi wa Halmashauri ya wilaya Mtwara, Jeshi la Polisi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Hayo yanajiri takribani wiki moja tangu Naibu Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznaia na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko afanye ziara Mkoani Mtwara, ambapo sehemu ya maagizo yake aliyoyatoa kwa TPDC ilikuwa kutatua changamoto walizonazo wananchi wa kijiji cha Msimbati ikiwemo barabara na kituo cha afya.
Dkt. Biteko alitoa maagizo hayo tarehe 14 Novemba, 2023 wakati aliposimama katika Kijiji cha Msimbati wilayani Mtwara, Mkoa wa Mtwara ili kuzungumza na wananchi akiwa anatokea kukagua visima vya kuzalisha na mitambo ya kuchakata Gesi ya Mnazi Bay iliyopo katika Kata ya Msimbati wilayani humo.
“Changamoto kwenye miradi hii zinatokea lakini lazima awepo mtu ambaye ni daraja kati ya Serikali na Wananchi, na Mtu huyu analipwa mshahara kwa kazi hiyo, haiwezekani Waziri au Rais kuja kutoa taarifa kwa wananchi wakati kuna mtu kaajiriwa kwa kazi husika, wananchi hawa wanapaswa kupata taarifa.” Alisisitiza Dkt.Biteko
Akizungumza hii leo wakati wa utiaji saini huo wa mkataba wenye thamani ya Bilioni 1.4, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda, amemtaka Mkurugenzi wa TPDC Mussa Makame, kuhakikisha miradi hiyo inaanza mara moja na itekelezwe ndani ya miezi Mitatu ikamilike.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mussa Makame, amesema gharama ya miradi yote miratu ni shilingi Bilioni 1.426.
Hafla hiyo imeshuhudiwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtwara Vijijini Nashiri Pontiya, ambaye amewasisitiza wananchi kujitolea katika hatua za awali za ujenzi wa miradi hiyo, pamoja na kuwa walinzi wa vifaa.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






