BRYSON MSHANA, MTWARA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limepokea boti ya kisasa ya doria kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya Bahari ya Hindi, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuimarisha vikosi vya usalama baharini.
Boti hiyo ni miongoni mwa boti 11 zilizotolewa kwa mikoa mbalimbali nchini, zenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 4.5, kupitia juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan. Lengo ni kuhakikisha kuwa mipaka ya nchi inalindwa ipasavyo dhidi ya uhalifu wa baharini kama vile uvuvi haramu, magendo, usafirishaji wa dawa za kulevya na uhamiaji haramu.
Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya boti hiyo katika Bandari ya Mtwara, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo ya kupeleka vitendea kazi muhimu kwa Jeshi la Polisi, hasa katika ukanda wa kusini mwa Tanzania.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kutupatia boti hii ya kisasa, Itatusaidia sana katika kupambana na uvuvi haramu, biashara ya magendo, pamoja na usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia baharini. Hii ni hatua kubwa kwa Mkoa wetu wa Mtwara,” alisema Mhe. Sawala.
Aidha Kanali Sawala ametoa wito kwa maafisa wa Jeshi la Polisi na wadau wote kuhakikisha kuwa boti hiyo inatunzwa kwa umakini na kuwahudumia wananchi kwa weledi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji Tanzania, SACP Moshi Sokoro, akizungumza kwa niaba ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillus Wambura ametoa shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa kwa ajili ya vikosi vya ulinzi na usalama.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






