BRYSON MSHANA, MTWARA
Taasisi ya Door of Hope Tanzania yenye Makao yake Makuu Mkoani Mtwara, imewaomba wadau mbalimbalimbali kujitokeza na kuunganisha nguvu kwa pamoja katika kuzuia vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kushika kasi mkoani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Door of Hope Bw. Clemence Mwombeki ameeleza hayo Disemba 18, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Taasisi zilizopo Mtaa wa Shangani Mashariki Mjini Mtwara, na kusema kuwa kumeendelea kushuhudiwa vitendo vilivyokithiri vya ukiukwaji wahaki za binadamu na ukatili kwa wanawake na watoto katika mikoa ya Mtwara na Lindi.
“Pamoja na jitihada za wananchi kuripoti, Serikali kuchukua hatua na wadau kuendeleza utekelezaji wa afua mbalimbali za kuzuia na kupambana na vitendo hivi, siku za hivi karibuni tumeshuhudia ongezeko kubwa la vitendo hivi”
“Kuendelea kwa hali hii kunahatarisha uhai na usalama wa baadhi ya makundi ya pembezoni hususani wanawake, watoto pamoja na watu wenye ulemavu, zaidi kuzorotesha ushiriki wao kwenye uchumi na shughuli nyingine za ustawi wao binafsi na Taifa” ameongeza Mombeki
Amesema katika ufuatilia mwenendo wa matukio mbalimbali, wamegundua kuwa wahanga ni wanawake na wattoto wa kike na wa kiume kwenye kesi za ubakaji, ulawiti na vipigo hadi kuuwa kwa wanawake, watoto wa kike kubebeshwa mimba, watoto wa kiume kulawitiwa.
Katika kukabiliana na vitendo hivyo, amependekeza wadau, jamii na Serikali kuongeza nguvu kwenye utoaji wa elimu kwa umma kutokana na kubaini kuwa asilimia kubwa ya wanaofanyiwa vitendo vya ukatili hawana ufahamu wa kutosha juu ya haki zao.
Vilevile amependekeza kuwa mifumo iliyopo kwa sasa itumike kikamilifu kusimamia haki,kuongeza ushiriki sawia wa makundi ya kijamii, utatuzi wa migogoro na migongano kwenye jamii ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha viongozi mbalimbali ngazi ya vijiji, viongozi wa dini, kimila na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii.
Taarifa hii ya Door of Hope imekuja ikiwa ni takriban juma moja kupita, tangu kukamilika kwa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili nchi, ambayo kimkoa ilihitimiohwa Wilayani Masasi Disemba 10, 2023 ikihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya anyumbu Dkt. Stephan Isaac Mwakajumilo, aliyemuwakilisha Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas.
Katika hotuba yake, Dkt. Mwakajumilo alisema vitendo vya ukatili wa kinjisia katika Mkoa wa Mtwara vimezidi kuongezeka kwa kipindi cha mwezi Januari mpaka Septemba 2023, ambapo jumla ya matukio 1,120 yaliripotiwa dawati la jinsia.
Kampeni ya siku 16 za kupinga Ukatili iliandaliwa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mtwara chini ya Mtandao wa MTWANGONET kwa kushirikiana na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mtwara, ikiwa na kauli mbiu ya isemayo “Wekeza Kuzuia Ukatili Wa Kijinsia”
Kampeni hiyo ilizinduliwa Novemba 25, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa Kanal Ahmed Abbas.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






