Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Komred Abdulrahman Kinana Akipokea tuzo ya pongezi kwa Kuchaguliwa kuendelea kuwa Makamu Mwenyekiti wa (CCM) Tanzania Bara kwa Mwenyekiti Ndg Marry Chatanda (Kushoto).
MWANDISHI WETU, DODOMA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amewataka viongozi wa CCM  wayaeleze kwa wananchi mambo mazuri yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kinana amesema hayo jijini Dodoma Machi 21, 2023, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya viongozi  wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya.
“Katika maeneo yenu hakikisheni mnakisemea Chama na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia, wala msione haya kusema ili wananchi wajue na hata katika chaguzi zijazo tusipate shida” ameeleza mzee Kinana
“Chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia katika kipindi cha miaka miwili kila kata kuna alama ya maendeleo kuanzia shule, zahanati, barabara na maendeleo ya watu, tuna kila sababu ya kujisifia na kuusifia uongozi wa mwenyekiti wa chama hiki.” amesema
Vilevile, Kinana amewataka viongozi wa UWT kubeba ajenda za wanawake kitaifa bila kuogopa jambo lolote.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Kinana amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili kufia lengo la kujenga jamii yenye usawa.
Amesema mwakani kuna uchaguzi wa viongozi wa serikai za mitaa, hivyo ni vyema wanawake wakajitokeza kuchukua fomu kuomba nafasi mbalimbali za uongozi na CCM itawapa ushirikiano wa kutosha.
“Kuelekea uchaguzi ujao jiandaeni na kuwahimiza wanawake kuwania nafasi zote za uongozi na ninawahakikishia kuwa, CCM itawaunga mkono kwa hali na mali ili kuwa na wanawake wengi waliochaguliwa katika majimbo,”amesema.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…