SALMA MKALINALA, MTWARA

mtwarapressclub@gmail.com

Watu watatu wamefariki dunia, na wengine wanne kujeruhiwa, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuligonga kwa nyuma lori lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara ya Mtwara-Lindi mkoani Mtwara, baada ya kupata hitilafu na kisha kuigonga pikipiki.

Akitoa taarifa ya ajali hiyo lOktoba 30, 2023 kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara, ACP Mtaki Kurwijila amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa 5:50 usiku, ikihusisha gari aina ya Toyota Alphad yenye namba za usajili T404 EDB ambayo iliigonga lori la kampuni ya Dangote Cement yenye namba za usajili T 203 DKB aina ya Howo Truck, na pikipiki aina ya TVS ambazo namba zake hazijatambulika.

ACP Mtaki amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva wa gari ndogo na kushindwa kuchukua tahadhali ya kutosha barabarani, na jeshi la polisi mkoani hapa linamsaka dereva wa gari hiyo ambaye ametokomea kusikojulikana baada ya kutokea ajali.

Amewataja waliofariki kuwa ni Mwanaidi Seleman Ahmad (51) na Niale Ally (32) ambao ni wamakonde na wakazi wa Magomeni, Manispaa ya Mtwara pamoja na Mohamed Mfaume Mtumanuma (60) Mmakonde, mkazi wa Ziwani, halmashauri ya Mtwara.

Miili ya marehemu hao ilifanyiwa uchunguzi  katika hospitali ya Kanda ya Kusini mkoani hapa na kukabidhiwa kwa ndugu na baadhi yao wamezikwa majira ya saa saba mchana, makaburi ya Mangowela, na majeruhi wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo ya Kanda

Check Also

WANANCHI WA MABOGINI WANUFAIKA NA MRADI WA RISE

MOSHI-KILIMANJARO Wananchi wa kijiji cha Mabogini, kata ya Mabogini, wilayani Moshi Mkoani…