MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
mtwarapressclub@gmail.com

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt.Selemani Jafo amewataka vijana kutoka sehemu mbalimbali duniani kuinua sauti na kuelezea wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la hasara na uharibifu unaohusiana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amewataka vijana kuwa mabalozi wa kampeni ya nishati safi ya kupikia na teknolojia, kuendeleza usawa wa kijinsia kwa wanawake wa vijijini na vijana katika nchi zinazoendelea, na kuchukua jukumu la kuhamasisha mabadiliko.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ameyasema hayo 4 Oktoba, 2023 alipofungua Kongamano la pili la Kimataifa la Viongozi Vijana na Mabadiliko ya tabianchi (GLOBAL YOUTH CLIMATE SUMMIT) lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt. Jafo amesema kongamano hilo ni jukwaa la kipekee ambapo vijana wenye ujuzi tofauti wanakutana kwa lengo la kuongeza uelewa wao wa sayansi ya mabadiliko ya tabianchi, kukuza uongozi, na kutengeneza suluhisho zitakalopeleka kuzuia na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Adha Dkt. Jaffo amewataka washiriki wa kongamano hilo kubadilisha mtazamo wao kutoka kwenye utayarishaji wa nyaraka kuwa vitendo kwenye ngazi ya jamii.

Amepongeza Kituo cha Uongozi wa Vijana wa Kimataifa (Global Youth Leadership Center), kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu wa Tanzania (TFS) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa juhudi zao za kuwawezesha vijana na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za uchumi wa kijani na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu wa Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo amesema Kongamano hilo linalohudhuriwa na takriban washiriki 500 kati yao 200 wanashiriki moja kwa moja kutoka nchi 24 duniani na wengine 300 wanajiunga kwa njia ya mtandao linalenga kujenga uwezo wa vijana na kuwaandaa vijana viongozi katika mapambano ya mabadiliko ya tabianchi duniani.

“Tumechukua jukumu la kuwekeza kwa vijana kwa sababu vijana wanarithi matendo ambayo yalifanywa na warithi wetu na hivyo tunalizimika kuwaandaa sasa ili wayalinde mazingira na kuifanya dunia kuwa sehemu stahimilivu,” amesema Prof Silayo.

Naye Prof. Joel Nobert ambaye ni Mkurugeni wa Taasisi ya Rasilimali (Institute of Resource Assment) ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam anasema Kongamano hilo ni muhimu kwa vijana kwa kile alichoeleza kuwa linakwenda kuamua hatma ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi duniani.

Lucky Michael ni mshiriki wa kongamano hilo toka nchini anasema kupitia kongamano hilo watapaza sauti duniani kote kueleza athari za mabadiliko ya tabianchi ili kuifanya dunia kuwa sehemu salama.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…