BRYSON MSHANA, TABORA

mtwarapressclub@gmail.com

Mkoa wa Mtwara ambao ni Mbingwa watetezi wa mpira wa Wavu Wasichana, wamefanikiwa kutetea Ubingwa katika Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) yanayoendelea Mkoani Tabora.

Matokeo haya yameipelekea Mtwara kuchukua Ubingwa mfululizo tangu mwaka 2003 na kuweka historia ya kipekee katika michezo ya UMITASHUMTA.

Katika mchezo wa fainali uliochezwa Tarehe 12 Juni 2023 majira ya saa nane mchana kwenye viwanja vya shule ya sekondari Tabora Wavulana, Mtwara iliishinda Manyara kwa Seti 3-0.

Kocha wa Timu ya Mtwara Gabriel Joshua, ameelezea furaha yake baada ya ubingwa huo wa kihistoria, akisema kuwa siri ya mafanikio ni kujituma kwa wanafunzi na kufuata maelekezo kutoka kwa waalimu.

Amesema Kuna vipaji vingi vya mpira wa Wavu nchini ambavyo vinakosa nafasi ya kufundishwa vizuri, na kuwaomba wadau wa michezo kuwekeza kwenye eneo hilo ili kusaidia kuwa na timu imara ya Taifa katika siku zijazo.

“Mtwara tunajivunia ubingwa huu, tumekuwa tukiushinda mara kwa mara na hata mwaka huu tulijua tutashinda tu maana hatukuona wa kutuzuia, hata ukiwauliza waalimu kutoka mikoa yote hapa watakuambia hili ni Kombe la Mtwara”

“Kikubwa hapa niwadau wa mpira wa Wavu nchini kujitokeza zaidi kuwekeza hususan kwa vijana kama hawa ili kuhakikisha kuwa vipaji vyao havipotei kwani hawa ni hazina kubwa ya Taifa kwa baadae” amesema Mwl. Joshua

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…