BRYSON MSHANA, MASASI

mtwarapressclub@gmail.com

Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mkoani MtwaraLauteri Kanoni , imesesema wanajipanga kuanza msako kwa wanafunzi watakaokuwa hawajaripoti shuleni na wazazi wenye wanafunzi waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza katika shule mbalimbali za Sekondari wilayani humo ifikapo Januari 15, 2024.

Amesema hayo Januari 10, 2024 wakati alipofanya ziara katika shule mbalimbali za Sekondari katika Halmashauri ya Masasi, kujionea mwenendo wa wanafunzi walioripoti na kuanza masomo tangu shule zifunguliwe rasmi Januari 8, 2024.

DC Kanoni amesema kuwa Serikali ilishakamilisha maandalizi yote muhimu kwa ajili ya wanafunzi wapya ikiwa ni pamoja na kuongeza shule mpya katika maeneo ambayo watoto walikuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata shule, hivyo jukumu lillilobaki sasa ni kwa wazazi kupeleka watoto wakasome.

“Serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya kukuza na kuendeleza elimu ya Sekondari katika Wilaya ya Masasi, leo pekee tumetembelea shule tatu mpya za Sekondari na moja ya Msingi zilizojengwa kwa ajili ya kuwarahisishia watoto wetu kupata elimu, hivyo niwasisitize wazazi kuwa hawana sababu ya kutowapeleka watoto shule”

“Iwapo ikifika Jumatatu tarehe 15 Januari mtoto aliyepangiwa shule hajaenda kuanza masomo, basi taratibu zingine za kisheria zitafuata ikiwa ni pamoja na kuanza msako wa kuwakamata na kuwafikisha mahali panapohusika” amesisitiza DC Kanoni

Kuhusu changamoto za Sare na Madaftari ambazo zimekuwa zikielezwa kuwa ni sababu za watoto wengi kutoripoti shule, Mkuu wa Wilaya amewataka kuripoti shuleni kwa kutumia nguo za kawaida walizo nazo wakati taratibu zingine zikiendelea.

Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Masasi Bw. Lusekelo Mkumbwa amesema waalimu wote wapo tayari kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi kwenye shule walizopangwa kwa ajili ya kuendelea na masomo.

“Tarayari wanafunzi ambao walisharipoti wameshaanza masomo, kiwango cha wanafunzi walioripoti bado ni kidogo iklinganishwa na walioandikishwa, tunaendelea kuunganisha nguvu na watendaji wa kata ili watusaidie kuhamasisha watoto waletwe shule wasome maana waalimu wapo wanawasubiri wao tu” ameeleza

Naye Diwani wa Kata ya Chikunja Halmashauri ya Masasi Samoni Mpili ameahidi kuanza kupita nyumba kwa nyumba katika kata yake akishirikiana na watendaji wengine, kwa ajili ya kutoa msukumo kwa wanafunzi kwenda kuanza shule.

Shule ya Sekondari chikunja ni moja ya zile ambazo wanafunzi waliopangwa bado hawajaripoti, ikiwa ni wanafunzi 25 tu walioripoti kati ya 100 walioandikishwa kuanza kidato cha kwanza shuleni hapo.

Shule zingine zilizotembelewa na Mkuu wa Wilaya ni Mpeta Sekondari inayotarajia kupokea wanafunzi 83 (wasichana 50, Wavulana 33) hadi sasa wakiwa wameripoti wanafunzi 7 pekee, na Shule ya Sekondari Metesa inayotarajia kupokea wanafunzi 64 (wasichana 29, Wavulana 35, huku walioripoti mpaka sasa wakiwa ni 19 pekee kati yao 11 wakiwa ni wasichana na 8 wavulana.

Shule nyingine ni Chikolopola Sekondari ambayo jumla ya wanafunzi waliopangwa ni 163, (Wasichana 82 wavulana 81) ambao hadi kufikia January 10 walioripoti ni 20 pekee, wasichana 10 na wavulana 10.

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…