BRYSON MSHANA, MTWARA

Usiku wa Tarehe 05 Mei 2025 ulikuwa wa kipekee na kihistoria katika Tasnia ya habari hapa Nchini, kufuatia utoaji wa Tuzo za umahiri kwa waandishi wa habari, Vyombo vya habari na wakongwe wa sekta ya habari zilizofahamika kwa jina la SAMIA KALAMU AWARDS 2025.

Tuzo hizi ziliandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikishirikiana na Chama cha waandishi wa Habari Wananwake Tanzania (TAMWA) katika hafla ya kufana iliyohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassana ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Hafla ya utoaji wa tuzi hizo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa the Super Dome Masaki Jijini Dar es slaam,ilihudhuriwa pia na Mawaziri, Manaibu waziri, Makatibu na Manaibu katibu wakuu kutoka Wizara mbalimbali, watendaji kutoka Tassisi za Serikali na binafsi, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, viongozi wa dini, Wanamuziki, Wasanii wa Maigizo na vichekesho, na waandishi wa habari.

SAMIA KALAMU AWARDS 2025, ni Tuzo zilizotolewa kwa wanahabari Watanzania kwa lengo la kuhamsisha, kuhimiza na kukuza wigo wa uchakataji na uchapishaji wa maudhui ya ndani kupitia vyombo vya habari yakiwepo magazeti, Redio, Televisheni na vile vya mtandaoni (Online Media).

Aidha utoaji wa Tuzo hizi zaidi ya 30 zilizoshirikisha kazi zaidi ya 1,000 zilizotumwa na wanahabari kutoka kote nchini, ulilenga kuchochea uandishi na utengenezaji wa maudhui ya ndani yaliyofanyiwa utafiti na uchambuzi kuhusu maendeleo ya nchi, uwajibikaji, uzalendo nan kujenga taswira chanya ya nchi.

Hizi ni Tuzo ambazo zimeiheshimisha sekta ya habari Nchini, kutokana na wazo na ubunifu mkubwa uliowekwa na waandaaji kuanzia kwenye hatua za awali mpaka siku ya utoaji wake, hali ambayo inazifanya kuwa za kipekee na za hadhi ya juu kuliko zingine zote ambazo zimewahi kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Pamoja na heshima kubwa iliyoletwa na tuzo hizi zilizokuwa na kauli mbiu ya “Uzalendo ndio ujanja”, lakini vilevile zimezidi kujenga motisha na kuongeza ari kwa waandishi wa habari nchini kuandika habari zinazoashiria kuleta na kuhamasisha maendeleo kwa Wananchi, kuchochea uwajibikaji, sambamba na kuhimiza uzalendo na mshikamano wa Taifa.

Tuzo hizi pia zimeleta hamasa mpya kwa wanahabari na vyombo vya habari kuongeza ushiriki kwa  kutuma kazi zao kwa wingi ili zishindanishwe katika shindano la mwaka unaokuja wa 2026, kutokana na mafanikio makubwa waliyoyaona mwaka huu wa 2025, jambo ambalo litapelekea mataifa mengine kuiga na kujifunza kwa yale yanaoyafanyika Tanzania kupitia sekta ya habari.

Katika kuipa hadhi na heshima halfa hiyo, Mhe.Rais Dkt.Samia suluhu Hassan alikabidhi tuzo mbalimbali kwa vyombo vya habari mahiri, wanahabari mahiri, wanahabari mahiri na chipukizi, huku akieleza kufurahishwa kwake kwa namna tukio hilo lilivyoandaliwa kwa utaribu wa TCRA na TAMWA na kusisitiza kuwa  wanapaswa kuliendeleza katika mwaka ujao wa 2026 na miaka inayofuata.

Mhe.Rais pia alisisitiza juu ya kalamu za waandishi wa habari kutumika vizuri kwa kuandika habari zisizoleta chuki na migawanyiko kwa jamii, ili kuhakikisha kuwa watanzania wanendelea kuwa wamoja hususana kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.

“Kalamu zilinde Nchi kueleka Uchaguzi Mkuu 2025, kalamu zikitumika vizuri tutakuwa salama. Lakinini zikitumika vibaya kutakuwa tofauti, niombe sana Kalamu zitumike kulinda nchi yetu na kuhimiza wananchi kushiriki Uchaguzi na kuchagua viongozi wazuri watakaotumikia” Amesisitiza Dkt.samia

Kwa maelezo haya yaliyotolewa na Mhe.Rais Dkt.samia suluhu Hassana, ni dhahiri kuwa Tuzo za uandishi wa Habari za Samia Kalamu Awards, zimetoa mwanga mpya kwa tasnia ya habari nchini na kuleta taswira mpya kwa wanahabari wanafanya shughuli zao katika vyombo mbalimbali vya habari.

Kwa upande wa waandaji wa Tuzo hizo Mamlaka ya mawasiliano Tanzania chini ya Mkurugenzi wake Mkuu Dkt.Jabiri Bakari wakishirikiana na Chama cha Waandishi wanawake Tanzania chini ya Mkurugenzi wake Dkt. Rose Rubeni wameingia kwenye kumbukumbu za wadau muhimu walioshiriki kuiheshimisha tasni ya habari kupitia SAMIA KALAMU AWARDS.

Ni Matumaini ya wadau kuwa maandalizi ya SAMIA KALAMU AWARDS 2026 yataanza mapema, na wadau wengine watajitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi hizi za TCRA naTAMWA, ili kuendelea kuiheshimisha Tasnia ya Habari Tanzania na kuzidi kuiweka katika viwango vya juu zaidi katiba Bara la Afrika na Ulimwenguni kwa ujumla.

Hizi ni tuzo ambazo zinapaswa kuenziwa kwa gharama yoyote ile, kwani zimebeba matarajio makubwa kwa wanahabari na mustakabali mwema wa wa Taifa lililo na wanahabari makini, weledi na wazalendo kwa nchi yao.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…