BRYSON MSHANA, MTWARA

www.mtwarapressblog.co.tz

Disemba 3 ya kila mwaka ni siku ambayo ulimwengu huadhimisha siku ya watu wenye ulemavu

Hapa nchini Tanzania maadhimisho hayo  yalifanyika kitaifa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha Disemba 3,2022 na kuhudhuriwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Professa Joyce Ndalichako.

Waziri Professa Ndalichako aliyemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Mkoani Mtwara Kituo cha Upendo Rehabilitation kilichopo eneo la Magomeni katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ni moja taasisi zilizoadhimisha siku hiyo.

Sehemu ya wanafunzi na watu wengine waliojitokeza katika hafla ya maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu Duniani, iliyoandaliwa na kituo cha Upendo Rehabilitation Tarehe 3 Disemba 2022.

Maadhinisho hayo yalifanyika kwenye viwanja vya kituo cha Upendo Rehabilitation na kuwakutanisha watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali pamoja na wadau wengine, kwa lengo la kubadilishana mawazo.

Mkurugenzi wa Kituo hicho Bi.Christina Chacha, ameieleza Mtwara Press Blog kuwa wazo la kukusanya watu wenye ulemavu lilikuwa kuwapa nafasi ya kujumuika pamoja na kuadhimisha siku hiyo kwa pamoja.

“Tuliona kuwa tunaweza kuandaa kitu katika ngazi ya Wilaya hivyo tulifanikiwa kuwakusanya wanafunzi wenye ulemavu kutoka katika shule mbalimbali za kuanzia awali, msingi, sekondari na vyuo pamoja na watu wazima”

“Pia ilikuwa kuonesha mafanikio ambayo yamepatikana kwa mwaka mzima hapa kituoni kwetu, hivyo tuliungwa mkono na wadau wengine ikiwepo serikali kupitia ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mtwara, wananchi pamoja na vyama vya watu wenye ulemavu”

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mtwara BW. Thomas Salala, ni mmoja wa wageni waliohudhuria hafla hiyo akimuwakilisha mkuu wa wilaya hiyo Danstan Kyobya ambaye alisisitiza juu ya jamii kuwazingatia watu wenye ulemavu kwa kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Salala alieleza kuwa Serikali inatambua mchango wa watu wenye ulemavu katika kuleta maendeleo na kuupongeza uongozi wa kituo cha Upendo Rehabilitation kwa jinsi kinavyojitahidi kuwahudumia na kuwajali watoto wenye ulemavu.

“Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali katika kuwahudumia watu wenye ulemavu, na nichukue nafasi hii kuwapongeza Upendo Rehabilitation na niwasihi wadau wengine waendelee kuiga mfano huu” alisisitiza Salala.

Akizungumzia siku hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha watu wenye Ulemavu Mkoa wa Mtwara Bw.Abdullah Athuman Chiwaula, aliwakumbusha waajiri kufuata miongozo ya ajira kwa wetu wenye ulemavu.

“Ipo miongozo mbalimbali imetolewa juu ya ajira kwa watu wenye ulemavu, ni vema ikaendelea kufuatwa ili kuendelea kutoa fursa kwa watu wenye ulemavu kuajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini”

“Sera zipo na ni nzuri wala hazina shida, labda cha kusisitiza hapo ni namna ya kuharakishwa utekelezaji wa sera hizo kwa vitendo na zisibaki kwenye makaratasi tu” alisisitiza Bw. Chiwaula.

Siku ya wetu wenye ulemavu huadhimishwa Disemba 3 ya kila mwaka, na kaulimbiu ya mwaka huu (2022) ikiwa ni “Suluhu za mageuzi kwa maendeleo jumuishi: jukumu la uvumbuzi katika kuchochea ulimwengu unaopatikana na usawa.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa siku hiyo alisema ulimwengu unakabiliwa na msururu wa majanga ambayo yanaathiri watu wenye ulemavu hivyo kunahitajika kupatikane suluhu za mageuzi ili kuwezesha kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs na kutomwacha mtu yeyote nyuma.

Taarifa ya ujumbe wake huo iliyotolewa jijini New York Marekani imemnukuu Guterres akisema suala la mageuzi linahitaji ushirikiano mkubwa wa sekta ya umma na binafsi ili kuandaa mikakati ya pamoja kwakushirikiana na watu wenye ulemavu.

“Msingi wa ushirikiano huu lazima uwe na ushirikishwaji kamili wa watu wenye ulemavu ili uweze kujumisha utofauti wao katika michakato yote ya kufanya maamuzi. Ubunifu na teknolojia zinaweza kuwa zana zenye nguvu za kuwajumuisha” amesema Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Picha mbalimbali za hafla ya maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu Duniani, iliyoandaliwa na kituo cha Upendo Rehabilitation Tarehe 3 Disemba 2022.

 

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…