BRYSON MSHANA, MTWARA

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limeeleza kuwa limefungua dirisha la udahili awamu ya pili kwa kozi za Afya na sayansi Shirikishi, ngazi ya Astashahada na Stashahada kuanzia Tarehe 25 Julai hadi 28 Agodti 2025.

Kwa mujibu wa Meneja wa NACTVET Kanda ya kusini Ndg.Claus Lugome udahili huo unafuatia kumalizaka kwa ule wa awamu ya kwanza ulioanza Mei 28 na kufungwa tarehe 11 Julai 2025 na kueleza kuwa maombi ya kozi ya Afya na Sayansi shirikishi kwa Tanznaia Bara, yatafanyika kupitia  mfumo wa udahili wa pamoja (Central Admission System) kwenye tovuti ya Baraza (www.nactvet.go.tz).

Ameongeza kuwa kwa kozi za Afya na Sayansi Shirikishi zitatolewa katika vyuo vilivyoko Zanzibar, na maombi yake yatatumwa moja kwa moja kwenye vyuo husika sambamba na maombi kwa kozi zisizo za Afya na Sayansi shirikishi pia yatatumwa moja kwa moja kwenye vyuo husika.

Lugome amesema hayo Tarehe 7 Agosti 2025 wakati aliposhiriki kwenye mahojiano katika Kipindi cha Safiri Nasi kinachorushwa na Kituo cha Safari Radio, ambacho pia kilishirikisha wadau wengine wa wanaohusika na mikopo ya elimu ya juu ikiwepo Benki ya NMB, HESLB na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

“Waombaji wanapaswa kusoma na kuelewa maelekezo katika kitabu cha Mwongozo wa Udahili kwa mwaka wa masomo 2025/2026, kitabu hiki kitamwongoza mwomaji kufahamu vyuo, program zinazotolewa katika vyo hivyo, vigezo katika program husika, gharama za masomo nk.”

“Udahili ufanywe na mwanafunzi mwenyewe, na endapo atahitaji usaidizi ahakikishe taarifa zinazojazwa kwenye mfumo ni za kwake, vilevile mwombaji ahakikishe namba ya simu na barua pepe anayotumia ni yake binafsi, na akumbuke kutunza taarifa zake na kuepuka kuzitoa mfano namba ya mtihani ya kidato cha Nne na namba ya simu kwenye chuo asichokusudia kujiunga” amesisitiza Lugome

Baraza la Taifa la ElImu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) ni chombo kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 129 pamoja na mapitio yake Na. 4 ya mwaka 2021 kwa madhumini ya kusimamia Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi stadi hapa nchini.

Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, inamaanisha mafunzo yatolewayo kwa mwanafunzi kwa lengo la kumpatia Ujuzi na stadi ili kumuwezesha kufanya kazi katika fani husika.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…