LUCY MWALONGO, NAMTUMBO

Katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, Jimbo la Namtumbo limepiga hatua kubwa na ya kuigwa katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Mafanikio haya yamesimamiwa kwa ukaribu na Mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Vita Rashid Kawawa, ambaye pia amejitosa tena kuwania nafasi hiyo kwa kipindi cha 2025–2030.

Kupitia ushirikiano wa karibu kati ya Mbunge, Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita, madiwani, wenyeviti wa vijiji na viongozi wa chama, miradi ya afya yenye thamani ya takribani Shilingi Bilioni 8.48 imetekelezwa, Hatua hizo ni mwitikio wa moja kwa moja wa maagizo ya Ilani ya CCM (Sura ya 3, Ibara ya 83) ambayo inaelekeza kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kila Mtanzania.

Katika kipindi hiki, jumla ya zahanati 15 zimejengwa katika vijiji mbalimbali vya jimbo hilo, Hii imechangia kupunguza umbali wa wananchi kufuata huduma za afya, hivyo kuokoa maisha na muda wa uzalishaji.
Vituo vya afya viwili pia vimejengwa na kuboreshwa kwa vifaa na miundombinu ya kisasa.

Mbali na hayo, nyumba za watumishi wa afya (waganga) zimejengwa, sambamba na uboreshaji wa mifumo ya vyoo na maji katika vituo vya kutolea huduma,Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo imejengewa majengo mapya pamoja na wodi za mama na mtoto, hatua ambayo imesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya uzazi.

Katika kuhakikisha huduma bora zaidi, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, na magari ya kubebea wagonjwa (ambulance) umeboreshwa kwa vituo mbalimbali vya afya. Pia, Mhe. Kawawa alifanikiwa kuleta madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), walioweka kambi maalum na kutoa huduma za kibingwa katika Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo, Kituo cha Afya Mtakanini, Lusewa na Mputa.

Aidha, Mbunge huyo ameshiriki kwa vitendo katika kuhakikisha vifaa tiba, mashine za usingizi, na vitanda vya kisasa vinapatikana katika vituo vya afya. Kwa kufanya hivyo, amedhihirisha utekelezaji wa ahadi za Ilani ya CCM kwa vitendo, akisimama imara kama sauti ya wananchi.

Kutokana na mafanikio haya makubwa, Mhe. Kawawa amejitosa tena kuomba ridhaa ya wananchi wa Namtumbo kwa kipindi cha 2025 hadi 2030 ili aendelee kuwatumikia kwa moyo wa kizalendo na kuendeleza kazi nzuri iliyoanzishwa.

Katika kinyang’anyiro cha ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Kawawa anakabiliana na ushindani kutoka kwa watia nia wengine wanne waliopitishwa na Kamati Kuu ya CCM, huku akielezwa na wachambuzi wa kisiasa kuwa na nafasi nzuri kutokana na rekodi yake ya utendaji.

Orodha ya Watia Nia Ubunge – Jimbo la Namtumbo (CCM 2025):

1. Dkt. Juma Zuberi Homera

2. Dkt. Sharif Hassan Ngonyani

3. Vita Rashid Kawawa (Mbunge wa sasa)

4. Mussa Kassim Chowo

5. Shaibu Hamisi Majiwa

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…