JUMA MOHAMED, MTWARA
mtwarapressclub@gmail.com
Mbunge wa Mtwara Mjini Hassan Mtenga, amesema kwa takribani miaka Minne, ya ubunge wake, akaunti ya Manispaa ya Mtwara Mikindani haijawahi kuwa na pesa inayofikia shilingi Milioni 60.
Mtenga amezungumza hayo Januari 01, 2024 katika mkutano wake na waandishi wa Habari, akielezea miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa ndani ya jimbo lake kuanzia mwaka 2020 alipochaguliwa kuwa Mbunge.
Katika maelezo yake, Mtenga akagusia utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mwalimu Hassan Nyange, ambaye amepokea kijiti kutoka kwa Kanali Emmanuel Mwaigobeko takribani miezi Mitatu iliyopita.
“Toka naingia mimi kuwa Mbunge kwenye jimbo hili, hatujawahi sisi kwenye akaunti ya manispaa kuwa na hata Milioni 60, hatujawahi toka 2020/21 mpaka hapa Nyange anaingia.”
Amesema Mkurugenzi Nyange wakati anaingia Manispaa iliikuwa na shilingi Milioni 5.757 kwenye akaunti yake, kabla ya makusanyo kuanza kuongezeka hadi kufikia Bilioni 1.5 zilizokusanywa kwa muda wa wiki Tano.
Kuhusu miradi ya maendeleo, Mtenga amesema ndani ya awamu ya Sita jimbo la Mtwara mjini limepata mafanikio makubwa ya zaidi ya asilimia 90 kwa utekelezaji wa miradi na utatuzi wa migogoro ya ardhi.
“Tulianza na barabara ya Mkanaledi pana kilometa Moja pale zaidi ya Milioni 500 tumetengeneza kwa barabara ya lami, lakini tuna barabara sasahivi tunatengeneza kata ya Likombe, na barabara ile mpaka kwisha itachukuwa zaidi ya kilometa 5-6 lakini niwaahidi tu wananchi wa kata ya Likombe barabara ile tutaunganisha kwa lami mpaka barabara inayokwenda Ziwani.” Amesema Mtenga.
Wakitoa maoni yao juu ya Mbunge wao, baadhi ya wakazi wa Mtwara mjini akiwamo Jabir Shaffih ambaye amemtaka Mbunge kujitokeza kwa wananchi ili iwe rahisi kumfikishia kero zao, huku Isihaka Bakari akilalamikia ubovu wa baadhi ya barabara za ndani ya mji.
“Mbunge ajitahidi kujitokeza sehemu za watu, ajitokeze sehemu za watu ili tumjue yeye asidhani kama anavyojenga vibanda vya Bodaboda vile anahisi kama amemaliza, kuna vitu vingi sana wananchi wanavyo.” Amesema Jabir.
Isihaka Bakari naye akaeleza kuwa “sisi malalamiko yetu makubwa ni kwenye barabara kwamfano ukija hii barabara ya Coco Beach kutoka kwa Jionee mpaka TTC, barabara ina viraka utafikiri unacheza bao yani..”
Tanzania inaingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu wa 2024, kabla ya kufanya uchaguzi Mkuu mwaka ujao wa 2025.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






