BRYSON MSHANA, MTWARA
mtwarapressclub@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamis Munkunda amewapongeza wanunuzi wanaoendelea kujitokeza kununua Korosho za Tanzania msimu 2023/2024, kuwa hiyo ni ishara njema ya kukubalika na kuaminika kwa Tanzania katika biashara za kimataifa.
Mkuu huyo wa Wilaya ametoa pongezi hizo Octoba 27, 2023 wakati akitoa salamu za Serikali kwa wakulima wa Korosho waliojitokeza kushuhudia mnada wa pili wa zao hilo uliofanyika katika Kijiji cha Madimba Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
DC Munkunda ameeleza kuwa idadi kubwa ya makampuni yaliyojitokeza kuomba kununua Korosho msimu huu, ni ushahidi tosha juu ya ubora wa Korosho inayotoka Tanzania hususan Mikoa ya kusini, hivyo wakulima wanapaswa kuendelea kuelimishwa juu ya kudhibiti ubora ili kuendelea kuvutia wanunuzi zaidi.

Wakulima wa Korosho waliojitokeza kushuhudia mnada wa pili wa zao hilo uliofanyika katika Kijiji cha Madimba Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Octoba 27, 2023 (PICHA NA MAHMOUD ISSA)
“ Nawapongeza sana wanununzi hawa kupitia kampuni zao ambazo nimesikia hapa kuwa ni zaidi ya 100 na wengine wanaendelea kuulizia taratibu za kupata vibali vya ununuzi, wametoka katika maeneo mbalimbali duniani, hii inazidi kuitangaza nchi yetu na kuvutia wawekezaji wengine kuja kwetu kuwekeza kwenye sekta nyingine”
“Sasa kwa hali hii hatupaswi kuishia hapa, amani hii tunayopewa na wanunuzi ni kubwa haipaswi kuondoka, na njia pekee ni kutunza ubora wa korosho ili tuzidi kuwavutia wanunuzi waje kununua Korosho Tanzania kama kituo chao cha kwanza kabla hawajafikiria maeneo mengine” amesema Mkuu wa Wilaya

Baadhi ya Wakulima waliowakilisha wenzao wakati wa ufunguzi na ukaguzi wa barua zilizowasilishwa na wanunuzi, zenye maombi ya kununua korosho kupitia mnada uliofanyika katika Kijiji cha Madimba Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Octoba 27, 2023. (PICHA NA MAHMOUD ISSA)
Awali akizungumza katika mnada huo muwakilishi kutoka Bodi ya Korosho Tanzania Bw. Revelian Ngaiza aliwaomba wakulima kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya masoko duniani ambazo zimekuwa zikiwasilishwa minadani.
Ngaiza ambaye ni Mkurugenzi wa Masoko na Udhibiti Ubora wa CBT, alieleza kuwa mwenendo wa soko la Korosho Duniani umekuwa wa kupanda na kushuka kutokana na mahitaji katika nchi zinazonunua Korosho, na wao kama wataalam wameendelea kufuatilia kila kinachotea kwa ajili ya kuwajulisha wakulima.
Amewaeleza Wakulima kuwa ni jukumu la Bodi ya Korosho Tanzania kuhakikisha kuwa inafuatilia mwenendo wa bei za Korosho zinavyoenda katika maeneo tofauti duniani, na kuziwasilisha kwa wakulima katika uhalisia wake bila kupunguza wala kuongeza.
“CBT ipo kwa ajili ya kumlinda Mkumlima wa Korosho nchini, hilo linaenda sambamba na ufuatiliajai na utoaji wa taarifa za halihalisi ya masoko ilivyo, na siku zijazo tunaenda kuimarisha sana eneo hili la taarifa za masoko kwa mkulima” amefafanua Ngaiza.
Aidha kwa upande wa Wakulima waliohudhuria mnada huo wameeleza kuzipokea bei zilizowasilishwa na wanunuzi na kukubali kuuza Korosho zao kulingana na hali halisi ya soko la Korosho Duniani ilivyo kwa sasa.
“Hakuna namna unaweza kuacha kuuza Korosho kwa bei hii, wote tumewasikia wataalam hapa wakisema akiwepo Mwenyekiti wetu wa Chama Kikuu naye amesema juu ya hali ya bei ilivyo, hivi ndivyo biashara zilivyo, kuna wakati bei zinapanda na kushuka, mwaka huu hizi ndii bei zilizopo sokoni hivyo tunauza Korosho tuangalie minada ijayo itakuwaje” amesema Abdallah Mkani Mkulima kutoka Kijiji cha Madimba.
Katika mnada huo zaidi ya Tani elfu 12 za Korosho ziliuzwa kupitia Chama kikuu cha Usiririka Masasi-Mtwara-Nanyumbu (MAMCU LTD), bei iliyofikiwa na wanunuzi ikiwa ni Shilingi 2,070 kwa kilo moja, ambayo ni bei ya juu, na bei ya chini ikiwa shilingi 1,920
Zaidi ya kampuni 50 ziliwasislisha maombi ya kutaka kununua korosho zilizohifadhiwa katika maghala mbalimbali ya Mtwara,Masasi na Nanyumbu.
WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE
MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…






