HASSAN MABUYE, DODOMA

www.mtwarapressblog.co.tz

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda amesema kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa utendaji wa Sekta ya Ardhi kwa watumishi walioko katika Halmashauri mbalimbali nchini.

Pinda amesema kwa muda mfupi aliokaa Wizarani amegundua kuwa kuna changamoto hiyo kutokana na mamlaka za kupanga na kumilikisha ardhi kuwa katika Halmashauri husika wakati mwajiri wa wataalam hao ni Wizara ya Ardhi jambo lilopelekea uwepo kwa changamoto hii.

Amesema hayo Machi 11, 2023 Jijini Dodoma wakati wa Kikao kazi cha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eng. Anthony Sanga pamoja na Makamishna Waasaidizi wa Miko na Waratibu Mikoa.

Ametumia fursa hiyo kuwataka viongozi hao kuwasilisha maoni ili sheria ya ardhi iweze kuboreshwa katika mapitio ya sheria yaliyoko kwenye mchakato.

Aamesema ipo haja ya kupitia muhundo upya wa watumishi hao ili ikiwezekana waweze kuwajibika kinidhamu kwa Kamishna Msaidizi wa Mikoa ili kuongeza uwajibikaji kiutendaji ili kusaidia Kamishna huyo kutekeleza kazi zake ipasavyo.

Suala lingine alilogusia kiongozi huyo nikuhimiza uwajibikaji wa pamoja wa watumishi walioko katika ofisi za mkoa bila kujali kada zao kwani wote kwa pamoja wanafanya kazi  katika Sekta ya Ardhi hapa Nchini.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Eng. Anthony Sanga aliwambia watendaji hao kuwa kipaumbele chake ni kuongeza makusanyo ya kodi ya ardhi na kwamba yeye kila atakapita katika Ofisi za Ardhi Mkoa ataomba kupatiwa takwimu za makusanyo ya kodi ya pango la Ardhi.

Katibu Mkuu Sanga ameongeza kuwa tayari timu ya wataalam wa Tehama na wengine wako kazini kutengeneza mfumo mpya na rafiki utakaowawezesha watanzania kulipa kodi ya ardhi kupitia miamala ya simu tofauti na sasa ambapo wananchi wanalazimika kupanga foleni katika Ofisi za Wizara Mikoani kwa ajili ya kulipa kodi.

Amewataka waratibu wa Kodi Mikoani kote kuwa na takwimu sahihi za walipa kodi ikiwemo kuwatambua wote ikiwemo wale ambao hawajarasimisha ardhi yao ili waweze kuingiza katika mfumo wa walipa kodi kama ilivyo katika miamala ya Mamlaka za maji hapa Nchini.

Amesema timu ya wataalam tayari iko kazini ikifanyia kazi mfumo wa ukusanyaji mapato ambao utakuwa ni wa aina moja nchi nzima tofauti na sasa ambapo mifumo ya ukusanyaji mapato inatofautiana kati ya mkoa mmoja na mwingine suala ambalo amesema litaongeza kasi ya makusanyo ya maduhuli ya serikali kupitia Pango la Ardhi.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi anakutana na Makamishna wa Ardhi Nchini pamoja na Waratibu wa Kodi kutoka Ofisi za Wizara ya Ardhi walioko mikoa yote ya Tanzania kwa lengo la kupeana taarifa likini pia kukumbushana masuala muhimu ikiwemo yatakonayo na Mkutano wa awali uliowakutanisha mjini Morogoro hivi karibuni. 

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…