BRYSON MSHANA, TABORA

mtwarapressclub@gmail.com

Wawakilishi kutoka visiwani Zanzibar, Timu ya mpira wa Kikapu Wavulana Kanda ya Pemba wametwaa Ubingwa kwenye Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) yanayoendelea Mkoani Tabora.

Pemba imeibuka na ushindi baada ya kuifunga Dar es salaam Vikapu 51 – 49 katika mchezo mkali na wa kusisimua uliochezwa kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari Tabora Wavulana Tarehe 12 Juni 2023, ukianza Saa 3:30 Asubuhi.

Wakicheza kwa kujiamini vijana wa Dar es salaam walianza vizuri na kuongoza mchezo huo, kabla ya Pemba kurudi mchezoni na kuchukua uongozi uliowafanya kumaliza kwa kupata ushindi na kufuta machozi ya mchezo wa awali wasichana ambao Pemba ilifungwa na Arusha.

Kocha wa Timu ya Pemba Aboubakar Msabaha, amesema walicheza vizuri wakati wote na walistahili ushindi dhidi ya timu ngumu ya Dar es salaam, akiongeza kuwa ushindi huo ni heshima kwa Pemba na Zanzibar kwa ujumla.

“Wewe mwenyewe umeona game ilivyokuwa, vijana wamecheza vizuri mchezo ulikuwa wa ushindani mkubwa, Dar es salaam ni wazuri hivyo walitupa changamoto kubwa, haya sio matokeo ya kubahatisha yametokana na juhudi, la sivyo tungepoteza hapa”

Ushindi huo wa Pemba wavulana, unahitimisha mchezo wa mpira wa Kikapu katika mashindano ya UMITASHUMTA 2023 ambayo yanafanyika Mkoani Tabora kwa mwaka wa pili mfululizo.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…