BRYSON MSHANA, MTWARA
0787 568 733
MINADA ya ununuzi wa zao la Korosho nchini Tanzania kwa msimu 2023/2024 imefunguliwa rasmi Oktoba 20, 2023 ambapo wastani Tani 18,000 zilipelekwa sokoni na kuuzwa kwenye minada miwili ya kwanza iliyofanyika Mkoani Mtwara kupitia vyama vikuu vya Ushirika vya Tandahimba – Newala (TANECU) na Masasi- Mtwraa – Nanyumbu (MAMCU).
Kwa upande wa Mkoa wa Lindi Vyama Vikuu vya Usirika Ruangwa – Nachingwea – Liwale (RUNALI) na LINDI Mwambao kinachojumuisha Wilaya za Lindi na Kilwa vilipeleka Sokoni na kuuza kiasi cha Tani 9.8 elfu katika minada iliyofanyika mwishoni mwa wiki (Octoba 21 na 22, 2023).
Minada hiyo minne ya awali iliyofanyika katika mikoa ya Mtwara na Lindi ilijumuisha jumla ya tani 10.3 Elfu za MAMCU, 7.7 Elfu za TANECU, 7.9 Elfu za RUNALI na 1.8 Elfu za LINDI Mwambao ikiwa ni wastani wa jumla ya Tani 28 elfu zilizopelekwa sokoni na kuuzwa kwa bei ya kati ya Shilingi 2,050/= (Bei ya juu) na 1,900/= (Bei ya Chini).
Bei za juu katika minada ya kwanza kwa msimu huu wa 2023/2024, zilizofanyika kati ya Tarehe 20 na 23 Octoba 2023, hazina tofauti sana na zile za msimu uliopita 2022/2023 zilizofanyika nati ya Tarehe 21 hadi 23 Oktoba, 2022 ambazo TANECU Ltd bei ya chini ilikuwa shilingi 1,630/= na bei ya juu shilingi 2,011/=, wakati katika Chama cha MAMCU Ldt bei ya chini ilikuwa shilingi 1,800/= na bei ya juu shilingi 2,000/=.
Kwa upande wa Mkoa wa Lindi, Msimu 2022/2023 kupitia chama kikuu cha LINDI Mwambao Ltd bei ya chini ilikuwa shilingi 1,507/= na bei ya juu ilikuwa shilingi 1,900/=, na RUNALI Ltd bei ya chini ilikuwa shilingi 1,480/= na bei ya juu ilikuwa shilingi 2,200/=.
Hata hivyo katika misimu yote miwili mfulululizo wakulima wameonesha kutoridhishwa na bei ambazo zimekuwa zikitajwa na wanunuzi, japo msimu 2023/2024 wakulima wamekubali kuuza Korosho katika mnada wa kwanza, tofauti na Msimu 2022/2023 ambapo baadhi yao waligoma na kulazimika kusubiri minada iliyofuata.
Akizungumzia mwenendo wa bei ya korosho katika Soko la Dunia Octoba 20, 2023 Wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara, Mkurungenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania Francis Alfred alieleza kuwa kumekuwa na kutetereka kwa bei ya zao hilo na umechangia kuathiri bei katika nchi ya Tanzania.
“Niwashukuru wa kulima kwa kufanya maamuzi haya kwa sababu bei hizi ambazo zimejitokeza ndio zile ambazo sisi kwa tathmini yetu tumekuwa tukifuatilia kwenye bei za kimataifa na zimetajwa kwenye minada yetu ya TANECU na MAMCU kwa msimu huu” alisema Francis na kuongeza kuwa
“Afrika Magharibi bei ya chini ni shilingi 1,650/= bei ya juu shilingi 1,980/=, kwa hiyo kwa bei walizouza wakulima wa Mtwara zipo juu kidogo ya zile ambazo zipo katika soko la kimataifa japo hawajaridhika lakini ndio uhalisia wa soko, na siku zinavyoenda bei inaweza ikaendelea kuimarika kutokana na mwenendo wa kidunia”
Pamoja na Bodi ya Korosho Tanzania kuelezea mwenendo wa biashara ya korosho katika soko la dunia wakati wa minada, bado wakulima wamekuwa wakilalamika kwamba bei zinazotolewa na wanunuzi ziko chini ikilinganishwa na matarajio yao.
Mmoja wa wakulima waliohudhuria mnada wa katika Kijiji cha Mburusa Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara Octoba 20, 2023 Mwanaisha Juma, alieleza kuwa walilazimika kuuza Korosho kwa sababu ya halihalisi ya soko waliyoisikia kutoka kwa wataalam waliokuwa kwenye mnada.
“Hii sio bei tuliyoitarajia lakini kwa maelezo yale yaliyotolewa ya mwenendo wa bei huko Duniani hata tukisema tusiuze tutazipeleka wapi wakati wanunuzi ni walewale? Alihoji Bi. Mwanaisha
Mkulima mwingine Ally Thabiti Maulana kutoka Wilaya ya Nanyumbu, anasema kuwa hawakuridhika na bei waliyouza korosho akiitaja kuwa ni ndogo na isiyo na maslahi kwa wakulima.
