BRYSON MSHANA, MTWARA

Wananchi katika Kata ya Msimbati Halamashauri ya Mtwara Mkoani Mtwara, wameishukuru na kuipongeza serikali kupitia kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko kufuatia kukamilika kwa ujenzi na kufunguliwa kwa Kituo cha Afya Msimbati, huku zaidi ya watu 12,000n wakitarajiwa kunufaika na kituo hicho.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti , Wananchi hao wameeleza kuwa awali walikumbana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kupata huduma za afya, lakini baada ya maelekezo ya Dkt.Biteko aliyoyatoa mwishoni mwa mwaka 2023 hatimaye ujenzi umekamilika.

Issa Mfaume Chande, Mzee wa Kijiji cha Msimbati, amesema kuwa kabla ya ujenzi wa kituo hicho, walikuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, hivyo, ufunguzi wa kituo hicho utawasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto hiyo.

Fatuma Waziri na Zaituni Lipemba, kwa upande wao, wameelezea furaha yao kwa kupata huduma za afya karibu, huku wamesisitiza kuwa ujenzi wa kituo hicho umeleta nafuu kubwa kwao.

“kwakweli mimi niishukuru Serikali na nimshukuru Rais Mama Samia na Waziri Dkt.Biteko kwa ukombozi huu waliotuletea, sisi akina mama wa msimbati tulikuwa tunapata shida sana kutokana na kukosa huduma za afya hapa Kijijini, lakini kwa sasa tumeondolewa usumbufu mkubwa” amesema Zaituni

Naye Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Msimbati, Henri Hatia, ameelezea kuwa uwepo wa kituo hicho umepunguza kwa kiasi kikubwa umbali kwa wananchi wa vijiji vya Msimbati, ambao sasa wanapata huduma za afya kwa urahisi zaidi.

Ameongeza kuwa tangu kufunguliwa kwa kituo hicho na kuanza kutoa huduma rasmi, kila siku wananchi wanapata huduma za afya, na kadiri siku zinavyoenda idadi itazidi kuongezekwa kulingana na uhitaji wa wanachi.

“Tumejipanga vizuri kuwahudumia wananchi, tumeshaanza kuwapokea na kuwahudumia, mfano leo tu hapa tumeshahudumia wananchi zaidi ya 20 na wengine wanaendelea kuja na jinsi siku zinavyoenda watazidi kufika hapa kupata huduma mbalimbali” amesema

Kituo cha Afya Msimbati ni matokeo ya ziara ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, ambayo ilimpelekea kutoa maagizo kwa shirika la TPDC kuhakikisha kuwa vijiji vinavyopitiwa na miradi ya gesi vinawekewa miundombinu ya kuwasaidia wananchi kupata huduma mbalimbali.

Dkt. Biteko alitoa maagizo hayo tarehe 14 Novemba, 2023 wakati aliposimama katika Kijiji cha Msimbati wilayani Mtwara, Mkoa wa Mtwara ili kuzungumza na wananchi akiwa anatokea kukagua visima vya kuzalisha na mitambo ya kuchakata Gesi ya Mnazi Bay iliyopo katika Kata ya Msimbati wilayani humo.

Katika ziara hiyo,Dkt. Biteko aligundua uwepo wa changamoto ya kutokuwepo kwa kituo cha afya, ukosefu wa Taa za barabarani, na uhaba wa umeme wa uhakika katika kata za Madimba na Msimbati hivyo kutoa maagizo ya kuanza mchakato wa kutekeleza miradi ya kuboresha huduma za afya na miundombinu katika maeneo hayo.

Maagizo hayo ya Dkt.Biteko yametekelezwa ndani ya mwaka mmoja, ambapo tayari katika eneo la Msimbati pekee kumejengwa kituo cha Afya, Ujezi wa kituo cha Polisi sambamba na uimarishaji wa miundombinu ya barabara.

Check Also

SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI USHIRIKI WA WADAU KATIKA MAENDELEO YA MAKAZI NCHINI

Na Munir Shemweta Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ushiriki wa wadau katika…