BRYSON MSHANA

mtwarapressclub@gmail.com

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan, ameongoza Kikao Maalum cha kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa leo tarehe 01April 2023 Ikulu Jijini Dar es salaam.

Katika kikao hicho, Kamati Kuu imezipongeza Serikali zote mbili za Chama Cha Mapinduzi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Rais Hussen Ali Mwinyi kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 kwa vitendo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa – Itikadi na Uenezi Sophia Edward Mjema Aprili 1, 2023 , Kamati  Kuu imepokea na kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kamati Kuu pia imepokea na kujadili Taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa mwaka wa fedha 2021/22, zilizowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni na kubaini kuwepo kwa maeneo ambayo taarifa zote mbili zimeonesha kuwa Serikali imeboresha na kuendelea kuimarisha kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwemo udhibiti na umakini katika matumizi ya fedha za umma, ambapo katika taasisi zilizokaguliwa, asilimia 96 zimepata hati safi.

Kamati Kuu katika mjadala huo wa kina, imesikitishwa na kuwepo baadhi ya maeneo mengine ambayo bado yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuondoa mapungufu/udhaifu uliobainishwa, ikiwa ni pamoja na mifumo ya malipo na ukusanyaji wa mapato kutokusomana.

Aidha Kamati kuu haijaridhishwa na kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu, hali inayosababisha serikali kukosa mapato na kupata hasara, uwepo wa mashirika ya umma yanayojiendesha kwa hasara na vitendo vya ubadhirifu wa mali na rasilimali za umma, kama vile kuongeza bei za manunuzi ya Serikali.

Kamati kuu imeipongeza Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa kufanya kazi zao kwa weledi na kuendelea kutimiza wajibu wao kwa taifa, kwa kuonesha maeneo ambayo Serikali imeyaboresha na kubainisha madhaifu yanayohitaji kufanyiwa kazi, kwa lengo la kulinda mali, rasilimali kwa maslahi ya taifa.

Kamati Kuu imeielekeza Serikali kuchukua hatua thabiti kwa wahusika wote waliobainika kuhusika katika ukiukaji wa sheria na kusababisha ubadhirifu wa mali na rasilimali za nchi.

Halikadhalika, imetoa maelekezo kwa Serikali kuwafuatilia watu wote wanaotumia dhamana za uongozi vibaya na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele katika nafasi walizoaminiwa kutumikia watu, badala yake wanaweka maslahi binafsi.

Aidha, Kamati Kuu ya CCM, imeipongeza Serikali kwa kuratibu na kufanikisha vema ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Harris Kamala aliyetembelea nchi yetu kwa siku tatu.

Ziara hiyo imeongeza uimara wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kufungua milango zaidi ya mahusiano yenye faida kwa maendeleo na ustawi kwa pande zote mbili, hususan katika maeneo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kukabiliana na magonjwa, uchumi, uwekezaji na ajira.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…