“Tunatumia gharama kubwa katika kilimo, bei ya Ufuta na Mbaazi ilikuwa nzuri tulitarajia na Korosho itakuwa hivyo ukizingatia na hadhi ya zao lenyewe lakini hali imekuwa tofauti sana na mbaya zaidi ni kuwa bei tumekuja kuzijulia mnadani hatuna cha kufanya imebidi tuuze tu” amesema Ally.
Maelezo haya kutoka kwa baadhi ya wakulima, ni kielelezo kuwa wengi wao wanakutana na bei ya Korosho mnadani wakiwa hawajui chochote kinachoendelea katika soko la Dunia, jambo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa upya.
Umefika wakati mamlaka zenye dhamana ya kusimamia Tasnia ya Korosho nchini kuanzia Wizara ya Kilimo, CBT na wadau wengine vikiwepo vyama vya ushirika na waandishi wa habari, kuhakikisha kuwa wanatoa elimu ya mwenendo wa soko lilivyo Duniani kabla ya kuanza kwa minada kama sehemu ya maandalizi ya msimu husika.
Hali hii itasaidia Mkulima kujua mwenendo wa bei ulivyo kabla hata hajapeleka Korosho Sokoni, hivyo kujiandaa na bei halisi ya soko la msimu husika na kupunguza malalamiko ya kutoridhishwa na bei baada ya mnada kwa sababu atakuwa alishajua hali ilivyo.
Ni ukweli usiopingika kuwa uzalishaji wa korosho duniani umekua ukiongezeka kila mwaka huku zaidi ya nchi 20 nyingi zikiwa barani Afrika zikitegemea kuuza Korosho ghafi katika masoko ya India na Vietnam pekee.
Uzalishaji wa korosho Afrika unatajwa kuongezeka kutoka tani 900,000 hadi 2.3 milioni katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022 zilizotolewa na Bodi ya Korosho Tanzania.
Kulingana na taarifa ya mwenendo wa soko la Korosho ghafi msimu 2022/2023 iliyochapishwa Octoba 24, 2022 kwenye tovuti ya Bodi ya korosho Tanzania www.cashew.go.tz Uzalishaji wa Korosho duniani umeongezeka kutoka wastani wa tani 1,400,000 kwa mwaka 2010 hadi kufikia zaidi ya tani 4,100,000 mwaka 2021, hivyo kuashiria ongezeko kubwa la korosho ghafi duniani ambalo kwa vyovyote lingeweza kuathiri bei katika msimu unaofuata.
Hadi mwaka 2022 Bara la Afrika pekee lilikuwa linazalisha asilimia 56 ya korosho zote ulimwenguni, huku ubanguaji ukiwa ni chini ya wastani wa asilimia 10, Hivyo kiasi kikubwa cha korosho ghafi inayozalishwa Afrika, hutegemea soko la India na Vietnam.
Je ni wakulima wangapi wa Tanzania wanayajua au wana uelewa wa mambo haya ya kidunia na wanajua kuwa yanahusika kwenye mjengeko wa bei ya Korosho wanazoazlisha katika maeneo yao?
Hii ndio sababu imefika wakati sasa wa kuelekeza elimu ya soko la Korosho kwa wakulima wa Korosho, kwa nguvu na kasi ileile inayotumika kuwaelemisha na kuwahamasisha wakati wa kulima, kupalilia, kupulizia na kuhifadhi.
Kama Mkulima anaelimishwa na kuhamasishwa kuhusu kulima, hakuna shida ya kuelemishwa pia juu ya hali ya soko ili kumsaidia kujipanga na bei za Korosho kwa wakati huo, badala ya kumsubiri akutane na bei siku yam nada.
Mkulima anapaswa kufamu kuwa, pamoja na kwamba Tanzania imekuwa ikijivunia kuuza korosho zake kwa bei ya juu ya wastani kutokana na ubora wa korosho zake; Athari, ya mwenendo dunia wa soko la korosho ulimwenguni katika mwaka 2023, tayari imejionesha katika minada iliyofanyika hadi sasa kwa msimu 2023/2024.
Kwa mujibu wa taarifa ya CBT iliyotolewa Octoba 2022, msimu wa 2021/2022 Tanzania iliuza korosho daraja la kwanza kati ya Tsh. 2,445 na Tsh. 1,750 kwa kilo katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2021.
Katika kipindi hicho cha msimu wa 2021/2022, bei za korosho katika soko la dunia zilikuwa kati ya dola 1,300 hadi 1,600 kwa tani ikilinganishwa bei ya kati 1,080 na 1,280 msimu 2022/2023, ikiwa ni bei za baada mzigo kuwa umenunuliwa na kufika aidha, India au Vietnam (CIF Price).
Hivyo bei zinazotokea msimu 2023/2024 za Tsh. 2,050 naTsh. 1,900 hazijapangwa na CBT, Vyama Vikuu vya Ushirika wala Serikali, bali ni bei zinazotokana na uhalisia wa soko lilivyo duniani ambalo wakulima wengi hata hawajui Soko la Dunia ni kitu gani.
Elimu ya soko kwa wakulima ni muhimu na itasaidia kupunguza lawama na minung’uniko wakati wa Msimu wa mauzo ya Korosho.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






