BRYSON MSHANA, DODOMA

mtwarapressclu@gmail.com

Waandishi wa Habari wametakiwa kujikita zaidi katika kufanya utafiti wa kihabari ili kupata undani wa taarifa na kuachana na kuandika habari zilizojikita upande wa viongozi pekee.

Rai hiyo imetolewa Desemba 08, 2023 jijini Dodoma na rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Deogratius Nsokolo, wakati wa ufunguzi wa tathmini ya mafunzo kwa viongozi wa klabu za Waandishi wa Habari Nchini.

“Ule uandishi ‘amesema’ zile table stories, si ndio mnafanya sana..! Ule umepitwa na wakati, kuendelea kuandika ‘amesema’ kamanda wa Polisi amesema, mkuu wa Mkoa amesema, sijui mkurugenzi wa taasisi gani amesema, unapoteza muda wako waachie wale waandishi wa mitandao weseme, mwachie mkurugenzi mwenyewe ata ‘Tweet’ kwenye nanii yake tutaona amesema nini..”

“Uandishi wetu ni wa umuhimu sana kwenye maendeleo ya nchi hii, ila uandishi wa amesema, amesisitiza, hauwezi kuwasaidia Watanzania hata siku moja.” Amesema Nsokolo.

Kufuatia rai hiyo ya Nsokolo, baadhi ya waandishi wa habari wamesema changamoto kubwa inayokwamisha kuandika habari za kina na utafiti ni kukabiliwa na hali ngumu ya kifedha, kwani kipato cha waandishi wengi hakikidhi mahitaji na kujikuta wanashindwa kufuatilia taarifa kwa kina.

“Suala la uchumi kwenye media bado sio zuri, kwasababu mtu anasubiri tu labda mkurugenzi, Mkuu wa Mkoa amuite, awalipie labda awasafirishe na vitu vingine watu waandike waondoke.” Amesema Lulu Samson, mwandishi kutoka mkoa wa Njombe.

FAtuma Maumba ambaye ni mwandishi kutoka Mkoa wa Lindi, amesema “hili tatizo linakuja kwasababu ya ugumu ama tunaweza tukasema kutokuwa na fedha ya kufikia kule kwa wananchi ili tukapata habari za wananchi kwasababu mnajua kabisa sisi waandishi wa habari sauti kubwa ya wananchi ni waandishi wa habari wanawategemea..”

Akijibia hoja hizo, Nsokolo amesema vyombo husika vinapaswa kuwagharamia waandishi wao katika kuwawezesha kuandika habari zenye tija.

“Kuna namna nyingine, sasaivi habari nyingi mwandishi akitaka kufanya zinafadhiliwa na taasisi mbalimbali, kama ni habari za afya na mwandishi amejikita kwenye habari za afya zitalipa tu na anaweza kufanya kutoka kwa wadau mbalimbali wa habari.” Amesema Nsokolo.

UTPC imewakutanisha viongozi wa klabu za waandishi wa Habari Tanzania Bara na Zanzibar jijini Dodoma katika tathmini ya mafunzo kwa viongozi wa klabu hizo, yatakayofuatiwa na maonesho ya utendaji wa klabu kisha Mkutano Mkuu wa wanachama.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…