HUSNA HASSANA, MTWARA

Wakazi wa Kata ya Chuno ,Shangani pamoja na watumishi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wamekusanyika Zahanati ya Chuno kwaajili ya kumwaga zege kwenye jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na jengo la Wodi ya kina mama na upasuaji (Combined Maternity Ward and Theater) ikiwa ni Mradi wa upanuzi wa Zahanati hiyo kuwa Kituo cha afya.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Gwakisa Mwasyeba amesema kukamilika kwa mradi huo utasaidia wananchi wa maeneo hayo kutotembea umbali zaidi ya kilomita 3 kwaajili ya kufuata huduma za afya.

Gwakisa ameongeza kuwa upanuzi wa zahanati hiyo ambayo inakwenda kuwa Kituo cha afya unahusisha upanuzi wa jengo la wagonjwa wa nje(OPD),jengo la wodi ya kina mama na upasuaji (Combined Maternity Ward and Theater),ujenzi wa maabara (Laboratory),kichoma taka (Incinetory) na jengo la kufulia (laundry).

Mradi huo unatarajiwa kukamilika Oktoba,2025 na kuanza kutoa huduma Novemba,2025 hivyo amewaomba wananchi kuendelea kusimamia kwa karibu kwa kila hatua ya ujenzi huo pamoja na kutunza majengo hayo kwani majengo hayo ni ya wananchi na sio ya Halmashauri au mafundi.

Nae Katibu Tawala Wilaya ya Mtwara Waki Mwalingo amesema serikali imewekeza kiasi cha shilingi milioni 660 kwaajili ya mradi huo na kuongeza kuwa ushiriki wa wananchi kwenye miradi mbalimbali inaonyesha kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni serikali ya uwazi na inawafanya wananchi kujua ubora wa miradi na fedha zinazotumika katika miradi hiyo.

Nasra Mohamed Mkazi wa Kata ya Chuno ameishukuru serikali kwa upanuzi wa zahanati hiyo kwani itawasaidia kuokoa maisha ya kina mama kwa kujifungua kwa wakati.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…